Writen by
sadataley
5:03 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu/AFPRio de Janeiro, Brazil. Ujerumani ndiyo mabingwa wapya wa dunia baada ya kuichapa 1-0 Argentina katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2014, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro, Brazil.
Shujaa wa Ujerumani katika mechi hiyo alikuwa ni
kinda Mario Gotze, aliyefunga bao la ushindi dakika ya 113, akiunganisha
vizuri krosi ya Andre Schurrle.
Hili ni taji la nne la ubingwa wa dunia kwa
Ujerumani huku ikiwa imecheza mechi nane za fainali ya Kombe la Dunia.
Kwa ushindi huo Ujerumani imekuwa timu ya kwanza ya Ulaya kutwaa ubingwa
katika ardhi ya Amerika Kusini, huku Argentina ikishindwa kumaliza
ukame wa miaka 28 wa kutwaa ubingwa wa dunia tangu ilipotwaa taji hilo
1986 ikiifunga Ujerumani ya Magharibi.
Mechi hii ya fainali ilikuwa kama marudio ya fainali za 1986 na 1990, ambazo zilizikutanisha Ujerumani na Argentina.
Katika mechi ya jana, Ujerumani waliianza kwa kasi
na kupeleka mashambulizi katika lango la Argentina, lakini Argentina
walikuwa mahiri kupeleka mashambulizi ya kushitukiza katika lango la
Ujerumani.
Dakika ya 21, Gonzalo Higuain alikosa bao akiwa na
kipa Manuer Neuer wa Ujerumani baada ya kupiga shuti kali ambalo
lilitoka pembeni ya lango.
Krosi ya Ezequiel Lavezzi ilimkuta Higuian katika
eneo la hatari dakika ya 30, ambaye aliuweka mpira nyavuni, lakini
mwamuzi alikataa bao hilo kwani Higuian alikuwa ameotea.
Ujerumani walilazimika kufanya mabadiliko katika
dakika ya 30, baada ya kuumia Kramer, na nafasi yake kuchukuliwa na
Andre Schurrle, mabadiliko ambayo yalileta uhai kwa Ujerumani kwani
dakika ya 45 Benedict Howedes alipiga kichwa mpira wa kona ambao
uligonga mwamba wa goli.
Kipindi cha pili Argentina ilimtoa Lavezzi na
nafasi yake kuchukuliwa na Sergio Aguero, hivyo kuanza kwa kasi na
katika dakika ya 47 Lionel Messi alipata nafasi nzuri, lakini alipiga
nje mpira akiwa amebaki na kipa Neuer.
Hata hivyo, katika kipindi hiki cha pili Ujerumani
walionekana bora zaidi katika kuanzisha mashambulizi ya kushitukiza,
lakini walishindwa kuipenya ngome imara ya Argentina.
Hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyopata
bao, hivyo mwamuzi kuongeza dakika 30. Beki wa kati wa Ujerumani, Jerome
Boateng pamoja na mabeki wa Argentina, Ezequeil Garay na Martin
Demichelis walifanya kazi kubwa katika safu za ulinzi za timu zao.
Mwanzoni mwa dakika hizo 30 za nyongeza, Ujerumani
ilipata nafasi nzuri, lakini shuti kali la Schurrle lilipanguliwa na
kipa wa Argentina, Sergio Romero, na Argentina walipata nafasi dakika ya
96, lakini Rodrigo Palacio alishindwa kuitumia.
No comments
Post a Comment