Writen by
sadataley
6:47 PM
-
0
Comments
Alikuwa "Kansela wa Muungano" na mwanasiasa aliyependwa Ulaya. Anasema Mhariri mkuu mstaafu wa DW, Alexander Kudascheff, katika maoni yake kuhusu kifo cha Helmut Kohl.
Helmut Kohl, alikuwa mwanasiasa mweledi. Anasema Mhariri Mkuu wa zamani wa DW Alexander Kudascheff, katika maoni yake ya kumuenzi kansela huyo wa zamani aliyehudumu kwa kipindi kirefu kabisa Ujerumani. Mohammed Dahman anakusomea maoni hayo.
Helmut Kohl alikuwa kansela kwa muungano wa Ujerumani na Ulaya. Alishika hatamu za uongozi kwa miaka 16 na kuwa mwenyekiti wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, kwa robo karne. Hilo pekee linadhihirisha shahiri uwezo, umahiri na ari ya madaraka, lakini vile vile pia inaonesha bahati kubwa ya kidemokrasia aliyokuwa nayo katika chaguzi. Alichaguliwa tena kushika wadhifa huo wa juu kabisa Ujerumani mara nne, jambo ambalo ni ufanisi mkubwa wa kusisimua katika ulingo wa siasa kwa vigezo vyote.
Katika jukumu lake lililoonekana kuwa la milele la mwenyekiti wa chama cha CDU, kiu chake cha maendeleo katika ngazi za uongozi na ukakamavu wake katika kukabiliana na upinzani ni mambo yaliyokumbukwa. Pamoja na hayo, mnamo 1989 alikabiliwa na changamoto na alikuwa akipigania kuulinda wadhifa wake wa uenyekiti wa chana cha CDU katika mkutano wa Bremen. Kuanguka kwa ukuta wa chuma, kusambaratika kwa muungano wa zamani wa Sovieti na kumalizika kwa vita baridi kulitokea wakati muafaka na Kohl alitumia fursa hiyo iliyojitokeza baada ya kuanguka kwa tawala za kidikteta za kikomunisti kwa maslahi yake mwenyewe na pia kwa masilahi ya Ujerumani.
Aliibadili historia na Helmut Kohl bila shaka yoyote alikuwa kansela wa muungano wa Ujerumani. Alipuuzilia mbali hofu, kusitasita na shaka shaka iliyokuwepo nyumbani Ujerumani na pia katika mataifa ya kigeni - na kuanzia Novemba 1989 kuendelea, Kohl alifanya kazi kwa bidii akielekeza nguvu kutaka kulifikia lengo hilo. Na ilipofika Oktoba 3, 1990, akafanikiwa kulitimiza lengo hilo. Alidhihirisha ujuzi na uwezo mkubwa kisiasa, na hata kihistoria, kwa wakati muafaka kabisa, wakati uliostahili. Na kwa baadhi, hilo lilimfanya kuwa Otto von Bismarck wa karne ya 20.
Lakini Kohl hakuwa tu Mjerumani mzalendo aliyekubali zawadi iliyotokana na mapinduzi ya kihistoria Ulaya Mashariki. Alikuwa pia raia halisi wa Ulaya. Kwa miaka 16 na katika mikutano kadha wa kadha ya kilele ya Ulaya, aliendelea kupigia debe na kuwatanabahisha watu na viongozi kuhusu mpango wa kuunda Umoja wa Ulaya.
Alikuwa pia muasisi mwenza wa sarafu ya pamoja ya euro, jambo ambalo ni la umuhimu mkubwa kwa haiba yake kama raia mzalendo. Alielewa kwamba sarafu ya pamoja ndiyo iliyokuwa njia pekee ya kukabiliana na changamoto zilizosababishwa na sarafu ya Ujerumani ya deutschmark iiyokuwa na nguvu na uwezekano wa upinzani nchini Ufaransa, Uingereza na nchi nyingine za Ulaya.
Helmut Kohl alikuwa mwanasiasa mweledi. Alikuwa mwanasiasa aliyependelea na kuunga mkono muungano wa Ujerumani na Umoja wa Ulaya uliotanuka. Alikuwa mtu shujaa, alifahamu kilichotakiwa kufanywa na kukifanya. Na hicho ndicho kilichompa heshima kubwa ya kimataifa na kumfanya kuwa kiongozi wa siasa wa haiba kubwa na aliyeheshimika sana, licha ya ukosoaji uliomkabili nchini Ujerumani.
DW Swahili
No comments
Post a Comment