MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amepiga marufuku tabia ya wakulima mkoani humo kuuza mahindi mabichi yakiwa shambani kwa bei ya kutupa huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunawadidimiza kiuchumi na kuendelea kuwa maskini.
Alipiga marufuku uuzaji huo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kubaini kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara wanakwenda vijijini na kuwashawishi wakulima wawauzie mazao hususan mahindi yakiwa hayajakomaa shambani.
Zelothe alisema mtindo huo maarufu kwa jina la ‘tuchomane’ umekuwa ikiwaumiza kiuchumi wakulima, hali ambayo imewafanya wengi wao kuona kilimo hakiwanufaishi.
“Haka kamtindo kanakoitwa tuchomane sikubaliani nako hata kidogo na ninapiga marufuku uuzaji mazao shambani kwani wakulima hawawezi kujua ni kiasi gani cha mazao wameuza hivyo kujikuta wakikandamizwa sana. Uuzaji huo unawafanya wengi waendelee kuwa masikini wa kutupwa,” alisema.
Alisema akimbaini mfanyabiashara yeyote anawafuata wakulima na kuwashawishi wamuuzie mazao yakiwa bado mabichi mashambani atahakikisha anamchukulia hatua za kisheria.
Hatua hiyo ya Zelothe imekuja siku kadhaa baada ya Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha kuwatahadharisha wakulima wa jimbo hilo kuacha kuuza mazao yakiwa shambani kwani kufanya hivyo kunasababisha baadhi yao kukumbwa na upungufu wa chakula.
Malocha alisema hayo katika kata za Nankanga na Ilemba kwa nyakati tofauti wakati wa ziara kukagua shughuli za maendeleo kwenye jimbo hilo.
Alisema baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kuuza mazao yao yote yakiwa shambani, hali ambayo imekuwa ikisababisha kaya zao kukumbwa na upungufu wa chakula hivyo kusababisha baadhi yao kutokuwa na uhakika wa kula milo mitatu kwa siku.
“Acheni kuuza mazao hasa mahindi mabichi yakiwa shambani kwani kufanya hivyo mnawanufaisha wanunuzi wanaowalipa fedha kidogo. Subirini mavuno ili mpange bei zinazostahili,” Malocha alisema.
No comments
Post a Comment