Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amejipalia makaa.
Onyo lake dhidi ya kuchanganya siasa na muziki, limewasha moto na sasa anashambuliwa nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na wasanii ambao wanasema ni jambo lisilowezekana kutofautisha mawili hayo.
Dk Mwakyembe, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuchukua nafasi ya Nape Nnauye aliwataka wasanii kuachana na nyimbo zinazoishambulia Serikali au viongozi na kuwataka wachague ama kuwa wasanii au wanasiasa.
Alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule, ambaye pia ni mwanamuziki wa rap akijulikana kwa jina la Profesa J, kuwa wasanii wanaoiimba nyimbo za siasa kuihoji Serikali wamekuwa wakinyanyaswa. Dk Mwakyembe alisema wakati akijibu swali hilo kuwa wasanii waelekeze tungo zao kwenye burudani si siasa. Juzi, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, ambaye kisanii anajulikana kama Sugu, alisema imefika wakati kwa Dk Mwakyembe kujiwekea utaratibu wa kusoma na kufanya tafiti za kina kabla ya kutoa kauli ambazo hazitekelezeki.
Alisema kumpangia mwanamuziki atunge au aimbe nini, ni jambo lisilowezekana kwa kuwa tungo nyingi ni zao la maisha halisi ya jamii ambayo mwanamuziki husika anatokea.
“Sitashangaa kusikia kauli hiyo imetenguliwa. Hili ni jambo la ajabu ndiyo sababu limetushangaza wengi. Muziki ndiyo silaha ya kwanza ya ukombozi na haiwezekani kumpangia mwanamuziki atunge au aimbe kuhusu nini,” alisema Sugu ambaye aliibuka kwa kuimba nyimbo za rap zenye ujumbe wa siasa.
“Inawezekana vipi tu juzi aseme kuwa Rais ameruhusu wimbo wa Nay (wa Mitego) upigwe redioni na kusisitiza kuwa yupo huru atunge nyimbo nyingine, halafu leo anakuja kusema kuwa mwanamuziki asiimbe nyimbo za siasa? Ndiyo sababu nina imani kauli hii nayo itakuja kufutwa,” alisema Mbilinyi.
Hoja hiyo haikuwa tofauti sana na iliyotolewa na mwanamuziki kutoka kundi la Weusi, Nikki wa Pili aliyesema kuwa sanaa ni mali ya msanii na mara zote anaimba kutokana na uzoefu wake wa kile kinachoendelea kwenye jamii.
Alisema licha ya kuwapo kwa mgongano wa muda mrefu kati ya Serikali na sanaa, ni vigumu kutenganisha siasa na sanaa kwa kuwa vimekuwa vikishirikishana.
“Sanaa imekuwa ikitumika kufanya harakati za ukombozi na siasa. Hakuna namna ambavyo unaweza kuzuia sanaa isiingie kwenye siasa kwa kuwa ina mchango mkubwa upande huo. Naweza kusema sanaa na siasa ni mapacha wa miaka mingi,” alisema Nikki.
Kauli kama hiyo ilitolewa na Nay wa Mitego, ambaye aliwahi kukamatwa kwa wimbo wake wa “Wapo”, aliyesema muziki na siasa ni maisha ya mwanadamu.
“Nadhani waziri mwenyewe atakuwa na majibu ya kina kuhusu alichokisema. Huenda ana nia njema ya kutuepusha vijana wake kwenye hatari kwa mujibu wa hali anavyoiona. Ila binafsi naamini naimba muziki unaogusa maisha halisi ya jamii niliyopo,” alisema.
Muigizaji wa filamu Shamsa Ford alisema kauli hiyo ya waziri inalenga kuwanyima haki wasanii kushiriki kwenye siasa ilhali nao ni sehemu ya jamii.
“Msanii naye ana haki ya kupiga kelele kwa masilahi ya Taifa lake. Anapoona jambo haliendi sawa ni jukumu lake kupaza sauti, kwa nini tuzuiwe. Kama hufanyi uchochezi sioni sababu ya kuwekewa mipaka,” alisema Shamsa.
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini (Taff), Simon Mwakifwamba alisema ipo haja ya sanaa kuangaliwa kwa mapana yake kwa kuwa ina nafasi ya kujenga au kubomoa jamii.
No comments
Post a Comment