Writen by
sadataley
5:01 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu/AFPRio de Janeiro, Brazil. Goli la Mario Goetze katika dakika ya 113 jana limeiwezesha Ujerumani kuchukua ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya nne katika uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro.
Goli hilo pekee la mechi pia limeiwezesha
Ujerumani kuandika historia kwa kuwa timu pekee toka Ulaya iliyoweza
kutwaa Kombe la Dunia katika kipute kilichopigwa Amerika Kusini.
Goetze, ambaye ni straika wa Bayern Munich,
alizamisha ndoto za Muargentina Lionel Messi za kuakisi mafanikio ya
mkongwe mwingine wa Argentina, Diego Maradona, aliyeiwezesha timu hiyo
kutwaa ubingwa wa Dunia mwaka 1986.
Dakika muhimu ya mchuano huo Jumapili ilidhihirika
mbele ya mashabiki karibu 75,000 katika uwanja maarufu wa Maracana,
pale Andre Schuerrle alipochomoka toka kushoto, akimpigia pande Goetze.
Mwana-Bayern huyo mwenye umri wa miaka 22
alituliza mpira kifuani kwa kujiamini, huku akijipinda na kufyatua
kigongo kikali kilichomwacha kipa wa Argentina, Sergio Romero, akitoa
macho.
Uwanja mzima uliokuwa umejaa mashabiki wa Ujerumani ulilipuka kwa shangwe wakati nyavu za Argentina zikitikisika.
Messi na vijana wake walibanwa mbavu, wakipoteza
nafasi chache za kufunga walizoambulia katika mchuano huo wa miamba
waloonekana kuwa nguvu sawa.
Fowadi huyo anayeichezea Barcelona atakumbukwa kwa
kushidwa kutumia ‘mchongo’ alotengenezewa katika kipindi cha pili, huku
akipiga nje ‘free kick’ walopata Argentina dakika za mwisho mwisho.
Ushindi wa Ujerumani jana ulishangiliwa vilivyo na
mashabiki wa Brazili, ambao hawakufurahishwa na uwezekano wa mahasimu
wao, Argentina, kuchukua Kombe hilo la Dunia huku Selecao wakiwa
wameshindwa hata kuambulia nafasi ya tatu.
No comments
Post a Comment