Writen by
sadataley
10:40 AM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu,Mwananchi
Dodoma na Dar. Bunge Maalumu la Katiba limeomba kuongezewa muda wa siku 60 kuanzia Agosti 5, mwaka huu litakapokutana kwa ngwe ya pili, Mwananchi limebaini.
Bunge hilo linahitimisha ngwe yake ya kwanza Aprili 25, mwaka huu likiwa limekutana kwa siku 67, kati ya 70 zilizokuwa zimetengwa awali.
Kwa muda huo wa ziada 60, iwapo wajumbe wote 629 watalipwa posho ya Sh300,000 iliyopangwa kwa siku, jumla ya Sh11.322 bilioni za walipakodi zitatumika ukilinganisha na Sh13.209 bilioni zilizotumika katika siku 70 za awali. Jumla ya fedha zote zitakazotumika kwa posho ni Sh24.53 bilioni, bila kuingiza gharama nyingine nje ya posho za wajumbe.
Jana, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alitangaza kwamba shughuli za Bunge hilo zitakoma wakati wajumbe wake watakapokwenda kusherehekea maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, Aprili 26, mwaka huu.
Sitta alisema jana kwamba aliwasilisha maombi ya kuongezewa muda kwa Rais Jakaya Kikwete, ambayo yalikuwa hayajajibiwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alipoulizwa jana alisema: “Mheshimiwa Rais (Kikwete) anachoafiki ni kama ambavyo kila mtu anaona mwenendo wa Bunge ulivyo, kwamba siku 70 haziwatoshi, hivyo alikubali kwamba wanahitaji kuongezewa muda. Ingawa mpaka sasa hajaamua atawaongezea siku ngapi, atakapoamua tutawafahamisha tu.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema upo uwezekano mkubwa wa Bunge hilo kuongezewa siku 60 lakini akaongeza kuwa hilo litategemea bajeti itakayoidhinishwa na Serikali.
“Kwa kuwa kazi hii ndiyo kwanza iko katika hatua zake za kwanza, ndiyo maana mchakato wake umesogezwa mbele mpaka Agosti mwaka huu,” alisema Jaji Werema.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema: “Mwenyekiti hajanipa taarifa rasmi kwamba tutakutana kwa siku ngapi, ila ninachofahamu ni kwamba tunasubiri barua rasmi kutoka kwa Rais.”
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, nyongeza ya muda wa kukutana kwa Bunge hilo inatolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Hamad alisema tayari Sitta alishawasilisha maombi ya kuongezewa siku za Bunge hilo kukutana, lakini akasema hana hakika kama majibu tayari yamerejeshwa.
Hamad alisema wakati Bunge litakapoahirishwa litakuwa limebakiza siku tatu, ambazo zitafidiwa wakati watakapokutana Agosti 5
Mmoja wa maofisa wa Bunge Maalumu alisema siku zilizoongezwa ni 60 na kwamba tayari yeye na maofisa wenzake walikuwa wanaandaa ratiba ya siku hizo.
Katika siku ambazo Bunge hilo limekutana limefanya kazi ya kuandaa na kupitisha kanuni za uendeshaji wake, kuchagua viongozi wa Bunge Maalumu na kujadili sura mbili kati ya 17 za Rasimu ya Katiba.
Katika hatua nyingine, Hamad alisema wanakusudia kuifanyia marekebisho Kanuni ya 35 (6) ya Bunge hilo ili kuruhusu Kamati ya Uandishi kufanya kazi ya majumuisho ya michango ya wabunge kuhusu Ibara ya Kwanza na ya Sita ambazo zinaendelea kujadiliwa.
“Kwa mujibu wa Kanuni ya 35 (6), Kamati ya Uandishi haiwezi kufanya kazi kabla ya Bunge kufanya uamuzi wake, sasa tunataka kamati hiyo ifanye majumuisho yake kisha ilete mbele ya Bunge ambalo litafanyia kazi majumuisho hayo,” alisema Hamad.
Alisema Kamati ya Uongozi ilielekeza Kamati ya Kanuni ikutane ili kuandaa marekebisho ya kanuni hiyo ambayo yatawasilishwa bungeni kufanyiwa uamuzi.
No comments
Post a Comment