Writen by
sadataley
7:48 PM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewasihi
viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea katika vikao vya
Bunge Maalumu la Katiba vinavyotarajiwa kuendelea tena kuanzia Agosti 5
mwaka huu.
Amesema kama tatizo la wajumbe wa umoja huo
kususia vikao vya Bunge hilo wiki moja kabla ya kuahirishwa kwake ni
kejeli na matusi kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman
Mbowe, jambo hilo linazungumzika.
Waziri Pinda alitoa kauli hiyo jana wakati wa
kuhitimisha na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za wabunge
waliochangia hotuba ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2014/15.
Mei 7 mwaka huu, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akitoa hotuba yake kuhusu Bajeti ya
Waziri Mkuu, alisema wajumbe wa Ukawa hawatarejea katika Bunge la Katiba
mpaka watakapohakikisha kuwa maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo
unafuatwa.
Alisema kama lengo ni kutumia mwamvuli wa Bunge
Maalumu la Katiba ili kuendeleza mfumo wa kikatiba na muundo wa muungano
uliopo sasa, wajumbe wa Ukawa hawatakuwa sehemu ya usaliti huo kwa
Watanzania, huku akisisitiza kukerwa kwake na lugha za matusi na kejeli
dhidi yao zilizokuwa zikitolewa na wajumbe kutoka chama tawala.
Hata hivyo Pinda jana alisema “Kauli zilizotolewa
na Mbowe zilikuwa kali na zilinitisha kidogo. Nadhani tusianze kutoa
picha kwa Watanzania juu ya hali ya kutokuwepo kwa amani katika siku
zijazo kwa sababu jambo hili siyo zuri,” alisema Pinda na kuongeza;
“Nadhani kubwa hapa ni kuendelea kuzungumza juu ya uwezekano wa namna ya kufikia hatima nzuri juu ya mchakato wa Katiba.”
Pinda alisema sababu za lugha za kejeli na matusi
zilizotolewa na Mbowe siyo sababu ya msingi ya kuwafanya wajumbe wa
Ukawa kususia vikao vya Bunge hilo.
“Hata kama tungefikia mahali tukavutana sana,
suluhu haikuwa kutoka nje ya Bunge. Hata kama mngesema liahirishwe ili
tukajadiliane na kukubaliana na kisha kurejea na kuendelea na mjadala,
sidhani kama lingekuwa tatizo.”
Waziri Pinda alisema Rais Jakaya Kikwete hakuwa
chanzo cha kuvuruga mchakato wa Katiba kama ilivyoelezwa na Mbowe na
kufafanua kuwa Rais Kikwete kama wananchi wengine naye alikuwa akitoa
maoni yake na kwamba alieleza wazi kuwa wabunge ndiyo wenye uamuzi wa
mwisho.
Huku akiwataja wajumbe kadhaa wa Ukawa, Pinda
alisema: “Bado naamini Mbowe, James Mbatia, John Cheyo na Profesa
Ibrahim Lipumba tunaweza kuzungumza, maana kama hoja ni matusi na
kejeli, hivi tukikubaliana si tunarudi na kukubaliana kutokuwapo kwa
vitu hivyo.”
Alisema kuwa anaunga mkono kauli ya Mbowe ya kukutanisha makundi yote yanayopingana ili kuzungumza ili yaweze kukubaliana.
“Kuna hoja kuwa CCM tuko wengi bungeni, hilo lipo sahihi lakini
wingi wetu usiwe nongwa. Wingi huu unatokana na ridhaa tuliyopata kutoka
kwa wananchi,” alisema na kuongeza: “Jambo la msingi ni kuendelea
kuona hoja zinazojengwa zinakubalika na pande mbili. Sitaki kuamini
kwamba wachache muda wote wako sahihi na wengi hawako sahihi.”
Mgogoro wa Kiteto
Waziri Pinda pia aligusia migogoro ya ardhi baina
ya wakulima na wafugaji katika hifadhi ya jamii ya Emboley Mortangosi
wilayani Kiteto mkoani Manyara na kufafanua kuwa uamuzi wa awali wa
mahakama unatakiwa kuheshimiwa kuhusu umiliki wa eneo hilo.
“Njia rahisi ilikuwa kupeleka jeshi na kuwaondoa
wakulima wote. Ila jambo hilo haliwezi kufanyika na nadhani suluhu ya
kweli ni kuzungumza na vijiji vyote saba vilivyopo katika eneo hilo ili
vitoe uamuzi kama vinataka eneo hilo kuendelea kuwa hifadhi au kila
kijiji kuchukua eneo lake,” alisema Pinda.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe na Daniel Mjema
No comments
Post a Comment