Writen by
sadataley
9:01 PM
-
0
Comments
Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi
imeihakikishia dunia kwamba uchaguzi mkuu ujao, utakuwa huru na wa haki.
Kabudi
ameyasema hayo kwenye hafla ya kukaribisha mwaka mpya ambapo amekariri
ahadi ya Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo aliyoitoa akizihakikishia
jumuiya za kimataifa kuhusiana na suala hilo. Akizungumza na mabalozi
na wawakilishi wa taasisi za kimataifa jijini Dar es Salaam Kabudi
amesema: “Mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa sita tangu
kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa na uchaguzi huo utakuwa wa uwazi,
huru na wa haki.” Ameongeza kwamba, Tanzania itawaalika waangalizi wa
uchaguzi watakaotaka kushuhudia namna Watanzania wanavyotekeleza moja ya
haki zao za msingi katika suala la kidemokrasia kwa kuchagua viongozi
wao.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Tanzania
ametoa kauli hiyo katika hali ambayo, kilio kikubwa cha vyama vya siasa
ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi, vikisema kuwa mfumo wa sasa wa
tume iliopo unawapa mamlaka wakurugenzi kusimamia uchaguzi wakati ni
wateule wa Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala cha CCM. Aidha
akihutubia kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa
Mataifa mjini Geneva, Uswisi Waziri Kabudi pia alisema serikali ya
Tanzania inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote za binadamu
zikiwemo za kisiasa na kwamba sheria zilizotungwa na bunge la nchi hiyo
zina lengo jema la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Taifa lenye amani,
umoja na utulivu. Alizidi kufafanua kuwa, madai yanayotolewa dhidi ya
Tanzania kuwa inakiuka haki za binadamu ni propaganda zinatokana na
hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma,
dawa za kulevya, uzembe katika ofisi za umma pamoja na hatua
zinazochukuliwa kulinda rasilimali za Taifa.
Parstoday swahili
No comments
Post a Comment