Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, May 13, 2017

Huu ndio Ukweli kuhusu ndege iliyovutwa kwa trekta

NI kioja. Tangu lini ndege ndogo inayoonekana kuwa ya kubeba abiria ikatembea kwenye barabara za magari mitaani kwa kukokotwa na trekta?

Hivyo ndivyo wananchi wengi wa maeneo ya Dodoma mjini, hasa kutoka Uwanja wa Ndege hadi Area C, ambako walikuwa wakijiuliza kutokana na kujiri kwa tukio hilo la aina yake.

Na ndivyo ilivyokuwa pia katika maeneo mengine nchini, hususan kwa wale waliobahatika kuiona picha iliyosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii juzi, ikionyesha ndege ndogo yenye mwonekano wa kuvutia pichani ikiburutwa na trekta barabarani.

Ni tukio lililotokea kutoka Airport kwenda Area D, kupitia barabara ya Maili Mbili, ambako ndege hiyo ilikuwa ikikatiza polepole kwa kukokotwa na trekta kiasi cha kuwashangaza mamia ya watu waliobahatika kushuhudia jambo hilo ‘live’.

Kwingineko nchini, uvumi mwingi ukasambaa, ukiwamo ule uliokanushwa na Jeshi la Polisi kwamba ndege hiyo ilikuwa ikikokotwa baada ya kuanguka.

Kutokana na yote hayo, ambayo mwishowe yaliibuwa mijadala ya aina yake kwenye mitandao ya kijamii, ndipo Nipashe ilipofuatilia kwa kina zaidi jana na kumpata mmiliki wake, ambaye alisema kuwa amefurahi kutimiza ndoto yake ya kuipata ndege hiyo ambayo haikuanguka, bali aliinunua kwa bei poa isiyotosha hata kununulia gari kama Toyota Noah.

Kwa sharti la kutotajwa jina lake wazi, akihofia baadhi ya ndugu zake kudhani kwamba sasa amekuwa bilionea mkubwa kiasi cha kununua ndege ilhali ukweli ni kwamba ameipata kwa bei ya chini, mmiliki wa ndege hiyo, ambaye pia anamiliki hoteli ya African Dreams iliyoko Area D, alisema aliipata ndege hiyo iliyokuwa ya Serikali (ikidaiwa kuwahi kuwa ya JWTZ) baada ya kuibuka kinara katika mnada wa wazi uliofanyika Julai, mwaka jana, na kuwashirikisha watu wengine kadhaa.

“Hii ndege niliinunua tangu mwezi wa saba (Julai), mwaka jana. Lakini tatizo lilikuwa ni je, tutaitoaje kama ilivyo kuifikisha hapa hotelini bila usumbufu kama vile wa kukata miti ovyo?” alisema mmiliki huyo alipohojiwa na Nipashe jana.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, pia aliithibitishia Nipashe jana kuwa taarifa nyingi zilizosambazwa mitandaoni hazikuwa za kweli, ikiwamo madai kuwa ni ndege iliyoanguka.

Bali, kilichotokea ni kwa mmiliki wa ndege hiyo chakavu kulazimika kuiondoa kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma ilikokuwa imeegeshwa kwa muda mrefu na kuipeleka kwenye hoteli yake ikiwa kama ilivyo – jambo lililozingatia taratibu zote za kisheria ikiwamo masuala ya usalama barabarani.

“Kuna taarifa zinasema kuwa imeanguka si kweli. Hii ndege ni chakavu na ilishauzwa kwa mtu binafsi ambaye ni mmiliki wa hoteli ya Africa Dreams… sasa alikuwa akiivuta kwa trekta kuiondoa kwenye uwanja wa ndege na kuipeleka kwenye eneo lake la hoteli,” alisema Kamanda Mambosasa.

MMILIKI AFUNGUKA ZAIDI
Akielezea zaidi, mmiliki wa ndege hiyo alisema licha ya kushinda katika mnada wa mauzo ya ndege hiyo tangu Julai na kukwama kuiondoa kwa kutojua aisafirishe vipi bila kuathiri pia mwonekano wake, juzi alilazimika kutumia trekta kutimiza ndoto ya kuifkisha hotelini kwake, baada ya kuamriwa kuitoa kwenye eneo ilikokuwa ili kupisha ukarabati mkubwa wa uwanja huo.

“Awali nilitaka kuibeba kwa lori. Lakini lengo langu si kuiharibu hata kidogo. Nataka ifike kama ilivyo, hivyo nilishindwa kuitoa. Njia pekee ambayo ilionekana inawezekana ni hii ya kukokota taratibu kwa trekta,” alisema.

Alisema vibali vya kuihamisha kwa kuipitisha kwenye barabara ya magari alivipata kwa mamlaka zote husika zikiwamo Manispaa ya Dodoma, Wakala wa Barabara (Tanroads), uongozi wa Uwanja wa Ndege, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Alisema lengo la kununua ndege hiyo ni kuongeza wigo wa biashara yake ya hoteli kwa kuifanya kama sehemu ya kivutio ambayo watu wataitumia kupigia picha mbalimbali za matukio kama ya sherehe za kuzaliwa, kipaimara, harusi na wanafunzi kupata fursa ya kujifunza pindi wakihitaji kufanya hivyo.

“Hapa hotelini nina eneo kubwa ambalo nitaiweka hii ndege na kuitengenezea mandhari kama ya ‘Airport’ (uwanja wa ndege) na itakuwa kama sehemu ya makumbusho ambako watu mbalimbali, wakiwamo watoto, watapata fursa ya kupigia picha kwa kulipia,” alisema na kuongeza:

“Ndani mle hamna viti (hivi sasa). Nitaanza kwa kuviweka, nitafunga kiyoyozi, nitatengeneza ndani ili iwe kama na kimgahawa au kioski kwa ajili ya vinywaji. Nitaiboresha zaidi ili itumike kupigia picha za harusi, birthday na kujifunzia pia.”

Akizungumzia chanzo cha ujio wa wazo lake hilo kibiashara, mmiliki huyo alisema ni kupingana kwake na wazo walilokuwa nalo washindani wake kwenye mnada wa mauzo ya ndege hiyo, ambao karibuni wote walipania kuibomoa ili wanufaike nayo kwa matumizi mengine kama chuma chakavu. Yeye akafikiria vinginevyo, akiamini kwamba ndege hiyo inaweza kumnufaisha zaidi kwa kuifanya sehemu ya kivutio hotelini kwake.

“Ndiyo maana hata kuitoa pale imekuwa ngumu ni kwa sababu nataka ifike hotelini kama ilivyo. Unajua hii ni rahisi mtu kuja hapa kuona na kujifunza. Wengine hawajawahi kuisogelea hata ndege… lakini hapa wataifikia, kupiga picha, wataingia ndani na kujifunza (zaidi) pia,” alisema.

Alisema changamoto mojawapo kwake ni hisia za baadhi ya watu wake wa karibu wanaoweza kudhani kuwa sasa ni tajiri sana kiasi cha kumiliki ndege, jambo ambalo si la kweli kwa sababu hiyo siyo mpya bali ni chakavu.

Aidha, alisema kumekuwapo pia na woga wa baadhi ya watu kuwa ndege inaweza kumilikiwa na taasisi za serikali au wazungu tu, jambo ambalo pia si sahihi kwa sababu kuna uwezekano wa Watanzania kumiliki ndege pia, kama yeye ambaye sasa anayo hiyo hata kama hairuki, lakini itamfaa kwa matumizi mengine ya kibiashara.

YAFIKIA AREA C
Hadi kufikia jana, ndege hiyo ilikuwa katika eneo maarufu la Wajenzi lililoko Area C, ikibaki hapo barabarani kwa muda wakati mchakato wa kuisafirisha hadi kwenye makazi ya kudumu hotelini, African Dreams ukiendelea.

Akizungumzia mahali ilipoweka kituo kwa muda sasa, mmiliki huyo alisema anashirikiana na wataalamu kuona namna ya kuipitisha salama bila kuharibu miti iliyoko pembezoni mwa eneo itakapopita hadi kufika hotelini na njia mojawapo ni kuifungua mabawa yake na kuyarudishia pindi safari yake hiyo itakapokamilika.

Alisema sababu nyingine ya kuiacha kwa muda eneo hilo hadi kufikia jana jioni ni kutoa fursa kwa wananchi kuiona ili wapunguze kiu, hivyo kupunguza idadi ya wale wanaoifuata kwa karibu kuishangaa safari ya kuipeleka hotelini itakapoanza tena.

“Kuna mtaalamu jioni ya leo (jana) tutakutana naye aangalie namna tutakavyoipitisha bila kusababisha uharibifu katika barabara ya Wajenzi hadi Area D. Kama ataona upana unaweza kuharibu miti, tutafungua mabawa yake halafu ikishaingia hotelini tutayafunga kama yalivyokuwa awali,” alisema mmiliki huyo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment