Writen by
sadataley
6:05 PM
-
0
Comments
Waziri wa Fedha,Saada Mkuya.PICHA|MAKTABA
Na MwananchiTunalazimika leo kuihadharisha Serikali kuhusu madhara
yatakayotokea kwa nchi yetu kutokana na kutolipa madeni, iwe ya nchini
mwetu au ya nje. Dunia sasa inajua kwamba Serikali yetu imelimbikiza
madeni na kujikuta ikidaiwa kila kona, huku watendaji wake wengi
wakiishi kwa matanuzi na kufuja fedha mithili ya mabaharia walevi.
Wakati huohuo, kasi ya kukopa inazidi kuongezeka na kutishia mustakabali
wa nchi yetu kutokana na Deni la Taifa ambalo wataalamu wa masuala ya
uchumi wanasema haliwezi kulipika iwapo Serikali haitaelekeza mapato
yake kwenye miradi ya kukuza uchumi badala ya anasa na matumizi yasiyo
na maana.
Wananchi wasiwe na matumaini yoyote kwamba huko
tuendako Serikali huenda ikaacha utamaduni wake wa kufanya matanuzi kuwa
kipaumbele chake. Hebu angalia mlolongo wa bajeti zake za kila mwaka.
Matumizi yake ya kawaida yanapewa zaidi ya asilimia 60, huku miradi na
shughuli za maendeleo zikipewa chini ya asilimia 40. Bajeti ya mwaka wa
fedha ujao, kwa mfano inaonyesha kwamba fedha za miradi na shughuli za
maendeleo ni Sh6,445 trilioni sawa na asilimia 32.4 ya bajeti nzima ya
Sh19.9 trilioni, huku matumizi ya kawaida yakitengewa Sh13.408 trilioni
sawa na asilimia 67.4 ya bajeti hiyo.
Bajeti hiyo kwa kiasi kikubwa inategemea mikopo na
fedha za wafadhili ambazo siyo tegemeo la uhakika kwa sababu
hazipatikani kwa wakati au kinapatikana kiasi kidogo tu cha fedha hizo.
Hivyo bajeti nzima inakuwa haitekelezeki, kwani inatayarishwa kwa
kutumia vigezo vya kutunga na kufikirika pasipo kuangalia vyanzo vya
uhakika vya mapato. Matokeo yake ni kushindwa kulipa madeni na
kulisababishia Taifa hasara kubwa kutokana na riba itokanayo na
ulimbikizaji wa madeni kwa muda mrefu.
Ipo mifano mingi ya hali hiyo. Kwa mfano, hebu
tuangalie hasara itakayosababishwa na Serikali itakapolazimika kulipa
riba ya Sh5 bilioni kutokana na malimbikizo ya miezi sita kwa kampuni ya
Jacobsen Elekron AS inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa
Kinyerezi, jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo ya Norway inaidai Serikali
Sh80.52 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya malipo kuanzia Novemba mwaka
jana na Mei mwaka huu.
Hivyo, inailalamikia Serikali kwa kuchelewesha
malipo yake mara kwa mara kinyume cha mkataba na imetishia kusitisha
kazi ya kutekeleza mradi huo muhimu utakaozalisha megawati 150 za umeme
baada ya kukamilika.
Upo ushahidi kwamba kampuni nyingi za kigeni
zimeamua kuweka vipengele vya ulipaji wa riba katika mikataba yake na
Serikali, baada ya kugundua kwamba Serikali ya Tanzania hailipi madeni
yake na kwa wakati. Madeni ya wazawa kama watumishi wa Serikali,
makandarasi, wazabuni na wakulima waliokopwa mazao yao au waliochukuliwa
ardhi yao pasipo fidia yanabaki pasipo kulipwa kwa miaka mingi, kwani
Serikali inajua kwamba hawana uwezo wa kuipeleka mahakamani. Hadhari
yetu kwa Serikali ni kwamba inaipeleka nchi yetu kubaya kwa kulimbikiza
madeni, huku ikiendeleza kasi ya kukopa. Ni makosa makubwa kutumia ubabe
kuchukua ardhi ya wananchi pasipo fidia au kukopa mazao yao bila
kulipa. Kwa utamaduni huu wa Serikali kuendekeza madeni na mikopo, nchi
yetu huko tuendako haiwezi kuepuka janga la kufilisiwa na hatimaye
kuuzwa.
No comments
Post a Comment