Writen by
sadataley
11:09 AM
-
0
Comments
Na Vicky Kimaro, MwananchiDar es Salaam. Uongozi wa Simba umemrudisha kundini mshambuliaji wake wa zamani, Emmanuel Okwi ukisema umechukua hatua hiyo: “Kumsitiri ili asipoteze kipaji chake” baada ya watani wake wa jadi Yanga, kumshtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya Simba, Zakaria Hans Pope alisema mbinu ambazo Yanga ilitumia Yanga
kumsajili Okwi wakati alipokuwa na mgogoro na klabu ya Etoile du Sahel
ya Tunisia ndiyo hiyohiyo kamati yake iliyoitumia kumrejesha Simba.
“Yanga walivyowafanyia Watunisia wakati wana
mgogoro na Okwi walijiona washindi, sasa na sisi kwa mantiki hiyohiyo
tumeamua kumrudisha kundini, “alisema Hans Pope.
Alisema Simba haina mkataba wowote na Okwi na
kwamba anaruhusiwa kuondoka muda wowote atakapoamua huku akisema timu
hiyo inasubiri uamuzi wa kesi ya mchezaji huyo na Yanga imalizike
kukamilisha mchakato.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa baadhi ya
viongozi wa Simba zinasema Okwi amemwaga wino wa kuichezea Simba kwa
miaka miwili na kwamba malipo ya awali ya mkataba huo ya Dola za
Marekani 10,000 alichukua mwaka jana.
Kauli ya Okwi
Akizungumzia madai yake na Yanga, Okwi alisema juzi alipewa barua na TFF ya kushtakiwa na Yanga.
Alisema katika madai, alisema Yanga inamtuhumu
kuchukua fedha za usajili na kushindwa kuitumikia huku akishindwa kuipa
ubingwa baada ya kufungiwa michezo minne.
“Mimi naishangaa Yanga, eti inadai fedha za
usajili, usajili maana yake nisaini wa wanipe fedha, sasa hizo fedha
wanazodai ni zipi? Mbona hawazungumzii mshahara wangu ambao nilikuwa
nalipwa kwa kutumia nguvu, nipo tayari kukaa meza moja na Yanga katika
kesi wala siogopi chochote na pale naamini kila mmoja atapata haki yake.
“Nawaomba wana Simba wanipokee mimi ni kijana wao,
nitaitumikia Simba kwa moyo wangu wote, mimi ni mpya nawaahidi sitakuwa
tena msumbufu,” alisema Okwi.
Wakati huo huo, baadhi ya klabu za Ligi Kuu
zimelipinga Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kusogeza usajili mbele
mpaka leo saa 6 usiku kwa kigezo kuwa ni timu moja tu ndio iliyokuwa
imekamilisha usajili wake hadi juzi saa sita usiku.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa
soka waliitaka TFF kuacha kudanganya umma wa Watanzania na badala yake
iseme ukweli kilichofanya wakasogeza mbele usajili.
No comments
Post a Comment