Writen by
sadataley
3:24 PM
-
0
Comments
NCHI za Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kushirikiana katika maeneo 11 yakiwamo ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, sayansi, teknolojia, uchumi wa viwanda, ulinzi na usalama, utalii na madini ambayo yataisaidia Tanzania kukuza uchumi wake.
Meneo hayo yalibainishwa kupitia mapendekezo yaliyoafikiwa na mawaziri wa nchi hizo mbili wa Mambo ya Nje na kuridhiwa rasmi jana katika mazungumzo ya ndani ya Rais John Magufuli na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye alikuwa na ziara ya kikazi nchini ya siku mbili kuanzia juzi. Aidha, katika kikao hicho cha ndani, Dk Magufuli alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Zuma ambaye pia ni mwanachama wa jumuiya ya nchi tano zenye nguvu kiuchumi duniani (Brics), aiombee mkopo nafuu Tanzania kwa ajili ya kumalizia mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard Gauge.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo hayo Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Magufuli aliyaelezea mapendekezo hayo ya mawaziri kuwa yatasaidia nchi hizo hususani Tanzania katika kukuza uchumi wake. Rais Magufuli alisema mawaziri hao walipendekeza nchi hizo ziendelee kushirikiana katika eneo la biashara na uwekezaji ambapo kwa mwaka jana pekee, biashara baina ya nchi hizo ilifikia thamani ya Sh tilioni 2.4 huku uwekezaji wa Afrika Kusini nchini Tanzania ukifikia Dola za Marekani milioni 800.15 na kutengeneza ajira 20,616.
“Tumekubaliana pia katika eneo hili nchi zetu ziondoe vikwazo vyote ambavyo vinakwamisha biashara kati yetu,” alieleza Magufuli. Alisema katika eneo la uchumi wa viwanda, nchi hizo zimekubaliana kupitia mkakati wa Maendeleo ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuhamasisha uwekezaji nchini katika maeneo mbalimbali ikiwemo mifugo, madini na kilimo ili kuinua sekta ya viwanda. Alisema katika mazungumzo yao ya ndani, alimuelezea Rais Zuma kuhusu azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuijenga Tanzania na kuwa nchi ya viwanda jambo lililoungwa mkono na rais huyo.
Akizungumzia eneo la ujenzi wa miundombinu, usafiri na nishati, alisema nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali na Tanzania imewasilisha ombi la wawekezaji kutoka Afrika Kusini kujitokeza kwa wingi na kuwekeza katika miradi iliyopo ikiwemo mradi wa treni ya kisasa ya standard gauge na makaa ya mawe. Alisema alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Zuma ambaye nchi yake ni mwanachama wa nchi tano zenye nguvu kiuchumi zikiwemo Brazil, Urusi, China na India (Brics), kwa ajili ya kuiombea Tanzania mkopo nafuu na kumalizia mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
“Ni ukweli kuwa Tanzania tumefanya mengi katika ukombozi wan chi za Afrika, tumejitolea katika mambo mengi na kwa upendo mkubwa. Ndio maana tunaomba hawa tuliowasaidia nao watusaidia kidogo. Nashukuru kwani katika hili tayari Rais Zuma ameonesha nia ya kutusaidia,” alisisitiza Dk Magufuli. Alisema katika eneo la utalii nchi hizo zimekubaliana kushirikiana na kubadilishana uzoefu na utalaamu hususani katika kutoa huduma za kitalii. “Lakini pia tumeomba wawekezaji kutoka Afrika Kusini waje wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na kuboresha fukwe kwani kwa sasa Tanzania imebarikiwa kuwa na fukwe nyingi ambazo hazijaendelezwa,” alieleza Dk Magufuli.
Kwa upande wa madini, alieleza kuwa nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika ikubadilishana uzoefu, utaalamu na usimamizi ikiwemo kuwahamasisha wawekezaji wa Afrika Kusini kutumia fursa hiyo na kuwekeza katika viwanda vya kuchakatua michanga ya dhahabu hapa nchini badala ya kupelekwa nje ya nchi. Aidha, alisema pia nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika eneo la afya kutokana na ukweli kuwa nchi ya Afrika Kusini imepigahatua hasa katika eneo la tiba ya magonjwa ya moyo na figo.
Kupitia makubaliano hayo, Tanzania imeomba uwekezaji kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya dawa. Akielezea eneo la elimu, sayansi na teknolojia, Dk Magufuli lisema nchi hizo zimekubaliana kushirikiana kupitia eneo la utafiti na elimu ya juu kwa kubadilisha uzoefu wa walimu lakini pia Tanzania imekubali kupeleka walimu wa Kiswahili kwenda kufundisha Afrika Kusini. Alisema pia wamekubaliana kushirikiana katika ulinzi na usalama katika kupambana na uhalifu wa ugaidi, biashara ya binadamu, uharamia, ujangili na dawa za kulevya.
Pamoja na hayo, alibainisha kuwa nchi hizo mbili zimekubaliana kuendelea kushirikiana kupitia vyama vyao vya siasa vikongwe vya ANC na CCM ambavyo vina historia ndefu Afrika. Alieleza kuwa katika mazungumzo hayo, marais hayo wamekubaliana kuhakikisha wanashirikiana katika kutatua migogoro ya nchi nyingine za Afrika hasa migogoro inayoendelea katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Lesotho. Alisema katika kuhakikisha makubaliano hayo na mikataba ya ushirikiano ambayo nchi hizo tayari imeingia yanatekelezwa ipasavyo, wamekubaliana kuunda chombo cha usimamizi kitakachofuatilia utekelezaji wa makubaliano na mikataba hiyo na endapo kutabainika kikwazo au uzembe hatua zichukulie kudhibiti.
“Napenda Watanzania watambue kuwa ziara hii ina mafanikio makubwa sana, Afrika Kusini ni ndugu zetu nawahakikishia Tanzania itaendelea kuheshimu uhusiano uliopo kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Dk Magufuli. Kwa upande wake, Rais Zuma alizungumzia mazungumzo yake na mwenyeji wake na kubinisha kuwa wamekubaliana kuyaunga mkono mapendekezo ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili yaliyowasilishwa na mawaziri wote wawili wa Tanzania na Afrika Kusini. Alisema katika mazungumzo hayo wamekubaliana mambo mengi ikiwemo kushirikiana katika ulinzi na usalama, elimu, sayansi na teknolojia, biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati na madini.
“Lakini kikubwa zaidi tumekubaliana kukuza uchumi wetu kwa kushirikiana na sekta binafsi,” alisema Rais Zuma. Alisema ziara yake hiyo ni ya mafanikio kwani wamezindua Tume ya Marais ambayo kazi yake kubwa itakuwa ni kuisimamia ukuaji wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili na wamepanga tume hiyo kukutana mara kadhaa tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambako tangu iundwe mwaka 2011, imekutana kwa mara ya kwanza mwaka huu.
“Tumewaelekeza pia mawaziri wetu hawa kuhakikisha wanamalizia kutafuta muafaka juu ya maeneo tuliyopendekeza kushirikiana ambayo mpaka sasa hayajapata ufumbuzi. Aidha Rais huyo aliielezea Tanzania kuwa ni nchi inayopewa heshima kubwa nchini Afrika Kusini kutokana na mchango wak katika kulikomboa taifa hilo katika mikono ya wakoloni na wabaguzi wa rangi.
Alisema ziara hiyo imekuja wakati muafaka wakati nchi hiyo ikisherehekea miaka 100 tangu kuzaliwa kwa aliyekuwa Rais wa ANC, Oliver Tambo ambaye nchi hiyo inamtambua kama shujaa na mwanapinduzi. “Hii ni ziara muhimu kwetu sisi Afrika Kusini kwani mwaka huu, Oktoba tunasherehekea kuzaliwa kwa shujaa wetu, Oliver Tambo. Tanzania imeshiriki kikamilifu katika maisha yake ikiwemo kuzaliwa kwa chama cha ANC,” alifafanua Rais Zuma.
Pia Rais huyo alimkumbuka mmoja wa Watanzania waliofanikisha harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, hayati Brigedia Jenerali Hashim Mbita aliyefariki mwaka jana kuwa alifanya kazi bega kwa bega na Oliver Tambo katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika Kusini. Alisema Tanzania ilikuwa ni nyumbani kwa wanaharakati wote wanaodai ukombozi na mpaka sasa nchi hiyo bado iko mstari wa mbele kupigania uhuru wa nchi nyingine za Afrika ikiwemo ukoloni mamboleo na ubaguzi wa rangi.
No comments
Post a Comment