Writen by
sadataley
12:11 PM
-
0
Comments

Mwenyekiti wa Chama cha wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam jana. Picha na Raphael Lubava
Na Joyce Mmasi, Mwananchi
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama
cha Wananchi (CUF), limelaani kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana aliyoitoa katika mikutano yake Zanzibar na kusema kuwa ina lengo
la kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
jana kuwa, kauli hizo zilizotolewa na viongozi wa CCM kuhusu SUK ni za
kichochezi zinazopandikiza mbegu za chuki na vurugu inayoweza
kusababisha maafa makubwa.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatokana na maoni
ya Wazanzibari wote na imesaidia kuleta amani na utulivu Zanzibar….
kauli za kuchochea kuivunja zinapandikiza mbegu ya chuki na vurugu,”
Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema Baraza Kuu pia limelaani kauli iliyotolewa
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kuwa
Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa siyo raia wa Zanzibar na
kuiita kuwa ya kibaguzi yenye lengo la kupandikiza chuki dhidi ya
Wazanzibar na Watanzania wenye asili ya Kiasia.
Wiki iliyopita, katika mkutano wa hadhara wa CCM
ulioongozwa na Kinana kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja, Mnadhimu
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Salmin Awadh Salmin alisema
wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza
hilo ili kuwapa nafasi wananchi wahoji iwapo wanataka kuendelea na SUK
au la.
Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo
kwa kuwa wanaona lengo na matumaini ya kuundwa kwake yamefutika na
hayana dalili njema katika siku za usoni.
Katika mkutano huo, Kinana alinukuliwa akisema
kuwa kwa miaka 20 tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu wa
CUF, Seif Shariff Hamad amekuwa akiwayumbisha Wazanzibari kutokana na
tabia yake ya kubadilisha ajenda za kisiasa na kutikisa misingi ya umoja
wa kitaifa nchini.
Alisema tabia ya kiongozi huyo imekuwa haifahamiki
na haijulikani anatafuta jambo gani licha ya kuwa Makamu wa Kwanza wa
Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa mwaka 2010 na CCM na
CUF.
Msimamo wa CUF kuhusu Ukawa
Profesa Lipumba alisema CUF inawahakikishia
Watanzania wote kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka chama
hicho hawatarudi katika Bunge Maalumu hadi pale litakapojadili na
kuiboresha Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
“Tutashirikiana na wajumbe wote wa Ukawa katika
mapambano ya kudai Katiba ya wananchi, tunawaomba wananchi waunge mkono
juhudi hizi za kupigania kuheshimika kwa maoni yao katika kupata Katiba
Mpya,” alisema.
Alisema Baraza Kuu la Uongozi la CUF, limeupongeza
Ukawa kwa uamuzi wa busara wa kujiondoa kwenye Bunge la Katiba kwa kile
walichoeleza kuwa lilipoteza mwelekeo na wajumbe walio wengi wakifuata
maelekezo ya CCM ya kuacha kujadili rasimu iliyokuwapo na kujadili mpya
yenye mfumo mpya ambao haukupendekezwa na wananchi.
Aliongeza kuwa, CUF inatoa wito kwa viongozi waliounda Ukawa
kuendeleza umoja huo na kufahamu kuwa wananchi wamepata moyo na hamasa
mpya baada ya kuanzishwa kwa umoja huo na kwamba wasikubali kugawanywa
na CCM.
“Baraza Kuu la CUF linampongeza Kiongozi wa Kambi
ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kwa ukomavu wa kisiasa aliouonyesha
wa kuvunja kambi rasmi iliyokuwa ikiundwa na chama kimoja na sasa
kuvishirikisha vyama vingine, kikiwamo CUF.”
Bunge la Bajeti
Profesa Lipumba alisema CUF kimebaini kuwa nidhamu
ya bajeti imeendelea kuporomoka na kutolea mfano wa bajeti ya 2013-2014
kwamba haikutekelezeka kutokana na makadirio ya mapato kuonekana
makubwa kuliko hali halisi ya ukusanyaji.
Alisema CUF inalaani utaratibu aliouita mbovu wa
misamaha holela ya kodi ambayo husababisha upotevu wa fedha za
Watanzania. Alisema kwa mwaka huu wa fedha, zaidi ya Sh2 trilioni
zimepotea kutokana na misamaha hiyo.
No comments
Post a Comment