Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Sunday, September 8, 2013

Hatuungi mkono vurugu za wabunge lakini kwa hili Ndugai amekosea

MOJA kati ya habari kubwa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini wiki hii, ni pamoja na ile ya kuzuka kwa ngumi bungeni. Kuzuka kwa sakata hilo, kulitokana na kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye alisimama kuomba nafasi ya kusema jambo. 

Lakini pia, kitendo cha Mbowe mwenyewe kukataa kutii amri ya Naibu Spika huyo aliyemtaka akae chini na hivyo kusababisha vurugu hizo.

Hatua hiyo ya Mbowe ilitanguliwa na tukio la wabunge kupiga kura ya kuamua au kutoamua kuuondoa muswada wa marekebisho ya pili ya sheria ya mabadiliko ya katiba, ambao baadhi, hasa wabunge wa upinzani, walikuwa wakidai kuwa ulikuwa na mapungufu makubwa.

Kwa upande wetu, tuseme tu wazi kwamba hatuungi mkono vitendo vyovyote vinavyoashiria vurugu, iwe kwa wabunge, viongozi wake, serikali na hata kwa mtu mmoja mmoja.

Kilichotokea bungeni wiki hii, kimelidhalilisha Bunge, kwa maana wabunge wenyewe lakini hasa kiti cha Spika ambacho sisi kwa upande wetu tumeona wazi kwamba kilionyesha udhaifu mkubwa katika kushughulikia jambo dogo ambalo pengine kama busara zingetumika, zisingelifikisha Bunge kwenye hatua kama tulizozishuhudia.

Si kwamba tunaunga mkono vurugu zilizofanywa na wabunge wa upinzani, hapa lazima tueleweke na tuseme wazi bila kumung’unya maneno kwamba kilichotokea bungeni ni ukosefu wa busara ndogo tu kutoka kwa Naibu Spika, Job Ndugai.

Jambo hili liko wazi, hasa kwa Tanzania ambayo mfumo wa uendeshaji wa Bunge lake ni kama ule wa mabunge ya Jumuiya ya Madola au mfumo wa uendeshaji wa mabunge ya vyama vingi, kwamba Mkuu wa shughuli za serikali bungeni, ambaye ni Waziri Mkuu, na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, wana hadhi sawa ndani ya Bunge.

Inaeleweka kwamba Waziri Mkuu akisimama ndani ya Bunge, hata kama kuna shughuli yoyote inaendelea, ni lazima kiti cha Spika kimpe nafasi ya kumsikiliza. Spika hana mamlaka yoyote ya kuamua kutomsikiliza Waziri Mkuu anaposimama kwa hoja yoyote. Vivyo hivyo, kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Hivyo basi kitendo cha Naibu Spika wa Bunge kumzuia Kiongozi wa upinzani asizungumze jambo alilotaka kusema na kumuamuru akae chini na kisha kuamuru atolewe nje, ni kitendo ambacho hakikupaswa kufanywa na kiti kama cha Spika na ndiyo maana tunasema kiti hicho kilikosa busara ndogo tu.

Tumejiuliza kama Waziri Mkuu angesimama, Ndugai angethubutu kumwambia kaa chini? Au aamuru atolewe nje?

Katika kutafakari kwetu, tunaamini kwamba kama Naibu Spika, angelimruhusu Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani kuzungumza, yaliyotokea bungeni yasingetokea.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, ingawa naye amekuwa akitajwa kuwa na upungufu katika utendaji wake, lakini si kwa kiwango cha Naibu wake.

Ushauri wetu ni kwamba wakati huu tukiwa na ndoto za kupata katiba mpya ambayo pamoja na mambo mengine itatizama udhaifu kama huu, kwa kuweka Spika na naibu wake ambao hawatokani na chama chochote cha siasa, lakini pia viongozi hao watambue kuwa Bunge haliongozwi kwa kanuni peke yake, bali pia kwa busara na hekima.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment