Writen by
sadataley
5:00 PM
-
0
Comments
Rais
wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia ujumbe maalumu Rais wa Tanzania,
Dkt. John Magufuli unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na
matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa jimbo la Starehe,
Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar.
Ujumbe
huo wa maandishi umewasilishwa leo (Jumanne, Julai 02, 2019) na Balozi
wa Kenya nchini, Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni
jijini Dar es Salaam.
Akipokea
taarifa hiyo Waziri Mkuu amesema Watanzania wamefurahishwa na hatua
mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo
zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya
Kenya wala wananchi wake bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge
huyo.
Amesema
siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au
biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki na pale yalipotokea
matatizo au kutokukubaliana serikali husika zilikaa mezani na kumaliza
tofauti hizo.
"Uhusiano
kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kidugu kwani kuna
baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na
Wakurya na Wajaluo hivyo ushirkiano katika masuala ya mbalimbali
yakiwemo ya kabiashara na ya kijamii haukwepeki."
Hivyo,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga
chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi kwani kauli hizo
zisipodhibitiwa mapema zinaweza kusabisha hofu na kutokuelewana miongoni
mwao.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa
amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za
Afrika ya Mashariki na duniani kwa ujumla ambao wapo nchini wakifanya
shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Mambo
yetu yote katika nchi za Afrika ya Mashariki hasa ya biashara na ya
kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo tutalinda na kudumisha
amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa kushirikiana”,
amesisitiza Mheshimiwa Majaliwa.
Waziri
Mkuu ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania kamwe ahaitaruhusu wala
kufumbia macho kauli au vitendo vyovyote vyenye viashiria vya
uchochezi dhidi ya nchi jirani ili na kulinda na kuunga mkono juhudi
mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na
viongozi wakuu wa Mataifa ya Afrika.
Kwa
upande wake Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake
aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na
wayachukulie matamshi ya Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua
kuwa ni msimamo wake binafsi na siyo msimamo wa Wakenya na Serikali
yao.
Balozi
Njagua mesema Msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea
na kuwakubali ndugu zao wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.
Mwanzoni
mwa wiki iliyopita Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya Njagua
alitoa matamshi ya kichochezi akiwataka raia wa kigeni kutoka Mataifa
mbalimbali wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Kenya wakiwemo
Watanzania waondoke ndani ya muda wa saa 24.
CCM BLOG
No comments
Post a Comment