Writen by
sadataley
10:09 AM
-
0
Comments
Marekani imelaani kukamatwa na kuzuiwa kwa muda kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, anayetumai kuifikisha kikomo miaka 30 ya utawala wa rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni.
Huku kura zikiendelea kuhesabiwa nchini Uganda kufuatia uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika hapo jana, Marekani imeilaani vikali serikali ya Uganda baada ya maafisa wa usalama kumkamata kwa muda mfupi mgombea urais wa upinzani Kizza Besigye. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani John Kirby alisema kitendo hicho kinatilia shaka uwajibikaji wa Uganda kufanya uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi.
Besigye ambaye ni mgombea wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wagombea saba wanaoshindana na Rais Museveni, alitiwa mbaroni wakati alipokuwa akichunguza madai ya wizi wa kura uliofanywa na chama tawala cha National Resistance Movement, NRM.
Msemaji wa chama cha Besigye, Forum for Democratic Change, FDC, Semuju Nganda, alisema kiongozi huyo alikamatwa wakati alipokuwa akifanya uchuguzi katika kituo kisicho halali kilichokuwa kikisimamiwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu, Kampala.
Msemaji wa polisi Fred Enaga alithibitisha baadaye kwamba Besigye aliachiliwa na kupelekwa nyumbani kwake, akisema walimzuia kiongozi huyo wa upinzani kuingia eneo la usalama ambalo raia hawakuruhusiwa.
Ingawa Besigye aliachiwa huru, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kirby alisema kuachiwa kwake hakufuti ukweli kwamba alikatwa.
Kirby aliongeza kusema kwamba Marekani pia ina wasiwasi kuhusu kufunguliwa kuchelewa vituo vingi vya kupigia kura, pamoja na hatua ya serikali ya Uganda kuifungia mitandao kadhaa mashuhuri ya kijamii na mitandao ya kutuma fedha kupitia simu za mkononi siku ya uchaguzi hapo jana. "Tunaendelea kuihimiza serikali ya Uganda pamoja na vyama vyote vya siasa na wafuasi wao kujiepusha na vitendo zaidi au kauli zinazoweza kusababisha machafuko zaidi au watu kufa."
Wakati haya yakiarifiwa, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binaadamu nchini Uganda, Uchenna Emelonye, alisema kufungiwa mitandao ya kijamii wakati wa upigaji kura kuna athari zake katika haki za binaadamu.
"Bila shaka suala la kutia wasiwasi katika ofisi yetu ni ukweli kwamba serikali ya Uganda imeifungia mitandao ya kijamii, ukiwemo mtandao wa WhatsApp. Hii ina athari katika haki za binaadamu na tumelijadili suala hili na maafisa wanaohusika."
Akitoa sababu za kiusalama, Godfrey Mutabazi, Mkuu wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda, alisema walizifunga huduma za mitandao ya Twitter, Facebook na WhatsApp. Shirika la kutetea waandishi wa habari, CPJ, lilisema hatua hiyo inavuruga mchakato wa kidemokrasia.
Fujo za hapa na pale
Raia wa Uganda walisimama katika foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura, huku upigaji kura ukianza kuchelewa kwa sababu vifaa vya kupigia kura vilichelewa kufikishwa vituoni.
"Wengi wetu tumejitokeza kupigia kura mageuzi, lakini serikali hii ina mipango ya kubakia madarakani," alisema Robert Ssebaggala, mpigaji kura wa mjini Kampala. "Lakini sharti nipige kura kupigania haki zangu, Museveni lazima aondoke madarakani," akaongeza kusema mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 53.
Muda wa kupiga kura uliongezwa katika wilaya mbili baada ya vituo kufungwa. Amama Mbabazi, ambaye pia anawania urais, alisema kucheleweshwa kwa upigaji kura huenda ni njama ya makusudi kwa kuwa hakuna sababu za msingi kufanya hivyo.
Matukio ya machafuko ya hapa na pale yameripotiwa. Msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema polisi walitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya wapigaji kura kadhaa katika kitongoji kimoja cha mjini Kampala, na kuwakamata wawili kwa sababu walijaribu kuwazuia wengine kupiga kura na kuzua vurugu.
Chanzo:DW SWAHILI
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments
Post a Comment