Writen by
sadataley
8:13 AM
-
0
Comments
Utawala wa familia ya Castro nchini Cuba umehitimishwa rasmi. Rais Raul Castro leo amekabidhi rasmi uongozi wa nchi hiyo kwa aliyekuwa makamu wake wa kwanza, Miguel Diaz Canel.
Utawala wa Castro umeunga mkono makundi mengi ya Kiafrika - hatua iliyochangia kuidhinisha msingi wa kusambaa kwa 'mapinduzi' ya kikomyunisti katika vita vya kupigania uhuru wa mataifa.
Tanganyika kulikuwa na vuguvugu kubwa la kudai uhuru, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akiungwa mkono na Fidel Castro, katika harakati za kudai uhuru.
Fidel Castro aliunga mkono hotuba ya Nyerere kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu kudai uhuru wa Tanganyika. Hata baada ya kupatikana uhuru, serikali ya Cuba ilichangia sana katika kutoa ufadhili kwa masuala ya elimu na afya hata sasa.
Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha. Mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Nyerere.
Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa hata baada ya ukomo wa Castro madarakani, mahusiano yaliyokuwepo yataendelea kuwepo pengine kuimarika zaidi.
''Bado kuna jambo linawaunganisha wa Cuba na mataifa hasa nchi za Afrika na nchi zilizo masikini, kupambana na hali ya kutokuwa na usawa kwenye biashara na uchumi wa kimataifa, Cuba bado haiko tayari kuona ubeberu wa nchi za magharibi ukiwa na nguvu juu ya mataifa mengine yaliyo masikini''. Ameeleza mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumu Bravious Kahyoza.
Ushawishi wa utawala wa Castro kusini mwa Afrika
Uhusiano wake umekuwa wa karibu na mataifa ya kusini mwa Afrika hususan Afrika kusini katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na umeheshimiwa kwa kiasi kikubwa.
Siasa za Fidel Castro, zinakumbukwa kwa dhati Africa na Amerika kusini ambapo ushawishi wake uliwatia moyo wengi na ulikuwa na jukumu kubwa katika kuielekeza historia ya eneo hilo la kusini mwa Afrika.
Wanajeshi wengi wa Cuba walipoteza maisha yao mbali na nchi yao katika nchi kama vile Angola, wakipigana vita vya ukombozi wa Afrika.
Ilisaidia pia wapigania uhuru Msumbiji, mbali na kufadhili ujenzi wa miradi mingi ya kuwafaa wananchi mataifa mbalimbali barani Afrika.
Baadhi wanaamini kwamba wakati watu muhimu wa karne ya 20 wanapokumbukwa, Fidel Castro ni mmoja wa wanaofaa kukumbukwa.
Wakati wa kutolewa kwa usaidizi wa kimataifa katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika mataifa ya magharibi mwa Afrika, Fidel Castro, aliwatuma takriban madaktari 300 wa ziada na wauguzi katika mataifa yaliyoathiriwa.
BBC
No comments
Post a Comment