KKKT- DMP USHARIKAA
WA KIJITONYAMA
SIKU YA
BWANA YA KUKUMBUKA MATENGENEZO YA KANISA (Reformation)
USHUHUDA
WETU- TUNATENGENEZA MAMBO
YALIYOHARIBIKA
ZABURI 25:14-22, 1KOR 3:16-17, YOHANA 2:15-17
29.10.2023
Leo tunatafakari juu ya matengenezo
ya Kanisa ambayo ndio ushuhuda wetu. Ushuhuda ni neno la kuthibitisha na
kuelezea mambo yalivyokuwa au kutokea, ni
uthibitisho/ushahidi.
Mungu alipoumba dunia na kuifanya
kuwa kanisa lake halikuwa na haja ya matenegenezo kwa sababu
aliona kila kitu ni chema (Mw 1:31) Ila baada ya anguko ndipo umuhi wa
matengenezo ulipoanza kuonekana.
Matengeno ya Kanisa yalianza mara
moja baada ya anguko la mwanadamu, mwanadamu alianza kuona udhaifu na Mugu
akaona mtu wake anahitaji matengenezo ili aweze kuwa mwema tena ndipo Mungu
aliamua kuanza matengenezo kwa kuwatengenezea Mavazi ya ngozi wanadamu wale wa
kwanza kuficha udhaifu. (Mwanzo 3:21)
Tunamuona pia Yoshua alipoona Kanisa la Mungu linataka kujichanganya na miungu mingine aliamua kusimama
na kuonyesha msimamo kuwa Kanisa lenye michanagnyiko linahitaji kutengenezwa na
liwe na msimamo mmoja ndipo aliposema mimi na nyumba yangu tutamtumikia Mungu kama ninyi
mnataka kuendelea kuabudu miungu. (Yoshua 24:15)
Katika Agano Jipya kwanza tunamuona
Yesu mwenyewe katika somo tulilolisoma alipofika Yerusalemu
na kukuta hekaluni zinafanyika biashara na sasa kugeuzwa kuwa soko
aliamua kufanya matengenezo yake kwa kuondoa uchafu wote na wafanya
biashara wote kule hekaluni. (Yn 2:13-17)
Tunamuona Mtume
Paulo nae anaweka mkazo zaidi kwa kuwataka Wakoritho
kujitambua zaidi kwamba wao ni hekalu la
Roho Mtakatifu. Kutokukubaliana na mambo ya hovyo hovyo yafanyike na wao kukaa
kimya. hata sasa wengi tumekaa kimya na tunashindwa kukemea na kuingia na kufanya matengenezo huku tukishuhudia utapeli na ongezeko la waalimu wa uongo linazidi ndani ya Kanisa ambalo Mungu amelinunua kwa bei ya thamani.
Matengenezo ya Kanisa yaliendelea
baadae na hata kuzaliwa kwa Kanisa la Kilutheri
Duniani, sasa katika somo hili nataka ujiulize kwa nini
wewe ni Mlutheri? na Mlutheri ni nani?
Yawezekana usiwe na majibu ya haraka
ila nitakapofikia mwisho wa somo hili utapata majibu.
Kanisa letu la Kilutheri kila
Jumapili ya kila mwaka mwishoni mwa mwezi wa kumi karibu na tarehe 31
huadhimisha sikukuu ya matengenezo ya kanisa yaliyofanyika tarehe 31/10/1517.
Ilipofika mwakani (2017) Kanisa la kilutheri
Duniani lilifikisha miaka miatano(500) ya matengenezo yake,
Lazima tujihoji je bado tupo kwenye msingi wa neno la Mungu au tayari
tumeshatoka? Tufanye nini ili kuendeleza kazi njema ya Kuutangaza ufalme wa
Mungu hapa duniani? Matengenezo haya lazima yawe ushuhuda wetu kweli katika
matendo yetu na sio kinadharia tu.
USHUHUDA WETU
Kama nilivyoeleza maana ya
Ushuhuda wetu mimi nina ujasiri wa kusema kuwa nimekuwa Mlutheri kwa sababu
nilizaliwa katika imani hiyo nikiendelea kujiboresha kumjua Mungu zaidi.
Jina mlutheri limetokana na chimbuko
toka jina la Dkt. Martin Luther, baba wa matenegenezo ya kanisa aliyekuwa na
lengo la kurekebisha na kutengeneza baadhi ya mafundisho na taratibu zilizokuwa
zikifanywa na kanisa la wakati ule kanisa la Kirumi(RC) ambazo zilikuwa
hazijengwi kweneye msingi wa Neno la Mungu ili kurejea katika msingi wa
Kibiblia.
Dkt. Martin Luther alizaliwa na
kukulia nchini Ujerumani na alisoma masomo ya falsafa na sheria akiwa kijana
mdogo, lakini baadae aliamua kujiunga na masomo ya Theolojia ambapo mwaka 1507
alibarikiwa kuwa padre wa katoliki na baadae alifundisha chuo cha
theolojia Wittenberg. Wakati akifundisha chuoni Luher alichukizwa na
mafundisho na matendo yaliyokuwa yakifanywa na Kanisa katoliki kama vile
mamlaka ya papa, vyeti vya msamaha, wakristo kuzuiwa kusoma biblia nk, ndipo
tar 31/10/1517 aliandika maoni (sentensi) 95 kwenye mlango wa Kanisa la Wittenberg ambazo zilizungumzia juu
ya ukosefu wa elimu ya Kibiblia, matendo mabaya na kutokuwajibika miongoni mwa
viongozi wa Kanisa, yeye alikuwa na lengo la kuwarejesha kwenye maandiko Matakatifu.
Dr martin Luther alisimamia ukweli wa
neno la Mungu katika kupambana na mafundisho potofu yaliyofanya wokovu ufikie
hatua ya kununuliwa kwa hela kupitia vyeti vya msamaha pamoja na mapungufu
mengine. Tunaweza kusema kuwa Luther alishuhudia ukweli wa injili kiasi cha
kuwa tayari kufa kwa ajili ya ukweli pale aliposema “Hapa nasimamia
ukweli wa neno la Mungu, sitabadili msimamo, nisaidie Mungu wangu” “Here I Stand, Lord Help Me”
Dkt. Martin Luther hakuwa na lengo
wala nia ya kuanzisha dhehebu jipya, bali alitaka tu kusahihisha kile
alichokiona kama ukiukwaji wa wazi wa mafundisho ya Biblia ila alitakiwa kukana
maandishi yake ila alisema asipothibitishiwa kutoka biblia kuwa amekosea hayupo
tayari kuyakanusha ndipo alipohesabiwa kuwa mzushi na kuhukumiwa Kunyongwa ila
alifanikiwa kutoroka na kujificha.
Ndipo mwaka 1597 watheolojia waliokaa
katika mji wa Wittenberg huko ujerumani walitafsiri jina ulutheri
kumaanisha ‘Kanisa la kweli’ ambalo limejengwa kweneye msingi wa neno la Mungu
ila Martin Luther alipendelea neno Kiinjili zaidi.
Hivyo
tunaitwa Walutheri kwa sababu tunafuata misingi na mafundisho ya Dr. Martin
Luther na aliweka mkazo katika mambo haya: -
- Mafundisho
rasmi ya Kilutheri ya wakati wote na mahali pote
huonyesha sisi sote
wenye dhambi na tunapokewa jinsi
tulivyo kwa neema ya Mungu lakini hatuaswi kubaki jinsi tulivyopokelewa.(Rumi
6:1-4) na tujue kuwa ya kale yamepita tutazame mapya (1Kor 5:17) na tukazane
kuzaa matunda(Mt 7:19) na huku tukiwajali wengine (Mt 25:36-46).
- Leo
hii Mlutheri anafahamika kuwa ni muumini wa dini ya Kikristo ambaye
anaabudu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ambalo ni ushirika wa watakatifu ambao injili
inatangazwa kwa usafi na sakramenti zinatolewa kwa usahihi wake. Kama Luther
alivyotafsiri maana ya Kanisa kuwa ni pale ambapo injili inahubiriwa na
kupokelewa tena na Sakrament ya Ubatizo
na Ushirika wa Meza ya Bwana vinatolewa kwa usahihi wake.
- Mlutheri
anamwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake na
kubatizwa katika Utatu Mtakatifu,
ambapo anasafishwa dhambi zake na kupokelewa katika kundi la waaminio na
kufanyika mwana wa Mungu kwa njia ya imani tu. (SOLAR FIDES)- Roman 1:17.
- Mlutheri
anaamini juu ya mafundisho, mafunuo, mapenzi na ahadi za Mungu
kupitia maandiko matakatifu yaani
Biblia, kuwa ndio msingi wa maisha yake. (SOLAR SCRIPTURA).
- Mlutheri
anakubali na kuamini ya kuwa wokovu wa mwanadamu
unapatikana
kwa Neema ya Mungu
tu. (SOLAR GRATIA).
- Mlutheri
anakubali na kuamini ya kuwa katekisimo ndogo ya Dkt Martin Luther,
ukiri wa Nikea, Mitume, Athanasio na
ungamo la Augusburg lisilobadiika ndio maelezo sahihi tena ya wazi ya neno la
Mungu
KKKT imejali maisha wa kiroho ya
waumini wake kwa kuzingatia Biblia na kuna vitabu vingine kama kitabu
cha nyimbo TUMWABUDU MUNGU WETU pamoja na kalenda ya mwaka inayomwongoza kila
mlutheri popote alipo kwa neno la Mungu kila siku asubuhi na jioni.
Nyakati hizi kumetokea mafundisho
mengi sana ambayo yanawachanganya washarika wetu. Ni lazima sisi
tufuate na kuenzi utaratibu wa ibada yetu ili watu waweze kutambua kuwa sisi
walutheri wenye umoja na tumebobea katika mafundisho sahihi ya neno la Mungu na
sakramenti zake zinatolewa kwa usafi wote
Kwa msingi wa katiba ya KKKT
tunapaswa kuuenzi, kuulinda na kuimarisha umoja wetu, twapaswa sisi kushuhudia
kila kona juu ya neema ya Mungu kwetu. Waasisi wa KKKT
waliweka wazi msingi wa Imani utakaofuatwa ambao ni
Kanisa lililojengwa juu ya msingi mmoja,
Yesu Kristo, hukiri kwamba Neno la Mungu lililoandikwa katika Agano la Kale na
Agano jipya ndio msingi pekee wa uhakika wa Imani na maisha ya kanisa.
Katika umoja wa Kanisa moja duniani, huungama ungamo la Mitume, Nikea, na la
Athanasio; hukubali pia maungamo ya Kanisa la Kilutheri hasa ungamo la Augusburg
lisilobadilishwa na katekisimo ndogo ya Martin Luther kuwa maelezo au
mafafanuzi sahihi ya neno la Mungu. Sharika zote, na wachungaji, sinodi na
dayosisi za kanisa hili zitakubali na kufuata nsingi huu wa imani.
HITIMISHO
Tunapoona habari hizi za matengenezo
ya kanisa na historia nzuri za watu waliotetea imani yao hata kwa
mateso yatatuhimiza sisi wa leo kuendelea kuona kuwa kanisa la Mungu linapaswa
kujifunza kwa usahihi ukweli wa neno la Mungu pasipo kuyubishwa.
Tunapoona neno la Mungu linayumbishwa
tusikubali hali hiyo tunapaswa kukemea kwa ukali kama alivyofanya
katika hekalu ya Yerusalemu na tunapaswa kupatwa na wivu tunapoona kweli ya
neno la Mungu inapindishwa.
Matengenezo ya Kanisa ni jambo
endelevu ili kuendelea kupokea neema ya Mungu katika ukombozi kwenye maisha
yetu.
Tunapewa pia
wito wa kujenga umoja wetu katika familia zetu, umoja wa
kifamilia, umoja wa jumuiya na sala, umoja wamitaa ya Sharika, umoja wa
sharika, umoja wa jimbo, Dayosisi na Kanisa zima.
Wapendwa washarika kwa kupitia siku
hii ya matengenezo ya kanisa, tunaletewa wito kujifanyia tathimini katika Imani zetu, mienendo na maisha yetu kwa
ujumla. Je bado tupo katika msatari wa kumfuata Yesu au la? Lazima tujihoji je
bado tupo kwenye msingi wa neno la Mungu au tayari tumeshatoka? Tufanye nini
ili kuendeleza kazi njema ya Kuutangaza ufalme wa Mungu hapa duniani?
Matengenezo haya lazima yawe ushuhuda wetu kweli katika matendo yetu na sio
kinadharia tu.
Mungu na
atusaidie sote, amen.
No comments
Post a Comment