Writen by
sadataley
8:48 PM
-
0
Comments

Bunge nchini Kenya lilikutana kwa dharura Alhamisi iliyopita kujadili hoja ya kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), iliyowasilishwa na Aden Duale, mmoja wa wabunge wa Muungano wa Jubilee ulioshinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu na kuunda Serikali chini ya Rais Uhuru Kenyatta. Kama ilivyotarajiwa, hoja hiyo ilipitishwa na Bunge siyo tu kutokana na wingi wa wabunge wa Umoja huo, bali pia kususiwa na wabunge wa vyama vya upinzani.
Hatua hiyo ya Bunge imekuja muda mfupi kabla ya kuanza kusikilizwa kesi za uhalifu dhidi ya binadamu zinazowakabili Rais Kenyatta, makamu wake, William Ruto na mtangazaji Joshua Arap Sang huko The Hague, Uholanzi kuhusiana na ghasia zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008.
Pamoja na Bunge hilo kupitisha hoja hiyo, ICC imesema kesi dhidi ya watu hao itaendelea kama kawaida. Kifungu cha 127 cha Mkataba wa Roma ambao ulianzisha Mahakama hiyo mwaka 2002 kinasema kuwa, itaichukua nchi kiasi cha mwaka mmoja kabla ya mchakato wa kuikubalia kujitoa kumalizika na kwamba hatua hiyo ya kujitoa haitaathiri kesi ambazo tayari zilikuwa katika Mahakama hiyo kabla ya uamuzi wa nchi husika wa kujitoa.
Ni vyema ieleweke kuwa, Kenya haitakuwa nchi ya kwanza kujitoa katika mkataba huo ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa (UN), Julai 17, 1988 kwani Marekani, Israel na Sudan ziliishafanya hivyo katika nyakati tofauti. Hivyo, Kenya pia haiko sahihi inaposema inataka kuwa mfano wa kuwa nchi ya kwanza Afrika kuchukua hatua hiyo.
Ni vigumu kuelewa sababu zinazoifanya Kenya kutaka kujitoa katika chombo hicho sasa, ikiwa kufanya hivyo hakutaondoa mashtaka yanayowakabili Rais Kenyatta na washtakiwa wenzake. Tunaweza kusema hatua hiyo haina masilahi mapana kwa Kenya na watu wa Kenya kutokana na ukweli kwamba kuna uwezekano mkubwa hatua hiyo ikaitenga Kenya na jumuiya ya kimataifa kiuchumi na kidiplomasia.
Yatakuwa makosa makubwa kufuata nyayo za Israel na Marekani kwa sababu nchi hizo kwa miongo mingi zimehusika na zinaendelea kuhusika na vita, hali inayoweza kutafsiriwa kama uhalifu wa kivita katika muktadha wa Mkataba wa Roma. Hata hivyo, kimsingi nchi hizo bado zinaendelea kuiunga mkono ICC kwa vitendo. Kenya na baadhi ya nchi za Umoja wa Afrika (AU), zinaendeleza dhana potofu kwamba ICC inaendekeza ubaguzi wa rangi na eti inafungua mashtaka ya uhalifu kwa kuwalenga viongozi wa Afrika pekee.
Tuliwahi kukemea upotoshaji wa kazi nzuri ya ICC unaofanywa makusudi na viongozi wa Afrika. Kama kuna viongozi wengi kutoka Afrika ambao wanakabiliwa na mashtaka ICC, ni kwa sababu Afrika ni kichaka cha viongozi madikteta wanaofanya uhalifu dhidi ya binadamu na siyo kitu kingine. Ndiyo maana serikali zinazofuata demokrasia ya kweli kama za Ghana, Senegal, Nigeria na Botswana hazikubaliani na uzushi huo wa nchi wanachama wa AU ambayo imekuwa kichaka cha viongozi madikteta.
Sisi tunasema ICC ienziwe kwa sababu ndiyo ngao ya pekee inayolinda haki na usalama wa wananchi, hasa barani Afrika. Tunaishauri Serikali ya Tanzania iendelee kuuenzi Mkataba huo wa Roma kama inavyoendelea kuenzi Mpango wa Nchi za Afrika wa Kujitathmini Zenyewe Katika Suala la Utawala Bora (APRM).
Chanzo www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment