Writen by
sadataley
5:38 PM
-
0
Comments
Kipa wa Hispania, Iker Casillas (kulia) akijinamia huku mshambuliaji wa
Uholanzi, Arjen Robben (katikati) na kiungo Wesley Sneijder
wakishangilia baada ya Robben kufunga bao la tano wakati wa mchezo
uliozikutanisha timu hizo Fonte Nova, Salvador. Picha zote na AFP
Salvador, Brazil. Kipa na nahodha wa Hispania,
Iker Casillas alipotea kabisa, Gerard Pique alizidiwa mbio na Sergio
Ramos alifanya uzembe wa hali ya juu.
Nini kilichoikuta ngome ya Hispania ambayo kwa kawaida inasifika kwa umakini?
Ngome hiyo ya Hispania ndiyo iliwasaidia kunyakua
mataji matatu makubwa mfululizo, lakini Ijumaa ilikuwa tofauti baada ya
kuruhusu mabao 5-1 kutoka kwa Uholanzi, hicho kikiwa ni kipigo cha
kwanza kikubwa kwa mabingwa hao watetezi wa dunia tangu walipofungwa
namna hiyo mwaka 1950.
‘’Sijui ni neno gani zuri la kuelezea hiki
kilichotukuta,’’ alisema kocha Vicente del Bosque. ‘’Sitaki kumlaumu
yeyote. Kufungwa kwa timu hakuwezi kuwa sababu ya mtu mmoja. Sitaki
kumnyooshea kidole (Casillas) au yeyote.’’
Casillas alitoa zawadi ya bao la pili la Robin van
Persie wakati kipa huyo wa Real Madrid alipoteleza kabla ya kupigwa
chenga na Arjen Robben aliyefunga bao la tano.
“Nilishindwa kufanya vitu vile nilivyozoea, hasa
katika mchezo huu wa ufunguzi wa Kombe la Dunia,’’ alisema Casillas.
“Haikuwa siku yangu nzuri, sikuwa kwenye kiwango changu cha kawaida.
Nakubali kupokea lawama zote.’’
Pique alipitwa kirahisi na Robben alipofunga bao la kwanza na pia alizidiwa mbio na Mdachi huyo alipofunga bao la pili.
“Kipindi cha pili kilikuwa kibaya zaidi kwetu,’’ alisema Pique. “Tulipotea kabisa mchezoni.’’
Katika mchezo mmoja, Hispania imeruhusu mabao mengi kuliko magoli waliyofungwa kwenye fainali mbili walizochukua ubingwa.
Mara ya mwisho kupokea kipigo cha aina hii ilikuwa
katika fainali za mwaka 1950 zilizofanyika Brazil, na Hispania
walinyukwa 6-1 na wenyeji Brazil.
No comments
Post a Comment