Writen by
sadataley
10:32 AM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mapema mwaka huu, iliibua madudu mengi ambayo hayajawekwa hadharani.
Wajumbe waliounda kamati hiyo kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa waligundua mambo mengi yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini.
Sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo inasemekana yamejikita zaidi katika kuzitupia lawama taasisi za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Udhaifu wa kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili unadaiwa umechangia kwa wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye mitihani ya Kidato cha Nne mwaka jana kiasi cha kuilazimisha Serikali kuunda tume kuchunguza tatizo kutokana na kilio kikubwa cha wadau wa elimu na wananchi.
Viongozi watatu waandamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hawakupatikana kuzungumzia uchunguzi huo jana.
Simu ya Waziri wa wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa haikupatikana kabisa pale ilipopigwa.
Naye Naibu wake, Philipo Mulugo alijitetea kwamba alikuwa na shughuli nyingi na hivyo hakuwa na muda wa kuzungumzia suala hilo wakati Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome hakupokea kabisa simu yake.
Matokeo hayo ya mtihani wa Kidato cha Nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wakiwa wamepata daraja la nne. Katika mtihani huo, watahiniwa 397,136 walikuwa wa shule na 68,806 wa kujitegemea.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliamua kuunda tume iliyoanza kufanya kazi kuanzia Machi hadi Juni mwaka huu.
Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Mchome ilimkabidhi Waziri Mkuu ripoti Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijawahi kutolewa hadharani baada ya tume kumaliza kazi yake.
Badala yake imeshuhudiwa Profesa Mchome, ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania akipandishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.Huku kwa upande mwingine, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako akichukua likizo ya muda mrefu ya mapumziko.
Madudu yaliyogunduliwa na tume
Wajumbe wa tume hiyo walisema kuwa matokeo ya uchunguzi wao yalibaini kuwa, maswali na mitihani iliyotungwa ilikuwa ni ile yenye kuzingatia maudhui badala ya kuzingatia kujenga maarifa na ujuzi.
“Tulitegemea kwa vile tangu mwaka 2006, mihutasari ya elimu ya Tanzania ilibadilika kutoka ile inayozingatia maudhui, kwenda kwenye ile inayozingatia kujenga maarifa na ujuzi basi na mtihani ungekuwa na mwelekeo huo,” alisema mmoja wa wajumbe wa tume ile.
Pia uchambuzi wa kamati ile uligundua kuwa hakukuwapo mawasiliano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).
TET, ambao ndio wasimamizi wa mitalaa ya elimu walitakiwa kuhakiki mitihani ile baada ya kutungwa na Necta, lakini hilo halikufanyika.
Chanzo kingine kililiambia gazeti hili kuwa tume hiyo ilibaini katika uchunguzi wake kuwa Necta ilitumia wataalamu wasio na juzi wa kutosha kutunga na kuhakiki mitihani.
Uchunguzi huo ulibaini baadhi ya mitihani kama ya masomo ya Hisabati, Kemia na Fizikia ilikuwa na maswali yaliyohitaji muda mwingi wa kuyajibu kuliko uliopangwa.
“Hii ilifanya wanafunzi kushindwa kukamilisha kujibu maswali yote yaliyotakiwa kujibiwa kwenye mitihani hiyo. Pia tulibaini kwamba baadhi ya maswali katika mitihani ya masomo ya Fizikia na Kemia yalikuwa nje ya mihutasari iliyotumika kuwaandaa wanafunzi,” aliongeza mjumbe mwingine.
Mjumbe mmoja aliongeza pia kuwa mitihani ilikuwa na misamiati migumu na hata kuwasumbua walimu walioisahihisha.
Hali hii inaweza kuwa imechangia, kwa kiasi kikubwa, kuongeza ugumu wa mitihani hiyo na hili linaweza kuchangia wanafunzi kushindwa kuelewa vizuri maswali wanayoulizwa kwenye mitihani.
Wajumbe wa tume hiyo walieleza hali hiyo imefanya imani kujengeka kuwa mitihani ya Tanzania ni migumu kuliko ya nchi nyingine.Katika kuthibitisha suala la ugumu wa mitihani, Tume ilijiridhisha kwa kuwafanyisha mitihani walimu waliochaguliwa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
“Baada ya kuwafanyisha mitihani matokeo yake yalikuwa, asilimia 41.2 ya walimu waliotahiniwa walipata alama chini ya asilimia 50,” kilieleza chanzo chetu.
Pia Tume ya Pinda ililaumu hali ya kukosekana kwa utaratibu wa mrejesho kutoka shuleni kuhusu mada zilizofundishwa, uwezo wa wanafunzi na walimu, changamoto katika ufundishaji na kujifunza, pamoja na mambo mengine ambayo yanaweza yakafanya mtihani unaotungwa kuwa wa haki.
Taasisi zilizotupiwa lawama ni TET, wakaguzi wa shule (Wizara) na Necta.
Tatizo lingine lililogunduliwa na tume ile ni kukosekana kwa majadiliano kati ya Necta na wasahihishaji wa mitihani ile kuhusiana na majibu ya mitihani ili pande hizo ziweze kuangalia dosari zozote.
“Matatizo tuligundua kwenye masomo ya Kiswahili na Hisabati. Wasahihishaji walitoa alama zilizostahili na hakukuwa na utaratibu makini wa kubaini upungufu wa aina hii katika usahihishaji,” alieleza mjumbe mmoja.
Tume hiyo inasemekana ilibaini katika somo la hisabati kwa mfano kuna mtahiniwa aliyejibu swali ambalo halikuwepo kwenye mtihani na kupewa alama 12.
Wajumbe wa Tume ya Pinda
Tume iliundwa na wajumbe 15, chini ya Profesa Mchome na Makamu wake alikuwa Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalumu – Kagera).
Wajumbe wengine walikuwa James Mbatia (Mbunge wa Kuteuliwa), Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Profesa Mwajabu Possi (Chuo Kikuu – UDSM), Honoratha Chitanda (CWT) na Daina Matemu (TAHOSSA) na Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).
Wengine ni Rakhesh Rajani (Twaweza), Peter Maduki (CSSC), Nurdin Mohamed (Bakwata), Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi), Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu – Suza), Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Z’bar na Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala).
No comments
Post a Comment