Writen by
sadataley
11:43 AM
-
0
Comments
Na Elias Msuya, Mwananchi
Ni kama amejifunga jiwe shingoni kwa kuahidi miezi mitatu ya kusafisha nyumba, tusubiri tuone
Baada ya John Tendwa kudumu katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa takribani miaka 13, sasa amestaafu na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi.
Jaji Mutungi amekula kiapo cha utii mbele ya Rais Jakaya Kikwete Ikulu ya Dar es Salaam juzi, Jumatatu. Yeye, ameapa kufanya kazi kwa uaminifu na kutunza siri zote za ofisi yake, isipokuwa kwa idhini ya rais tu.
Sherehe ya kuapishwa kwa Jaji Mutungi ilihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, viongozi wa vyama vya siasa na ndugu na jamaa wa Jaji Mutungi.
Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.
Kazi ya Msajili wa Vyama vya siasa
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, kifungu cha 7(1-3); kazi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ni kusajili vyama vyote vya siasa vinavyoanzishwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“(2) Bila kuathiri masharti ya kifungu cha (1), Chama cha Mapinduzi au CCM ambacho kabla ya sheria hii kilikuwa chama kimoja kilichotawala Jamhuri ya Muungano, kinapaswa, kilipaswa kujisajili upya katika ofisi ya Msajili na kupewa cheti cha usajili chini ya sheria hiyo.”
Jaji Mutungi ana lipi jipya?
Baada ya kuapishwa, Msajili mpya wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewataka waandishi wa habari na jamii kwa jumla impe miezi mitatu ya kujifunza kazi aliyopewa kabla ya kuanza kumwuliza maswali.
“Kwa leo sitakuwa na mengi ya kuzungumza na ninyi, nipeni kwanza nafasi… nipeni miezi mitatu halafu nitawaita, tena nataka kufanya kazi kwa karibu mno na waandishi wa habari,” anasema Jaji Mutungi.
Hata hivyo akizungumza baada ya kuombwa na waandishi wa habari, Jaji Mutungi alisema kuwa anao uzoefu wa ujaji kwa muda mrefu, hivyo atatenda haki kwa vyama vyote.
“Ugumu wa kazi ndiyo matarajio yangu makubwa kwa jamii… mimi nimekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu, hivyo nitakuwa tayari kutumika,” anasena na kuongeza:
“Ni kweli najua ipo changamoto ya kumtii rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM na kuvitendea haki vyama vingine. Mimi nimekuwa jaji katika nchi hii kwa muda mrefu, vinginevyo nisingeweza kufanya kazi. Demokrasia ina changamoto nyingi, niacheni mwone nitakavyofanya.”
Jaji Mutungi anaingia katika ofisi hiyo wakati ikiwa imejaa malalamiko mengi ya upendeleo kwa chama tawala, CCM.
Lawama hizo zilizidi hasa katika utawala wa mtangulizi wake, John Tendwa. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndiyo kilikuwa mstari wa mbele kulalamika.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa anasema chama chake kimekuwa kikipeleka malalamiko ya unyanyasaji kwa Msajili wa Vyama vya Siasa (Tendwa) lakini hayafanyiwi kazi.
“Tumelalamika mara nyingi, tumezungumza mara nyingi lakini hakuna linaloendelea. Kumbuka Msajili huyo huyo ananipigia simu ananiambia kuwa Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) asiende Arumeru Mashariki kulitokea tishio la vurugu. Maana yake ni kwamba chama kiache kazi yake kwa sababu kuna Watanzania wanatisia kuua, huyomsajili yuko huru?” anasema na kuongeza:
“Msajili huyohuyo ndiye aliyetuandikia tusitishe kwa siku 14 shughuli zetu za siasa kwa sababu sensa inaendelea. msajili huyo ni mwanasheria, anajua sensa haizuii kazi kuendelea. Sisi Chadema hatumuhesabu kuwa mlezi na ndiyo maana kamati kuu ya chama iliamua kuwa hatutashirikiana na msajili wa vyama vingi mpaka aondolewe.”
Tendwa apiga vijembe
Naye msajili mstaafu aliyemaliza muda wake hivi karibuni, John Tendwa amepiga vijembe bila kutaja majina ya anaowarushia vijembe hivyo.
“Mtu akikupiga madongo usimrudishie hata kidogo, atakuja kuona baadaye mwenyewe kwamba alikuonea,” anasema Tendwa na kuongeza:
“Katika jamii ukiona watu wanakupigia sana makofi, jiulize, kweli ninayofanya yanastahili makofi au wanakupaka mafuta kwa mgongo wa chupa? Ukiona watu wanalalamika sana, ujue hao wameshindwa.”
“Hata Yesu alipokuwa akifundisha alitumia mifano, mimi sijataja jina la mtu nimetoa tu mifano.”
Tendwa ameongeza kuwa anajivunia miaka 13 ya kazi yake hiyo ambapo ameacha vyama 21 vyenye usajili wa kudumu.
“Haya yote mnayoyaona ni mafanikio yangu, leo tuna vyama 21 vyenye usajili wa kudumu,” anasema.
Ilikotokea Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa
Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilianzishwa chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1993.
Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilipata kiongozi wake wa kwanza Julai mosi 1993 ambaye alikuwa ni Jaji George Liundi.
Jaji Liundi alianzisha ofisi hiyo wakati bado mfumo wa vyama vingi ukiwa mchanga na vyama vilikuwa bado vikijipanga.
Hata hivyo kulikuwa na upinzani mkali wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Zanzibar huku upande wa Bara, chama cha NCCR nacho kilionyesha makali yake.
Uchaguzi wa kwanza katika mfumo huo wa mwaka 1995 uligubikwa na utata, hasa upande wa Zanzibar baada ya CUF chini ya Seif Shariff ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kudai kuwa ameporwa ushindi na aliyekuwa rais wakati huo, Dk Salmin Amour.
Malalamiko hayo yalisababisha wawakilishi wa chama hicho kususia vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa karibu miaka mitano.
Kwa upande wa Bara, NCCR Mageuzi kikiwa chini ya Augustine Mrema ambaye sasa ni Mwenyekiti wa TLP na Mbunge wa Vunjo, kiliambulia ushindi wa asilimia 40.
Jaji Liundi pia alishuhudia purukushani zilizozuka ndani ya NCCR Mageuzi ambapo kambi za Mrema na katibu wake mkuu Mabere Marando zilipambana vilivyo.
Ugomvi huo uliishia kwa kukisambaratisha chama hicho kilichokuwa kikuu cha upinzani upande wa Bara, baada ya Mrema na kambi yake kuhamia TLP na kambi ya Marando kubakia.
Jaji Liundi alitumikia ofisi hiyo hadi mwaka 2000 alipomwachia John Tendwa. Tangu wakati huo upepo wa siasa umekuwa ukibadilika, kutoka nguvu ya NCCR Mageuzi mwaka 2000 kwenda CUF Bara na visiwani hadi mwaka 2005.
Mwaka 2010, Chadema kiliongeza nguvu yake maradufu baada ya kumsimamisha Dk Wilbrod Slaa kugombea urais. Tangu wakati huo chama hicho kimekuwa kikimtaja Tendwa kama mchawi wa mapambano yao.
Chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment