Writen by
sadataley
2:17 PM
-
0
Comments
Lilongwe. Malawi. Mgombea urais wa Chama cha Democratic Progressive Party (DPP) nchini Malawi, Profesa Peter Mutharika, ametangazwa kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kuwashinda wagombea wengine.
Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Mei 20 mwaka huu, uligubikwa na vituko, huku rais
aliyeshindwa Joyce Banda akitangaza kufuta uchaguzi huo kwa madai kuwa
uligubikwa na vitendo vya wizi wa kura.
Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), ilimtangaza
Profesa Mutharika kuwa rais baada ya kuwashinda wagombea wengine 12. MEC
ilitangaza matokeo hayo Ijumaa usiku baada ya kutokea mvutano mkali
kati ya Tume hiyo na Banda.
Profesa Mutharika ameshinda kwa asilimia 36.4,
akifuatiwa na mgombea urais wa Malawi Congress Party (MCP), Lazarous
Chakwera aliyepata asilimia 27.8, Banda asilimia 20.2 na mgombea wa UDF,
Atupele Muluzi alishika nafasi ya nne kwa kupata asilimia 13.7.
Mwenyekiti wa MEC, Jaji Maxon Mbendera baada
kumtangaza Profesa Mutharika kuwa rais, alimtaka kufanya kazi kwa
uaminifu na bila upendeleo.
“Wamalawi wanaamini unaweza kufanya mabadiliko, tafadhali usiwaangushe kwa sababu wamekuamini,” alisema Jaji Mbendera.
Katika hatua nyingine, Jaji Mbendera alisema
matokeo ya ubunge na udiwani yatatangazwa baada ya saa 72 tangu
kutangazwa kwa matokeo ya rais.
Watu waliojiandikisha kupiga kura walikuwa milioni
7.5 na waliopiga kura walikuwa milioni 5.3 sawa na asilimia 70.78 na
kura zilizoharibiika ni 56,675.
Awali, MEC iliiomba Mahakama Kuu ya Malawi iongeze
siku 30 ili itangaze matokeo baada ya kumaliza kurudia kuhesabu kura,
lakini mahakama hiyo ilikataa na kuagiza yatangazwe jana.
“Sheria iko wazi, hakuna sababu yoyote ya kuongeza muda,” alisema Jaji Kenyatta Nyirenda.
Awali, Banda alifuta matokeo kutokana na kuibwa kwa kura na kukiukwa kwa taratibu nyingine za kuhesabu kura.
Banda alisema uchaguzi huo ungefanyika ndani ya siku 90 na kwamba asingegombea tena.
No comments
Post a Comment