Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, February 27, 2016

Kilio cha wafanyakazi waliomzuia Majaliwa chamfikia waziri

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, amesikiliza kilio cha wafanyakazi wa Kampuni ya Tarmal ambayo ni Wakala wa Kampuni ya PSI. Jenista alikwenda jana kusikiliza kilio cha wafanyakazi hao baada ya juzi kumfikishia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya kuzuia msafara wake uliokuwa ukitoka katika hafla ya kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya Sh bilioni 10 vilivyotolewa na umoja wa kampuni zinazozalisha vinywaji laini kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Wafanyakazi hao waliopo katika Ghala la PSI lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam, waliuzuia msafara wa Waziri Mkuu na kumwambia baadhi ya kero wanazokumbana nazo wawapo kazini. Baada ya Jenista kufika katika ofisi za kampuni hiyo, aliwapa muda wafanyakazi kutoa malalamiko yao na kwa kupokezana walisema kilio chao kikubwa ni suala la mishahara midogo pamoja na mikataba. Pia walisema jambo jingine ni makato yao ya mishahara kutopelekwa katika Mfuko wa Pensheni wa PPF. “Tumekuwa tukikatwa fedha zetu huku tukiambiwa kuwa zinaenda PPF kumbe hazipelekwi, mfano tangu mwaka 2014 hakuna fedha yoyote iliyopelekwa, sisi tukienda kufuatilia tunaambiwa hakuna fedha iliyopelekwa,” alisema Amani Athumani kwa niaba ya wenzake. Pia alisema ushirikiano baina ya mwajiri na waajiriwa ni mdogo na wanaweza kupeleka matatizo yao lakini wasipate majibu, hawapandishiwi mishahara na kama wakipandishiwa ni Sh 500 pia hailipwi kupitia benki. Baada ya kumaliza kuwasikiliza, Jenista alilazimika kutoa maagizo yatakayowezesha upatikanaji wa haki zao. Katika maagizo yake aliunda kamati ndogo itakayojadili malalamiko ya watumishi hao na baada ya siku tano itatoa mrejesho wa makubaliano yaliyofikiwa. “Naagiza kamati hii niliyoiunda ambayo ina wawakilishi watano kutoka miongoni mwa watumishi hawa, uongozi wa kampuni, mwakilishi kutoka PPF pamoja na wataalamu wa wizara na itaanza kufanya kazi leo (jana) na baada ya siku tano itarudi hapa kuleta mrejesho wa yale waliyokubaliana,” alisema Jenista. Alisema kazi ya kamati hiyo itakuwa ni kupitia mikataba yote na kupitia taarifa za makato ya fedha zilizopaswa kupelekwa PPF na kuomba uongozi wa kampuni hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha. Pia aliuagiza uongozi wa Tarmal kuhakikisha unawezesha wafanyakazi hao kuunda chama chao kitakachokuwa kinashughulikia malalamiko yao. Katika hatua nyingine, baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Tech Park inayoshughulika na uzalishaji wa mifuko ya kupakia saruji walimzuia kuondoka hadi atakapowasikiliza shida zao. Hata hivyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Antony Mavunde, alilazimika kukatisha safari yake na kwenda kusikiliza malalamiko yao. Wafanyakazi hao walimweleza Mavunde kuwa kwa muda mrefu wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi huku mishahara wanayolipwa ni midogo. “Kazi tunayoifanya ni kubwa wakati malipo tunayolipa ni madogo ukilinganisha na ukubwa wa kiwanda chenyewe ambacho ni kikubwa kuliko viwanda vyote vya Afrika vinavyozalisha mifuko ya saruji inayotumika nchi nzima,” alisema James Charles. Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Sultan, alisema wananyanyaswa na raia wa kigeni walioko kiwandani hapo, kupewa mikataba mifupi, mishahara midogo na makato yao kutopelekwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Chanzo:http://mtanzania.co.tz Baada ya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi hao, Mavunde aliagiza hadi kufika Ijumaa ya wiki ijayo uongozi wa kampuni hiyo uwe umewapa waajiriwa wao mikataba inayoendana na taratibu zote na kuhusu mishahara aliagiza wataalamu wa wizara kukaa na uongozi na wawakilishi wa wafanyakazi hao kujadili stahiki hizo. “Kufikia Jumatatu nataka niletewe nakala za vibali vya hao wafanyakazi wageni raia wa India na ripoti ya kuwa ni Watanzania wangapi hao wageni wamewaongezea ujuzi kama sheria za kazi zinavyosema,” alisema Mavunde. Kuhusu malalamiko ya makato ya mishahara yao kutopelekwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii, Mkurugenzi Uendeshaji wa PPF, Asunta Mallya, alisema ofisi yake imekuwa ikiifuatilia kampuni hiyo lakini imekuwa na usumbufu. “PPF imekuwa ikifuatilia sana stahiki za wafanyakazi hawa na mwajiri wao amekuwa akituletea shida na hadi sasa tunamdai zaidi ya shilingi milioni 74 na tumekwisha kumpeleka mahakamani ili kulipa fedha hiyo,” alisema Mallya.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment