Writen by
sadataley
8:49 PM
-
0
Comments
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na mwenzao mmoja, wamekamatwa mjini Iringa. Tukio hilo lilitokea mjini hapa jana baada ya Mbowe na wenzake kudaiwa kuzidisha muda wa kuhutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika juzi katika Viwanja vya Mwembetogwa.Pamoja na kukamatwa, Mbowe na wenzake hao baadaye waliachiwa baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na mwingine aliyekuwa katika kundi hilo, kuwa ni Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Manispaa ya Iringa, Frank Nyalusi.
“Tuliwakamata na kuwahoji kwa masaa matano ili wajibu tuhuma za kuchelewa kumaliza mkutano wa hadhara uliokuwa na lengo la kukusanya maoni ya rasimu ya Katiba Mpya katika Manispaa ya Iringa.
“Walizidisha muda kwa zaidi ya dakika 25 kinyume cha sheria na kama watathibitika kutenda kosa, basi watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema kamanda huyo.
Alifafanua kuwa, Chadema waliomba kibali cha kufanya mikutano mitatu mkoani Iringa, ambapo ratiba yao ilielekeza kuwa wangefika wilayani Mufindi na kuanza mkutano saa 4:00 hadi saa sita mchana badala yake waliwasili saa 9:20 alasiri huku wakiwa wamechelewa.
Alisema walienda Ilula, wilayani Kilolo saa 10.45 jioni badala ya saa 6:00 hadi 8:00 mchana kama walivyoomba.
Kutokana na hali hiyo, alisema walichelewa kuanza mkutano wao wa Mwembetogwa ambapo waliwasili Iringa Mjini saa 11.30 jioni na kuanza mkutano ambao ulimalizika saa 12.25 kinyume cha kibali chao.
Alisema kitendo cha kufanya mikutano nje ya muda waliopangiwa ni utovu wa nidhamu na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia sheria na taratibu zilizowekwa.
Katika mkutano huo uliofanyika juzi, Mbowe kabla ya kuanza kuhutubia mamia ya wananchi, aliliomba radhi Jeshi la Polisi kwa kuchelewa kuanza na baada ya kumaliza kuhutubia, aliomba tena radhi.
Mikutano ya Chadema ambayo ina lengo la kukusanya maoni kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ambapo, Mbowe aliwataka wakazi wa Mkoa wa Iringa kukiunga chama hicho mkono, katika kuhakikisha wanaondoa baadhi ya vipengele vinavyowakandamiza.
Habari kutoka kwa Tumaini Msowoya
No comments
Post a Comment