Writen by
sadataley
9:32 AM
-
0
Comments
Na Habel Chidawali na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),
David Kafulila jana aliibua tuhuma nzito bungeni akiwahusisha mawaziri
wawili na Sh200 bilioni zilichotwa katika Akaunti ya Escrow, iliyokuwa
inamilikiwa kwa pamoja kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya
IPTL.
Katika tuhuma hizo, alimuunganisha pia Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na
vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wa Serikali,
wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa
Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu
Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick
Werema.
Kafulila alitoa tuhuma hizo bungeni alipokuwa
akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri
Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/15.
Mbunge huyo alisema fedha zilizoibwa katika
Akaunti ya Escrow ni nyingi kuliko zile zilizoibwa katika kashfa ya
Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT mwaka 2005.
“Pamoja na hilo, Watanzania wamekuwa wakisikia
kwenye vyombo vya habari kwamba Tanesco wakati ilipokuwa na mgogoro na
IPTL walifika mahali wakafungua akaunti ya Escrow,” alisema.
Mbunge huyo alisema akaunti hiyo ilifunguliwa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2004 na hadi jana, akaunti ile
ilishafikia Dola za Marekani 122 milioni,” alisema Kafulila.
Alisema fedha hizo ziliwekwa kwa lengo maalumu
kutokana na mgogoro uliokuwapo kati ya IPTL na Tanesco ili ziweze
kusaidia malipo baada ya mgogoro kuisha katika Baraza la Usuluhishi wa
Kibiashara la ISCID.
Alitaka jambo hilo liingie kwenye rekodi kwa kuwa
linahusu BoT na vigogo akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa
Nishati na Madini pamoja na Katibu wake na pia Waziri wa Fedha.
Alisema wakati Tanesco ikidaiwa madeni zaidi ya
Sh400 bilioni, viongozi hao wameidhinisha kugawanywa kwa fedha hizo
kihuni jambo alilosema halivumiliki hata kidogo.
Kafulila alisema fedha hizo zilichotwa na Kampuni
ya PAP aliyosema ya “Singasinga na ya kitapeli” ambayo iliidhinishiwa
kuchota fedha hizo kinyume na utaratibu.
Alisema fedha hizo hazikupaswa kuchukuliwa kwa kuwa kulifanyika
udanganyifu mkubwa kwamba PAP ilikuwa imenunua IPTL wakati jambo hilo si
la kweli.
Alisema IPTL ilikuwa na makubaliano ya kufanya
kazi kwa kampuni mbili ambazo ni VIP Engineering ya Tanzania iliyokuwa
na hisa asilimia 30 na Mecmer ambayo ilikuwa na asilimia 70 ya hisa.
Hata hivyo, alidai kuwa anao ushahidi kuwa PAP
ilikuwa imenunua hisa za VIP na hakukuwa na vielelezo vya kununua Mecmer
kwa kuwa kampuni hiyo tayari ilishapoteza uhalali wake kwa kuwa ilikuwa
chini ya muflisi nchini Malaysia.
Aliliambia Bunge kuwa wakati wa uchukuaji wa fedha
hizo kutoka BoT, ilipaswa kulipiwa kodi lakini zilichukuliwa kinyemela
bila hata ya kulipiwa kodi.
Alisema TRA iliiandikia Hazina na nakala kwa BoT
kwamba wakati wa kulipa fedha hizo lazima kodi ikatwe, lakini cha ajabu
hilo halikufanyika licha ya kukumbushwa.
“Kwa mfano, tulimwita Gavana katika kikao chetu
cha Kamati ya Uchumi pale Bagamoyo na alikiri kuwa alibanwa na viongozi
wa juu kiasi cha kushindwa kufurukuta, kwa hali kama hiyo Naibu Spika
unategemea nini?” alihoji.
Kafulila alisema, Gavana katika kikao hicho
alikiri kuwa, kulikuwa na presha (shinikizo) ambazo asingeweza kuzizuia
na kuwa alikuwa amejitahidi kwa kiasi kikubwa hadi kufikia alipofika.
Alisema ISCID lilitoa hukumu ndogo Februari, mwaka
huu kuwa Tanesco na IPTL wakae pamoja na kupitia hesabu zao namna
watakavyogawanya fedha hizo na walipewa siku 60 ambazo mwisho wake
ulikuwa jana.
Aliituhumu Tanesco kuwa katika makubaliano hayo
ilikataa kukaa meza moja na kufanya hesabu za namna ya kulipana jambo
alilosema linaonyesha ilidhamiria kufanya hivyo.
“Kwa sababu wanajua kuwa fedha ile ilishaliwa na
wajanja wachache, Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili kwa vyovyote halikubaliki
na halivumiliki kwa sababu Dola122 milioni ni zaidi ya Sh200 bilioni
ambazo ni nyingi kuliko za EPA, lazima litoke na mtu.”
Alisema hayuko tayari kuona fedha hizo zikitafunwa
bila ya utaratibu na akashangazwa kuona Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akishindwa kuchukua hatua.
Akoleza moto jioni
Katika kikao cha jioni, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu
alimwita tena Kafulila kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa mchana,
ambayo iliombewa mwongozo na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina kwamba
Gavana alishinikizwa kutoa fedha hizo.
Wakati wa mwongozo huo, Kafulila hakuwapo na ndiyo
sababu ya Mwenyekiti kumpa nafasi ya kufuta kauli yake kuwa Gavana
alishinikizwa. Hata hivyo, Kafulila alikazia akisema alishinikizwa kutoa
fedha hizo.
“Gavana aliwahi kuniambia, mnanionea bure.
Kulikuwa na presha kubwa sana kuhusu fedha hizi… ukweli ni kwamba IPTL
inabadilishwa tu rangi na watendaji ni walewale.”
Baada ya Kafulila kuzungumza, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama
na kusema: “Tuhuma dhidi ya Gavana wa Benki Kuu zinatolewa kwa kuwa
hawezi kuingia bungeni kujitetea.
“Lakini Gavana tulimuuliza na akakanusha kuwa
aliwahi kuyatamka hayo maneno na kiongozi wa shughuli za Serikali
bungeni atakuja kufafanua jambo hili kesho (leo) katika hotuba yake,”
alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee
alisimama kuomba mwongozo akisema: “Kamati ya Bunge iundwe ili
tuchunguze fedha hizi za Escrow zimekwenda wapi? Kafulila ana ushahidi
wa kutosha, kwa nini hamtaki athibitishe?
“Vikao vyote vya kamati vinawekewa kwenye
kumbukumbu rasmi (hansard) ili kujua kama Gavana alitoa maneno hayo ama
hakutoa, iundwe kamati ijulikane mbivu na mbichi na wezi wa fedha za
Escrow tunao humu ndani ya Bunge.”
No comments
Post a Comment