Writen by
sadataley
10:55 AM
-
0
Comments
Na Neville Meena, MwananchiDodoma. Kamati za Bunge Maalumu, zimekamilisha kazi ya kujadili na kuchambua Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku ikiwa imefanyiwa mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Wajumbe wanatarajiwa kuanza kukutana kama Bunge
zima kuanzia Jumanne ijayo, Septemba 2, 2014 wakati kamati zitakaposoma
taarifa zake baada ya kufanya uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba
kwa zaidi ya wiki tatu, huku yakitarajiwa mabadiliko makubwa.
Mabadiliko yaliyofanywa yameondoa mambo makubwa
yaliyokuwa yakiifanya rasimu hiyo kuonekana mpya, hivyo sasa baadhi ya
wachambuzi wa mambo wanaiona rasimu kama ‘Katiba ya 1977 iliyofanyiwa
marekebisho.’
Mwelekeo wa kubadili karibu misingi yote muhimu
iliyojengwa na tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba akiwa
mwenyekiti, ilianza baada ya kuwekwa kando kwa mfumo wa muungano wa
Serikali tatu uliopendekezwa na badala yake kurejea katika muundo wa
sasa wa serikali mbili.
Uamuzi huo uliathiri mtiririko na muundo mzima wa
sura na ibara za rasimu hiyo, kwani sasa wajumbe wa Bunge Maalumu
walilazimika kutengeneza Katiba yenye mwelekeo wa serikali mbili na siyo
tatu tena zilizokuwa zimependekezwa na tume.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad
aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba mwelekeo wa uchambuzi wa rasimu kwa
sura hizo 15, lazima ufuate kile ambacho kamati zilikiamua katika
uchambuzi wa awali wa sura ya kwanza na ya sita.
Miongoni mwa mambo ambayo yameachwa baada ya
kurejesha mfumo wa serikali mbili ni muundo wa uongozi wa juu wa nchi
hususan nafasi ya Makamu wa Rais, muundo wa Bunge la Jamhuri, kupunguzwa
mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wa
ubunge.
Kadhalika, habari kutoka ndani ya kamati zilisema
suala la kuwekwa kwa maadili ya uongozi kwenye Katiba nalo lilizua
mjadala mkali kutokana na baadhi ya wajumbe kutaka liondolewe kwa
maelezo kwamba linapaswa litajwe kwenye sheria na siyo Katiba.
Mambo ya muungano
Miongoni mwa mambo ambayo kuna kila dalili kwamba
yatabadilika ni Bunge Maalumu kuongeza mambo ya muungano kutoka saba
yaliyopendekezwa na tume na huenda idadi yake ikazidi 22 yaliyomo kwenye
Katiba ya sasa.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika baadhi
ya kamati za Bunge hilo na kuthibitishwa na baadhi ya wenyeviti wake,
umebaini kuwa yapo mapendekezo ya mambo ya muungano kuongezwa, tofauti
na mtazamo wa awali kwamba yangepungua kama moja ya njia za kuondoa kero
za muungano.
Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza mambo saba tu
kwenye orodha ya muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu, mfumo ambao
hata hivyo ni dhahiri umeshawekwa kando na Bunge Maalumu na kurejesha
muundo wa serikali mbili.
Mambo yaliyopendekezwa na tume hiyo ambayo yapo kwenye sura ya
17 ya Rasimu ya Katiba inayohusu masharti ya mpito ni pamoja na Mamlaka
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Uraia na Uhamiaji.
Mengine ni Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje,
Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa Bidhaa na mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Mapendekezo hayo yaliyaacha nje mambo mengine 15
yaliyopo kwenye Katiba ya sasa ambayo ni polisi, mamlaka juu ya mambo
yanayohusika na hali ya hatari, mikopo na biashara ya nchi za nje,
utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, bandari, mambo
yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu na leseni ya viwanda na
takwimu.
Pia yamo elimu ya juu, maliasili ya mafuta, pamoja
na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina
nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia, Baraza la Taifa la
Mitihani la Tanzania, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utafiti
wa hali ya hewa na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano.
Baadhi ya wenyeviti wa kamati za Bunge Maalumu
wamesema kuna kila dalili kwamba baadhi ya mambo yaliyoachwa
yatarejeshwa huku kukiwa na mtazamo kwamba mengine yanaweza kuongezwa
kutoka nje ya orodha ya sasa.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid
Mohamed alisema orodha iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba ina upungufu
mkubwa kwani imeacha mambo mengi ya msingi yenye sura ya muungano.
“Mathalani huwezi kuzungumzia kwamba usalama ni
suala la muungano halafu ukaacha mambo ya anga, au ukaacha suala la
mitihani, yaani Baraza la Mitihani limeachwa pia suala la utafiti nalo
huwezi kuliacha, kwa hiyo orodha itaongezeka,” alisema Mohamed.
Mwingine ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita,
Stephen Wassira alisema kuna mambo mengi ya muungano yaliyotajwa kwenye
Rasimu ya Katiba lakini hayako katika orodha iliyowekwa kama moja ya
nyongeza kwenye rasimu hiyo.
“Ngoja nikwambie kwamba mambo hayo yataongezeka,
hilo halina ubishi na kamati yangu tulijadili kidogo na kesho (leo)
tutakutana kumalizia. Ukisoma vizuri ibara kwa ibara, utagundua kuwa
kuna mambo mengi kama vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo ni chombo
cha muungano hata ukiangalia muundo wake,” alisema Wassira.
Alitaja mambo mengine kuwa mahakama ya juu
inayopendekezwa kuanzishwa lakini haimo kwenye orodha pamoja na masuala
ya elimu ya juu na utafiti.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kamati Namba nne,
Christopher Ole Sendeka alisema kuna kazi kubwa ya kutazama upya orodha
ya mambo ya muungano na kwamba suala la usalama wa anga ni moja ya mambo
hayo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu
alisema, licha ya kwamba kamati yake haikujadili suala hilo lakini
orodha hiyo inaweza kuongezeka kwani kuna mambo mengi yameachwa.
“Leo tulikuwa tunaangalia suala la fedha na kuna mambo
ukichuguza humo yanagusa sehemu zote mbili, sisi hatukujadili sehemu
hiyo kutokana na kwamba haikuwa kwenye orodha ya kazi tulizopewa ila
nadhani tukipata fursa bungeni lazina mambo hayo yaangaliwe,” alisema
Mwalimu.
Kamati nyingine ambayo haikujadili suala hilo ni
namba tatu ambayo mwenyekiti wake, Dk Francis Michael alisema orodha ya
mambo ya muungano iko kwenye sura ya 17 ambayo haikuwa sehemu ya kazi za
kamati.
No comments
Post a Comment