Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, April 26, 2014

Kingunge apinga matusi, kejeli dhidi ya Warioba

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru akizungumza katika kikao cha Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi  
Na Habel Chidawali, Mwananchi
Dodoma. Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru amekemea kauli za kejeli na matusi dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba, alisema wanaombeza Warioba wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa hawamtendei haki.
“Siyo sawa hata siku moja kumshambulia Warioba eti kwa sababu ya misimamo yenu ya vyama, hata mimi japo nimestaafu lakini bado ni mwanaCCM kwa hiyo tabia hii ni mbaya na haileti heshima,” alisema Kingunge.
Alisema kuwa misimamo ya vyama inapotokea kuwatukanisha watu tena wenye heshima zao inakuwa ni aibu kwa chama pamoja na jamii kwa jumla na inaondoa heshima ya mtu.
Kauli ya Kingunge imekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kujitokeza kwa hali ya mashambulizi ya matusi ndani ya Bunge ambayo yalikuwa yakielekezwa kwa Warioba kuhusu tuhuma za kuchakachua maoni ya wananchi.
Tuhuma za hivi karibuni zilitoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia ambaye alimtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani kufunga mdomo wake kwa kuwa kazi yake imekwisha.
Mbali na huyo, Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba alimfananisha Warioba na Adam na Hawa ambao waliasi katika Bustani ya Edeni.
Akizungumzia Rasimu, mkongwe huyo alisema Katiba haitapatikana pasipokuwapo na maridhiano na makubaliano na akawataka wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba warudi bungeni ili waweze kujadiliana na kutengeneza katiba ya wananchi.
Kingunge aliwasifia waganga wa tiba za jadi kwa kumpendekeza kama mlezi wao tangu 1998 ili aweze kuwawakilisha hivyo akasema hakubebwa wala kupita njia za panya kama ambavyo wengine wanasema.
Pinda awaomba Ukawa warudi bungeni
Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alitumia dakika 13 alizopewa na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kuwaomba wajumbe wa kundi la Ukawa kurejea bungeni ili waweze kukubaliana katika utungwaji wa katiba ya wananchi.
Pinda alisema, “Yaliyopita si ndwele, naomba nitumie nafasi hii kuwasihi sana hawa ndugu zetu waliosusia Bunge, warudi tukubaliane pamoja katika kutengeneza katiba ya wananchi.”
Hata hivyo, alikiri ofisi yake kutuma maoni kuhusu muundo wa serikali tatu lakini akakanusha kuwa yeye hakuhusika bali waliotuma ni watumishi katika ofisi yake na walifanya hivyo kwa utashi wao.
Kwa mujibu wa Pinda yeye, alipeleka mawazo yake kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu ambayo hayakuzungumzia serikali tatu kwa hiyo mawazo ya watumishi ofisini kwake yasibebeshwe kuwa ndiyo mawazo yake.
Sitta asita kutoa adhabu
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alitoa sababu za kutowachukulia hatua baadhi ya wajumbe ambao walionekana kuwa na shida ndani ya bunge akisema ilitokana na busara za kiti chake kuepusha migogoro zaidi.
Sitta alisema katika kutoa uamuzi, walikubaliana na Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan kwamba kama wangechuka uamuzi wowote huenda wangesababisha migogoro zaidi  kwa wajumbe.
“Tulishauriana na Makamu wangu kuwa tutasababisha mambo mengi hapa ikiwamo kuongeza matusi na kwa hiyo busara tulizitanguliza mbele,” alisema Sitta.
Mwenyekiti huyo aliahirisha shughuli za Bunge la Katiba hadi Agosti 5 mwaka huu ili kupisha Bunge la Bajeti ambalo linatarajiwa kuanza vikao vyake Mei 5 mjini Dodoma.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment