Writen by
sadataley
11:48 AM
-
0
Comments
Fursa ya aina yake, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Rais John Magufuli, ni ile ya kufundisha Kiswahili katika taasisi za kielimu zikiwamo shule na vyuo vikuu nchini Afrika Kusini.
Akielezea jambo hilo, Rais Magufuli alisema wakati wowote kuanzia sasa, Tanzania itapeleka walimu hao wa lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kufundisha somo hilo.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana Ikulu mbele ya Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, ambaye alitua nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili baada ya kupata mwaliko wa mwenyeji wake (Magufuli).
“Tutapeleka walimu kwao (Afrika Kusini) wakati wowote kufundisha Kiswahili vyuo vikuu na shule zao na Rais Zuma amesema yuko tayari kwenye hili,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Tumekubaliana taasisi zetu za utafiti hususani zenye kushughulikia masuala ya sayansi na teknonojia zishirikiane na vyuo vyetu vitakuwa na utaratibu wa kutembelea na kufanya ziara za mafunzo ili kubadilishana uzoefu na utaalamu.”
Awali, marais hao, kwa pamoja walizindua rasmi Tume ya Pamoja ya Marais (BNC) na kufanya kikao cha kwanza tangu ianzishwe mwaka 2011 na kupokea makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha tume hiyo, ngazi ya mawaziri.
Aidha, marais hao walishuhudia utilianaji saini wa hati tatu za ushirikiano kati ya nchi hizo ambazo ni muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa tume ya pamoja ya marais, makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya baioanuwai na uhifadhi na makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.
Katika mkutano huo, mbali na kuzungumzia fursa za ajira nchini Afrika Kusini, Rais Magufuli pia aliyataja maeneo mengine waliyokubaliana, hasa kushirikiana katika biashara na uwekezaji.
“Kwa mujibu wa takwimu, biashara kati yetu kwa mwaka jana ilikuwa ni Sh. trilioni 2.4 na uwekezaji Afrika Kusini katika sekta mbalimbali hapa nchini ni dola za Marekani milioni 803.15… na ajira zilizotolewa ni 29,916,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa, wamekubaliana kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili na kusaidia Tanzania kukuza sekta ya viwanda kwa sababu ni eneo muhimu katika maendeleo ya nchi.
Aidha, Rais Magufuli alisema amemweleza Rais Zuma kuhusu azima ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda na kuwakaribisha nchini wafanyabiashara wa nchi hiyo kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, uvuvi, misitu na madini.
MIUNDOMBINU, NISHATI
Kuhusu miundombinu na nishati, Rais Magufuli alisema wamekubaliana kushirikiana na Afrika Kusini kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Pia Rais Magufuli alimweleza Rais Zuma kuhusu miradi ya miundombinu ya usafiri na umeme pamoja na ujenzi wa reli ya kati wa kiwango cha Standard Gauge wa Kilomita 1,200, pamoja na miradi ya kuzalisha umeme wa makaa ya mawe Kiwira na Mchuchuma na kuwakaribisha wawekezaji wa nchini humo kuja kuwekeza Tanzania.
Akizungumzia mikopo, Rais Magufuli alimwomba Rais Zuma kuisaidia Tanzania kupata mkopo wa masharti nafuu kupitia benki ya kundi la nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi ambazo ni Brazili, India, Urusi, China na Afrika Kusini (Brics).
Alisema mkopo huo utasaidia kwenye ujenzi wa Reli ya Kati ambayo kilomita 300 zinajengwa kwa fedha za ndani.
“Nimemwomba hili kwa sababu ni ukweli usiofichika Tanzania tumefanya mengi ya ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, tumejitolea mambo mengi na kuna maeneo yalishindwa kuendelea kwa sababu tuliyaacha… ndiyo maana tunaomba kupitia tuliowasaidia nao watusaidie angalau kidogo.
“Kwa sababu nchi yako ni mwanachama mzuri wa Brics na tunajua unaipenda Tanzania na sisi tunaipenda Afrika Kusini, tunaamini mtatupa mkopo,” alisema.
Aidha, Magufuli alimweleza Rais Zuma kuwa reli hiyo ya kati itajengwa hadi Morogoro ingawa haijafika eneo la Kongwa ambako wapiganaji wa Afrika Kusini walikuwa wanakaa wakati wa harakati za ukombozi.
“Tunapenda siku moja wananchi wa Afrika Kusini waje kwa treni hadi Dodoma ambako ndio makao makuu ya nchi, wakipita maeneo walikokaa wapiganaji wao kuikomboa Afrika Kusini,” alisema.
ZUMA AMPONGEZA JPM
Rais Zuma alimpongeza Rais Magufuli kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati na kuahidi kumuunga mkono kwa sababu anatambua kuwa italeta manufaa kwa Tanzania na nchi nyingine za maziwa makuu.
Pia alilikubali ombi la Rais Magufuli la kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika ya Kusini kushirikiana na Tanzania kufanikisha mradi huo.
Aidha, Zuma alimwahidi Magufuli kuwa makubaliano yote ya Tume ya Pamoja ya Marais yaliyofikiwa atahakikisha yanatiliwa mkazo na kutekelezwa kwa muda uliopangwa.
Alisema Afrika Kusini inatambua na kuheshimu mchango mkubwa wa Tanzania kwa ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika ikiwamo Afrika Kusini, ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alishirikiana na waasisi wa Taifa, walioongozwa na Hayati Nelson Mandela kupigania ukombozi na uhuru.
Alisema anafurahi kuona Tanzania bado inatoa mchango mkubwa wa kupigania amani katika bara la Afrika.
“Nikuhakikishie kuwa nchi yangu itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ndugu na marafiki wa Tanzania katika kujenga uchumi kwa manufaa ya wananchi,” alisema.
Viongozi hao jana walishiriki mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini unaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na jioni Rais Zuma alihudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa Ikulu na Rais Magufuli kabla ya kurejea Afrika Kusi
No comments
Post a Comment