Writen by
sadataley
11:36 AM
-
0
Comments
SALAMU YA MWENYEKITI WA
CCT-IBADA YA MAZISHI YA HAYATI BABA ASKOFU DKT. THOMAS O. LAISER
(15 FEBRUARI 2013)
“Kwa maana kwangu mimi
kuishi ni kristo, na kufa ni faida” Wafilipi 1:21
Jumuiya ya Kikristo Tanzania ina masikitiko makubwa ya
kumpoteza kiongozi mahiri, mkweli, shujaa mwenye ujasiri na nabii wa Kanisa
aliyetoa mchango mkubwa sana katika maendeleo na Maisha ya Kanisa na Jamii.
CCT inapenda kutoa salamu ya pole kwa mama mjane Mary Laiser
na watoto wake; kwa Dayosisi ya Kaskazini Kati na pia kwa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania.
Kiongozi huyu amelitumikia Kanisa lake, CCT, Jukwaa la
Wakristo Tanzania na Kanisa zima la Ulimwengu katika nyadhifa na nyanja
mbalimbali kwa uwezo na uaminifu mkubwa.
Katika kumkumbuka kiongozi huyu na kuheshimu mchango wake ndani
ya CCT na taifa kwa ujumla, CCT inapenda kuweka bayana kwamba Hayati Ask. Dkt.
Laiser ametuachia pengo kubwa sana ambalo kuzibika kwake hakutakuwa rahisi hasa
ikizingatiwa kuwa sauti yake ya kinabii imekuwa ikihitajika sana katika vipindi
vingi na hasa wakati kama huu ambao umegubikwa na changamoto nyingi
zinazohatarisha amani, mshikamano, utulivu na umoja wa kitaifa.
Ili kumuenzi na kumheshimu Hayati Askofu Dkt. Thomas Laiser, CCT
inatamka bayana mambo yafuatayo:
1. Ziko dalili za wazi zinazoonyesha
kuwa wakati huu Kanisa katika Tanzania
limeingia kwenye kipindi cha mateso ya wazi ambayo yamejidhihirisha katika
matendo ya uchomaji wa makanisa, kutishia usalama wa watumishi wa Kanisa na wengine
hata kuuwawa. Mfano wa wazi ni wa kuuwawa Mchungaji wa Kanisa mojawapo huko Buselesele-Geita.
Kifo chake ni matokeo ya wazi ya uchochezi unaotolewa kiwaziwazi kama
alivyofanya mmoja wa mashehe wa huko Mwanza aliyesema wazi wazi kuwa ‘ukimuona
Kadinali ua, ukimwona Askofu ua, ukimwona Mchungaji au Padri ua; iwe ni kwa
wazi au kwa kificho. Tunashangaa kuona serikali haijamchukulia hatua kwa
uchochezi huo. kwa hiyo tunatafsiri kuwa kifo cha Mchungaji wa Buselesele kuwa
ni mwanzo tu wa vifo vya watumishi na wakristo wa Tanzania. Kwa hiyo tunaiomba
serikali ielewe kuwa kifo cha Mkristo mmoja ni tangazo la kifo kwa wakristo
wote.
2. CCT inaikumbusha Serikali kwa mara
nyingine kwamba nchi yetu inatawaliwa kwa kufuata misingi ya Katiba na Sheria
inayobainisha kwamba Serikali haifungamani na dini yoyote. Na hakuna Kiongozi
wa Serikali anayeweza kuisemea dini au Kiongozi wa dini anayeweza kuisemea
Serikali. Kwa maana hiyo basi viongozi wa Serikali wasiwe na tabia ya kuegemea
upande mmoja na kuulemea upande mwingine.
3. Maadamu sasa imekuwa dhahiri kuwa
kuchinja nyama itakayotumiwa na walaji wengi ni jambo la ibada linalogusa imani
ya dini husika, kwa msingi huo huo na kwa mantiki hiyo hiyo watu wengine wa
imani nyingine wasilazimishwe na kiongozi wa aina yoyote kushiriki jambo la
kiimani na kiibada lisilowahusu.
4. CCT inawatia moyo wakristo wasiopenda
kushiriki mambo ya imani na ibada zingine zisizowahusu kwamba wasishurutishwe
kushiriki imani na ibada hizo wasizohusika nazo kwa namna iwayo yoyote ile.
5. Aidha CCT kwa kuheshimu mchango wa
Hayati Askofu Dkt. Laiser inawasihi Wakristo waendelee kutoa ushirikiano na
vyombo vya dola na jamii vinavyotenda haki katika kudumisha amani, mshikamano,
utulivu na umoja wa kitaifa.
Mungu ailaze pema roho ya Hayati Askofu Dkt. Thomas O.
Laiser: BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA LIBARIKIWE.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
No comments
Post a Comment