Writen by
sadataley
11:05 AM
-
0
Comments
Kwamba Rais Jakaya Kikwete muda wowote kuanzia sasa atafanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge, wakiwamo viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hakika ni habari njema ambazo zimewapa wananchi matumaini makubwa.
Hivi sasa habari hiyo ndiyo gumzo kuu katika kila
kona ya nchi yetu na vyombo vya habari, ikiwamo mitandao ya kijamii
ambayo imesheheni maoni ya wananchi wanaounga mkono uamuzi huo wa Rais.
Sisi wa Mwananchi tunaungana na wananchi hao
kumpongeza Rais kwa uamuzi huo wa busara wenye lengo la kuwaunganisha
wananchi waliogawanyika vipandevipande baada ya mchakato wa kupata
Katiba mpya kuvurugwa na wanasiasa.
Bila shaka Rais atakuwa ameona mbali na kutambua
madhara yanayoweza kusababishwa na kitendo cha Bunge la Katiba kuendelea
na mchakato wa Katiba bila kuwapo mwafaka wa kitaifa, kwa maana ya
kutokuwapo uwakilishi mpana katika kujadili na kuboresha Rasimu
iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Hakuna asiyejua kwamba mwelekeo hasi wa mijadala
katika Bunge hilo linaloandika Katiba mpya ndiyo hasa uliowasukuma
wajumbe wake kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kususia vikao
na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Moja ya sababu za kufanya hivyo ni vitendo vya
kibaguzi, kejeli, matusi ya nguoni na vitisho kutoka kwa wajumbe wa
chama tawala, CCM, ambacho Ukawa wanasema kiliteka mjadala na mchakato
mzima kwa kuweka kando Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
kupenyeza yao iliyotayarishwa na chama hicho. Kwa mtazamo wa Ukawa,
katiba ambayo itatokana na mazingira hayo haitakuwa ya wananchi, bali
itakuwa ya CCM.
Ni jambo la kusikitisha kwamba tangu wajumbe wa
Ukawa wasusie Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu hawajawahi kusikilizwa na
chombo chenye mamlaka ya juu au chombo ambacho hakina masilahi ya moja
kwa moja na mgogoro huo.
Wito wao wa mara kwa mara wa kukutana na Rais
Kikwete ulibezwa na kupuuzwa na makada wa chama chake ambao walipaswa
kumshauri akutane nao ili kupata maridhiano na mwafaka wa kitaifa.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna mahali
popote duniani ambako katiba ya wananchi iliyo nzuri na endelevu
ilitokana na mazingira ya ghiliba, hadaa na shari kama ambayo
tumeyashuhudia katika Bunge hili.
Katiba yoyote nzuri huhitaji mazingira yenye masikilizano, maelewano na kustahiana.
Mazingira ya matusi ya nguoni, uadui, kebehi,
dharau, vitisho na hadaa kama ilivyotokea katika Bunge letu la Katiba
huzaa chuki, hivyo katiba inayotokana na mazingira kama hayo kamwe
haiwezi kukubalika kwa wananchi kwa sababu hupandikiza chuki na hatimaye
kusababisha vurugu.
Ndiyo maana tunampongeza Rais Kikwete kwa kuona
hilo na kuridhia kukutana na viongozi wa vyama vyenye wabunge
kuzungumzia kadhia hiyo.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliandaa Rasimu ya Katiba kwa
kuzingatia maoni ya wananchi. Bahati mbaya Bunge la Katiba limetekwa na
wanasiasa wanaopigania masilahi binafsi.
Ndiyo maana, pamoja na mambo mengine wamekataa
uwepo ukomo wa vipindi vyao vya ubunge, wamekataa wapigakura
kuwawajibisha wabunge wao na pia wamekataa pendekezo la mawaziri
kutokuwa wabunge.
Katika hali kama hiyo, Rais atafanya vyema iwapo atasitisha Bunge hilo hadi mwafaka wa kitaifa utakapopatikana.
No comments
Post a Comment