Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, June 20, 2017

Indhari ya viongozi wa Kiafrika kuhusu mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Rais Joseph Kabila
Machafuko yaliyozuka DRC kulalamikia kubakia madarakani Rais Kabila
Sambamba na kuendelea mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuendelea kutolewa miito ya kuzuia kuchukua mkondo mpana zaidi mgogoro wa nchi hiyo, Kofi Annan Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na Marais kadhaa wa zamani wa nchi za Afrika wametoa indhari wakieleza kwamba, hali ya nchi hiyo ni mbaya na hivyo wametaka kutumiwa njia za amani kuinasua nchi hiyo na mgogoro huo.
Mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekuwa ukishuhudiwa kwa muda sasa na ulianza baada ya kuakhirishwa uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo. Kwa mujibu  wa Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, muhula wa uongozi wa Rais Joseph Kabila ulifikia tamati Disemba 20 mwaka jana na ilipasa ufanyike uchaguzi baada ya kipindi hicho kumalizika. Hata hivyo Kamisheni ya Uchaguzi ya DRC ilitangaza kuwa, kutokana na sababu kadhaa zikiwemo za kiufundi na kutokuweko bajeti ya kuendeshea zoezi la uchaguzi huo, haingeweza kuitisha na kusimamia zoezi la uchaguzi huo mwaka jana. Kwa muktadha huo, Tume ya Uchaguzi ikaakhirisha uchaguzi huo pasina kutangaza tarehe mpya ya kufanyika kwake na kubainisha kwamba, serikali ya Rais Joseph Kabila itaendelea kuongoza hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.
Hatua hiyo ililipua ghadhabu za wapinzani na vyama vya siasa vya nchi hiyo. Wapinzani wanaamini kwamba, kutofanyika uchaguzi huo katika muda uliokuwa umepangwa hapo awali ni njama za kutaka kumbakisha madarakani Rais Kabila. Wapinzani hao wanasema kuwa, Rais Kabila kama walivyo Marais wengine wa bara la Afrika ana nia ya kubakia madarakani. Kwa msingi huo, kuakhirishwa uchaguzi kunampa fursa kiongozi huyo ya kujiandalia mazingira ya kisheria ya kubakia madarakani au hata kuandaa uchaguzi ambao utakuwa na maslahi kwake.
Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndio maana wapinzani waliandaa mikusanyiko ya kuonyesha malalamiko yao dhidi ya hatua ya kuakhirishwa uchaguzi. Mikusanyiko hiyo ilipelekea kuibuka makabiliano baina ya wapinzani na vikosi vya usalama. Katika hali ambayo tishio la kuibuka vita lilikuwa kubwa, kwa upatanishi wa kanisa katoliki kulianza mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kisiasa ili kuhitimisha mgogoro huo. Baada ya mazungumzo marefu hatimaye makubaliano hayo yalifikiwa. 
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ilikubaliwa kuwa, Rais Kabila mwaka huu aachie madaraka na kisha kuundwe serikali itakayojumuisha pia wapinzani na wakati huo huo kuanze mchakato wa kuandaa uchaguzi wa Rais ambao utafanyika mwaka ujao wa 2018. Licha ya kwamba, kupitia makubaliano hayo, kulikuwa na matumaini ya kufikia tamati mgogoro huo, lakini kutokana na kutoheshimu viongozi wa serikali ya Kinshasa baadhi ya vipengee vya hati ya makubaliano hayo, hivi sasa hatari ya ukosefu wa amani iliyotokana na mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa tishio zaidi. Hivi karibuni, Tume ya Uchaguzi ya DRC ilitangaza kuakhirishwa tena uchaguzi huo kutokana na machafuko yanayosababishwa na makundi ya wanamgambo. 
Filihali, viongozi mbalimbali wa Kiafrika na asasi za kimataifa wanataka kuheshimiwa makubaliano yaliyofikiwa na kuandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi katika nchi hiyo ili kuzuia kutokea vita vingine katika bara hilo.
Pamoja na hayo, kung'ang'ania madaraka na kutumia mbinu mbalimbali ili kuendelea kubakia uongozini umekuwa mtindo na mchezo unaofanywa na baadhi ya viongozi barani Afrika. Mfano wa hilo ni nchini Burundi, ambapo licha ya upinzani wote wa kieneo na kimataifa, Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo ameendelea kubakia madarakani. Katika baadhi ya nchi za Kiafrika, viongozi wengine hutumia mchezo wa kubadilisha Katiba na hivyo kujifungulia njia ya kuendelea kubakia madarakani. 
Umasikini wa utamaduni, uchu wa madaraka, kutofungamana na misingi ya demokrasia na uungaji mkono wa nyuma ya pazia wa baadhi ya madola ya Magharibi kwa ajili ya kuhakikisha vibaraka wao wanaendelea kubakia uongozini ili maslahi yao yadhaminiwe, ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma viongozi wa Kiafrika kufanya juhudi za kubakia madarakani kinyume kabisa na Katiba za nchi zao. Hii ni katika hali ambayo, kutokea mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni katika akthari ya nchi za bara la Afrika kutawafanya raia wa nchi nyingine waliochoka na madikteta watake kutekelezwa sheria.
Katika mazingira kama haya, inaonekana kuwa, hatua ya Rais Kabila katika mkondo wa makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa na kuandaliwa uwanja wa kutekelezwa kwake itaweza kuzuia kupanuka tena mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hivyo kutoruhusu kuwaka moto wa vita vingine katika eneo.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment