Writen by
sadataley
9:19 AM
-
0
Comments
Kumbe vyama vidogo vinawajibika zaidi bungeni?

Mbunge wa TLP,Augustine Mrema
Asasi mbili mashuhuri nchini zilizofanya tathmini kuhusu utendaji wa wabunge, jana zilitoa ripoti inayoonyesha kwamba wabunge wa vyama vidogovidogo ambavyo vina viti vichache katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana wastani wa juu zaidi wa ushiriki ndani ya Bunge.
Asasi za Twaweza na Kituo cha Ustawi wa Kiuchumi (CEP), zinazoheshimika hapa nchini zimefanya tathmini ya utendaji na ushiriki wa wabunge kwa jumla kwa kila chama, kila mbunge na kwa aina ya ushiriki katika kipindi cha miaka miwili ya Bunge kuanzia 2010 hadi 2012.
Muhtasari wa tathmini hiyo unachambua data zilizopatikana katika Tovuti ya Bunge kuhusu ushiriki wa kila mbunge wakati wa vikao vya Bunge katika kipindi hicho. Ni tathmini inayofuta dhana kwamba wastani wa ushiriki mkubwa wa wabunge unatokana na vyama vikubwa, hasa CCM chenye wabunge 254 dhidi ya vyama vya upinzani vyenye jumla ya wabunge 90 tu.
Tathmini ya asasi hizo inaonyesha kwamba ushiriki wa wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi na wale wa kuteuliwa na Rais ulikuwa hafifu. Pia inaonyesha kwamba TLP ambacho kina mbunge mmoja na NCCR-MAGEUZI chenye wabunge watano ndivyo vilivyokuwa na wastani wa kiwango kikubwa zaidi cha ushiriki kwa mbunge. Tathmini hiyo iliangalia ushiriki bungeni wa aina tatu. Kwanza ni kuuliza maswali ya msingi. Pili ni maswali ya nyongeza. Tatu ni kuchangia katika mijadala ya hoja mbalimbali.
Wakati wastani wa uchangiaji wa Augustine Mrema wa TLP ulikuwa ni 87, NCCR-MAGEUZI wabunge wake watano walikuwa na wastani wa 74, huku John Cheyo wa UDP akiwa na wastani wa 37 tu. Hata hivyo, tathmini hiyo inaonyesha kwamba ukiondoa vyama vidovidogo vyenye chini ya asilimia tano ya uwakilishi bungeni, Chadema kimeonyesha kufanya vizuri zaidi kwa ushiriki wa wastani 57 kikifuatiwa na CUF chenye wastani wa 41, huku CCM ikiwa na wastani wa 39 tu.
Tafsiri ya takwimu hizo ni nini? Tafsiri ya moja kwa moja ya takwimu hizo ni kwamba wabunge wengi wa vyama vikubwa, hasa CCM hawahudhurii vikao vya Bunge au wanaripoti ili wasaini posho lakini baadaye wanatoroka. Wengine wanachapa usingizi au wanaamua tu kukaa kimya wakisubiri kupiga kura za kupitisha au kukataa miswada na hoja za Serikali kwa maagizo na matakwa ya vyama vyao. Haiingii akilini, kwa mfano kuona wastani wa ushiriki wa wabunge 254 wa CCM ukiwa 39 tu, huku mbunge mmoja tu wa TLP akiwa na wastani 87 wa ushiriki.
Hii bila shaka ni changamoto kubwa kwa vyama vyenye wabunge wengi bungeni. Somo tunalopata hapa kutokana na hali hiyo ni kwamba vyama vyenye wabunge wachache sio vya kubeza, kwani wabunge wake sio tu wanahudhuria karibu vikao vyote vya Bunge, bali pia wanashiriki katika mijadala yote na wanatoa hoja nzito na zenye mashiko. Mfano mzuri ni wabunge wa NCCR-MAGEUZI.
Sisi tunazipongeza asasi hizo kwa kutufungua macho kuhusu ushiriki wa wawakilishi wetu tuliowatuma bungeni. Ni kweli kwamba chama kikipata wabunge wengi kinapata ruzuku kubwa, lakini hilo sio jambo la msingi katika muktadha wa kuwatumikia wananchi. Jambo la msingi ni aina ya mbunge anayechaguliwa kwenda Bungeni.
No comments
Post a Comment