Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, June 2, 2014

HOJA: ONGEZEKO LA UCHAWI MAKANISANI TANZANIA (2)

Katika toleo lililopita niliwasilisha makala haya kuhusu “ongezeko la imani za uchawi makanisa Tanzania” na kutoa takwimu za tafiti zilizofanyika ambazo zimeiweka Tanzania kuongoza kimataifa kwa uchawi katika Bara la Afrika. Takwimu za kutisha zilidai 93% ya watanzania wanaamini katika uchawi na kujihusisha na vitendo vya ushirikina na uchawi. Aidha niliweka bayana Madhumuni ya makala haya kuwa ni kuelimisha, kutahadharisha na kuonya kanisa kuonesha mamlaka ya Kristo aliyoliachia; na sio kutangaza imani potofu inayodai kwamba wachawi wa freemasons ndio wanaofanikiwa kiuchumi. Leo ninaendelea na uchambuzi wa hoja hii nyeti:

Marejeo ya athari za imani za uchawi makanisa

Askofu Sylvester Gamanywa

Madai yaliyotawala ndani ya baadhi ya makanisa ni “tuhuma-shirikina” zinazodai kwamba baadhi ya watu wanaoonekana kufanikiwa kiuchumi “makanisani”; hata kama ni wacha-Mungu lazima wamepata utajiri kwa za uchawi wa freemason. Hii ni pamoja na watumishi wa Injili ambao wanatokea kuwa na wafuasi wengi katika mikutano yao, au ibada zao, nao hutuhumiwa kutumia “ndumba za freemason”

Aidha, nidokeza bayana kwamba, kuongezeka kwa kasi ya hizi “tuhuma-shirikina” tayari kumekuwa “kichocheo” kwa baadhi ya waamini wenye “imani dhaifu” kujikuta wanashawiki kuwasaka akina freemason wakitaka kujua ni akina nani, wako wapi ili wajiunge na kuupata utajiri kama unavyotangazwa “makanisani”!

Athari nyingine mbaya zaidi itokanayo na “tuhuma-shirikina” ni kufuga tabia ya uvivu makanisani ambapo waamini hudhoofika kifikra na bidii ya kufanya kazi ambayo ndiyo njia muafaka ya kiuchumi; na kujengewa tabia ya “utegemezi wa maombezi ya kuvunja laana” kama njia peke ya kufanikiwa kiuchumi! Ile mantiki nzima ya “maombezi” imepoteza mwelekeo wake wa Kibiblia!

Hata hivyo, nilitahadharisha mapema kwamba sipingi wala sikatai kuwepo kwa uchawi na wachawi. Pia siko kinyume na huduma halisi za kukemea pepo wachafu na roho za mizimu ya uchawi. Nilikiri na kuthibitisha na kutambua utekelezaji wa agizo kuu la Yesu Kristo aliposema “kwa jina langu watatoa pepo”! Ninachopinga ni hali ya kupoteza mwelekeo ambapo “kutoa pepo” kumemezwa kiushirikina na “kupunga pepo”!

Kama nilivyobanisha kuhusu madhumuni ya makala, na bado nasisitiza kwamba, nia ni kuelimisha, kutahadharisha na kulionya kanisa kwa upendo na upole, lirudi kwenye wito wake asilia wa kuidhihirisha mamlaka ya Kristo lilioachiwa; badala ya kutangaza na kutukuza nguvu za uchawi wa freemason!

Historia ya Nimrodi mwasisi wa Uchawi

Nimrodi ni mtoto wa Kushi, mjukuu wa Hamu ambaye ni mwana wa Nuhu! Imeandikwa Nimrodi alikuwa hodari wa kuwinda wanyama mbele za BWANA. Yeye ndiye mwasisi wa ufalme wa Babeli pamoja na “tawala za kifalme” za Ereku, na Akadi, na Kalne katika nchi ya Shinari. Ni huko huko katika nchi ya Shinari Biblia imeandika:

Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana, haya, na tufanye matofari tukayachome moto. Walikuwa na matofari badala ya chokaa. Wakasema, haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.” (Mw.11:2-4)

Kwa kupitia maandiko haya, inasadikiwa kuwa ndio mwanzo wa imani za uchawi ambazo mwasisi wake ni Nimrodi. Wengine wanatafsiri kwamba, kile ambacho Nimrodi alikuwa anakijenga sio mnara wa kawaida ambao alikusudia ufike mbinguni, bali ulikuwa alikuwa akiongozwa na nguvu za uchawi katika ujenzi huo, na ndio maana ilibidi Mungu mwenyewe kuingilia kati ili kusitisha uchawi huo:

BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni pa nchi yote.” (Mw.11:5-9)

Mfano wa mnara wa Babeli

Mnara wa Babeli ulikuwa ni ishara ya uasi wa Nimrodi dhidi ya kusudi la Mungu ambapo aliwaagiza binadamu kutawanyika duniani kote. Nimrodi akafanya ushawishi wake wa kugoma na kujenga mnara utakaofika mbinguni ili “binadamu wasipate kutawanyika duniani”!

Katika kisa hiki, tunajifunza kwamba, kila mbinu inayopangwa kwa hila au kwa nia ya kupingana na kusudi la Mungu; mwenye kuidhibiti isifanikiwe na Mungu mwenyewe na si vinginevyo.

Nguvu za uchawi na uganga dhidi ya Musa

Suala la nguvu za uchawi kupingana na mpango wa Mungu halikuishia kwa Nimrodi, bali lilienea kwa makabila mengine mpaka nchi ya Misri. Inasadikiwa miungu ya uchawi wa kimisri asili yake ni Nimrodi. Tunaweza kuthibitisha katika maandiko wakati Mungu alipomtuma Musa kwa Farao ili kuwakomboa wa Israeli. Wakati Musa alipotenda muujiza wa kwanza wa kugeuza fimbo iwe nyoka mbele za Farao; tunasoma kwamba Farao naye aliita wachawi na waganga ambao nao walifanya muujiza ule ile:

"Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.  Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.  Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao." (KUT. 7:10-12)

Kama ilivyo ada, ushindi wa wachawi na waganga wa Farao ulikuwa ni wa muda, kwani Mungu ilibidi athibitishe uwezo mkubwa zaidi ya ule wa Farao kwa fimbo ya nyoka wa Haruni kuzimeza nyoka zote!

Haya, muujiza mwingine ambao, wachawi walichuana na Musa ni pale Musa alipopiga maji ya mtoni yakageuka damu na samaki wote wakafa:

"Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu.  Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri.  Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena." (KUT. 7:20-22)

Mashindano haya ya miujiza kati ya Musa na wachawi wa Farao yaliendelea. Kila Musa alipofanya muujiza wachawi na waganga nao walifanya vile vile:

"Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri.  Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri." (KUT. 8:6, 7)

Jambo ambalo mpaka leo linanishangaza kibinafsi ni hili. Hawa wachawi walikuwa na uwezo wa kuigiza miujiza ambayo ni mapigo ya Mungu kwa Wamisri. Bila wao kutafakari kila walipofanya miujiza ya Musa ni sawa na kuipiga Misri mara mbili! Kwa maelezo mengine, pamoja na kuonesha umahiri wao, bao walijikuta wakiungana na nia ya Miujiza ya Musa ya kumwadhibu Farao badala ya kuzuia adhabu hiyo! Mfano wachawi hawa walipoigiza muujiza wa vyura, bado walishindwa kufanya muujiza wa kuondoa vyura hao mpaka Musa alipomwomba Mungu:

Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia BWANA katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.  BWANA akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.  Wakawakusanya chungu chungu; na nchi ikatoa uvundo. (KUT. 8:12-14)

Hatimaye, Mungu ilibidi aanze kuwadhibiti wachawi wa Farao ili kuonesha kwamba, uchawi wao hauna mamlaka ya kuigiza kila muujiza wa Mungu:

BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.  Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.  Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.  Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.” (KUT. 8:16-19)

Habari kwa hisani ya http://www.bbc.co.uk/swahili

« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment