Writen by
sadataley
2:59 PM
-
0
Comments
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mto Nile ni miongoni mwa mito
mikubwa iliyopo upande wa Mashariki ya Bara la Afrika na Duniani kote
ukiwa na urefu wa kilomita 6,695 ambapo beseni ya Nile hukusanya maji ya
eneo linalojumuisha 10% za eneo la Afrika yote.
Kwa muonekano wa juu Mto Nile
unaonekana kama pembetatu wakati upande wa chini wa eneo la Nile
(Kaskazini) na upande wa juu (Kusini) kuna mimea mbalimbali inayoota kwa
wingi pia katika kipindi cha mwisho wa mwaka eneo la mto Nile huwa
linakuwa na mwonekano mwekundu na kuwa na maua yanayojulikana kama lotus
flowers.
Japokuwa mimea hii haioti kwa
wingi wakati huu kama ilivyokuwa hapo awali, mimea inayoota kwa wingi
katika eneo la Mto Nile kwa upande wa chini ni yale yanayojulikana kama
Egyptian lotus na kwa upande wa juu hujawa na mimea inayoitwa Cyperus
papyrus.
Chemchemi za Nile ni mito yote
inayopeleka maji kwenda Ziwa Viktoria katika nchi za Tanzania, Burundi,
Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Kenya na kwa upande
mwingine wa Nile unaanzia Ethiopia ukiitwa Abbai au Nile ya Buluu
unatoka katika Ziwa Tana wakati chanzo cha mbali kabisa ni mto wa
Luvironza huko Burundi unaoingia katika mto wa Kagera na kufika Ziwa
Viktoria.
Mto huo ambao unaanzia Ziwa
Victoria nchini Tanzania, ni chanzo kikubwa cha maji kwa ajili ya
matumizi ya nyumbani, viwandani, kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha
umeme kwa wakazi wa nchi za bonde hilo.
Kutokana na nchi nyingi
kuzungukwa na mto Nile, suala la ushirikiano katika kusimamia na
kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto huo limepewa kipaumbele ili kuzuia
migogoro inayoweza kuzuka baina ya nchi ambazo wanatumia mto huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi
inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent
Ntabana anasema kuwa azma ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za
Bonde la Mto Nile limepewa kipaumbele na nchi zote zinazozungukwa na mto
huo, jambo hilo ndilo limesababisha kuanzishwa kwa Sekretarieti ya NBI
mwaka 1999 jijini Dar es Salaam.
“NBI ina jukumu la kusimamia
na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile kwa niaba ya nchi
wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo na Misri,” anasema Ntabana.
Kwa upande wa Mratibu wa Kanda
wa Kitengo cha Uratibu cha Bonde la Mto Nile (NELSAP-CU), Elicad
Nyabeeya anasema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi wanachama
kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri ambayo
yanapelekea kuinua uchumi wa nchi hizo pia kwa upande mwingine uwepo wa
ushirikiano huo umesaidia nchi wanachama kufahamu tamaduni za watu
tofauti tofauti.
Nyabeeya anakaririwa akisema
kuwa “Nchi ya Tanzania inafaidika kutokana na uwekezaji mkubwa
uliofanywa na NBI kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo
miradi ya ujenzi wa bwawa la Bisrawi na usanifu wa bwawa la Borenga,
mkoani Mara”.
Kwa mujibu wa Nyabeeya, nchi
hii itanufaika na miradi ya maji na nishati ya umeme, pamoja na miradi
mingine mingi ambayo NBI inaendelea kuitekeleza kama vile ujenzi wa
mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na umwagiliaji katika mabonde ya mito
Kagera na Ngono iliyopo mkoani Kagera.
Anaendelea kufafanua kuwa
mradi wa umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 za umeme ambazo
zitatumiwa na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo Tanzania
inatarajiwa kupata megawati 16.
Miradi mingine ni ya kuunganisha umeme kutoka Ethiopia, Kenya hadi Tanzania, mradi wa umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Aidha, NBI wanatarajia
kukamilisha upembuzi yakinifu wa kina wa miradi ya Mara na Ngono ifikapo
mwezi Aprili mwaka huu ambapo wananchi 20,000 pamoja na hekari 13,630
katika vijiji 21 vinatarajiwa kunufaika na mradi wa Ngono wakati Bonde
la Mara litanufaisha wanachi 10,000. Miradi hiyo itahusisha usambazaji
wa maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, mifugo na shughuli za
umwagiliaji.
Wakati huo, Bwawa la Borenga
litakuwa likisambaza maji katika Bonde la Mara kwa wakazi wa vijiji 13
kwa ajili ya umwagiliaji na 17 vitapata maji kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani na mifugo.
Madhumuni ya miradi hiyo ni
kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji ya uhakika, kuimarishwa kwa
soko na mahusiano na kukuza sekta binafsi, kilimo, usalama wa chakula na
kupunguza umaskini.
Kutokana na kuwepo kwa umuhimu wa
rasilimali za Bonde la mto huo, iliamuliwa kuwa Februari 22 ya kila
mwaka iwe ni siku rasmi ya kuadhimisha uanzishwaji wa muunganiko wa
matumizi ya pamoja ya rasilimali za mto huo baina ya nchi 10 wanachama .
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali
za Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Sylvester Matemu
amesema kuwa lengo la Siku ya Nile ni kukuza uelewa kwa watu wote kuhusu
umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote wanachama, masuala
yanayotekelezwa na faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya
rasilimali za Bonde la Mto huo.
“Maadhimisho ya siku ya Nile
kuadhimishwa katika nchi fulani ni tukio la kihistoria kwasababu ni
tukio ambalo halifanyiki katika nchi moja kila mwaka hivyo kwa vile nchi
wanachama tuko 10 basi linatokea mara moja kila baada miaka
10,”anasema Mhandisi Matemu.
Maadhimisho ya 11 ya Siku ya Nile
kwa mwaka huu yameadhimishwa nchini Tanzania kwa ushirikiano wa Wizara
ya Maji na Umwagiliaji pamoja na Sekretariati ya Nile Basin Initiative (NBI)
ambapo mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan na lilihudhuriwa na watu zaidi ya 600 wakiwemo Mawaziri wa
nchi wanachama kutoka kwenye nchi husika, mabalozi mbalimbali, wabunge,
watu kutoka taasisi na mashirika mbalimbali pamoja na wanafunzi wa
shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu.
Shughuli hizo zilianza kwa
maandamano yaliyoongozwa na Bendi ya Polisi kuanzia Viwanja vya Mnazi
Mmoja hadi Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambako
maonesho pamoja na ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo vilifanyika.
Chanzo:Fullshangwe blog
No comments
Post a Comment