Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, ametamka kuwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bado mgumu huku akitaja sababu mbili zitakazokwamisha taji hilo kutua Msimbazi.
Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon, mchezo uliopigwa wikiendi hi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba yenye pointi 62, inachuana vikali na mabingwa watetezi Yanga wenye 59 wakiwa wamebakisha michezo minne kabla ya mchezo wao wa jana, tofauti na wapinzani wao ambao wamebakiza miwili.
Omog alisema changamoto ya kwanza wanayokabiliana nayo ni kutoka kwa timu pinzani zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja ambazo zinapambana kubaki katika ligi kuu.
Omog alisema, timu hizo zinaonyesha upinzani mkubwa katika mechi ambazo wanaendelea kukutana nazo, hali inayompa hofu ya kutwaa taji hilo.
Aliongeza kuwa, kingine kinachompa hofu ya ubingwa ni presha ya wachezaji na viongozi kwenye timu ya kuwa na kiu ya ubingwa hali inayosababisha wawe wanaingia uwanjani na woga wa kupoteza mchezo na kusababisha wachezaji wake kucheza kwa kutojiamini.
"Kiukweli ni mapema sana kuzungumzia ubingwa wa ligi kuu kutokana na changamoto kadhaa tunazozipata ambazo huenda zitakwamisha ndoto zetu.
"Kama unavyojua zipo baadhi ya timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja zinazopambania kubaki katika ligi kuu ndiyo zinazotupa changamoto ya ubingwa.
"Kingine ni presha ya ubingwa iliyopo katika timu yetu ya Simba, inayowafanya wachezaji na viongozi kuingia uwanjani na hofu ya kupoteza mchezo,” alisema Omog aliyebakisha michezo miwili ya ligi dhidi ya Stand United na Mwadui FC.
No comments
Post a Comment