Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, April 26, 2014

Warioba: Matusi, uongo vinaniumiza

Jaji Joseph Warioba 
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wametumia vibaya Bunge hilo kwa kumshambulia na kumsingizia mambo ya uongo kwa makusudi, akisema matusi yanayotolewa dhidi yake yanamuumiza.
Aidha, Warioba amesema ingawa haelewi kwa nini wanaomshambulia wameamua kutumia lugha za matusi dhidi yake binafsi, hatajutia kuchaguliwa kuiongoza tume hiyo kwa kuwa ilikusudia kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa kuwapatia Katiba wanayoitaka.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na viongozi wa CCM wakiikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kwa maneno makali,huku wakimshutumu na kumkejeli yeye na baadhi ya wajumbe wa tume aliyoiongoza.
Akizungumza kwa mifano katika mahojiano na gazeti hili jana, Warioba alisema kuwa anawashashangaa wajumbe hao na viongozi wa CCM kwa kuacha kuijadili Rasimu ya Katiba, badala yake wanamkosoa yeye na kumsingizia maneno yasiyo ya kweli.
“Bulembo (Abdallah Bulembo mjumbe wa Bunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM) amenitukana, amenitukana… amesema niliwahi kupokea rushwa huku akijua kabisa kuwa ni uongo. Yeye ni kiongozi wa Kamati Kuu ya CCM, anasema uongo akijua ni uongo. Kwanza mimi simjui wala sijawahi kumwona huyu mtu naambiwa tu anatoka Mara,” alisema Jaji Warioba kwa sauti ya upole iliyoashiria kuumizwa.
Aliongeza kwamba siyo mara ya kwanza kwa Bulembo kumshambulia kwa lugha za matusi, kwani aliwahi kufanya hivyo tena kwenye moja ya mikutano ya CCM mkoani Tanga.
“Alifanya hivyo Tanga, anachokifanya siyo kitu cha mzaha kwa sababu anafahamu kilichotokea,” alisema.
Akizungumzia kauli aliyoitoa Waziri Hawa Ghasia wakati akichangia mjadala wa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba aliyemtaka Jaji Warioba kufunga mdomo kutokana na kazi yake ya kuwasilisha Rasimu kumalizika, Jaji Warioba alisema: “Wao wanataka waseme uongo, mtu mwingine asiseme kitu.”
Warioba alieleza kuwa tangu lugha za matusi na kejeli zilipoanza kutolewa dhidi yake, baadhi ya watu walimshauri kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini alikataa kwa kile alichodai kuliheshimu Bunge.
Alisema Bunge ndiyo lenye mamlaka ya kufuatilia na kudhibiti kauli zinazotolewa bungeni, kama wahusika hawafanyi hivyo hawezi kuchukua hatua yoyote.
“Kama kinga ya Bunge inatumika vibaya unafikiri mimi nitafanya nini? Sina nia ya kuchukua hatua, watu walipendekeza niende mahakamani, kuna wanasheria walisema hata nisipokwenda, wao watakwenda mahakamani nikawazuia,” alisema Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu.
Akisimulia kuhusu uchaguzi wa ubunge wa mwaka 1995 ambapo aligombea na kutuhumiwa kupokea rushwa na kufungiwa kwa miaka minne, Warioba alisema taarifa hizo siyo sahihi kwa kuwa aliyepokea rushwa ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi (wakati huo), Stephen Wassira ambaye sasa yuko CCM na ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu.
“Uchaguzi ule ulikuwa umejaa sana rushwa, tukaenda mahakamani, Wassira akafungiwa asigombee,” alisema.
Akizungumzia maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Warioba alisema: “Mimi ni muumini wa muungano, kwa miaka 50 taifa limekaa kwa amani, mshikamano na umoja. Ni kweli tumekuwa na matatizo lakini yanaweza kutafutiwa ufumbuzi.”
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment