Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, July 2, 2015

Upinzani wambana Dk Migiro, AG bungeni

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, jana alibanwa bungeni baada ya wabunge wa upinzani kuhoji juu ya Muswada wa Sheria ya Kulinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 wakieleza umewahishwa bila sababu yoyote. Dk Migiro alikutana na kimbuga cha upinzani ikiwa ni siku moja baada ya Bunge la 10 kuigomea Serikali ilipotaka kuingiza bungeni miswada mitatu iliyohusu Wizara ya Nishati na Madini wakisema inahitaji muda mzuri. Mapema jana, Dk Migiro aliwasilisha ndani ya Bunge muswada huo akilitaka lijadili na kuupitisha ili kutoa nafasi ya kuwalinda watu wa aina hiyo. Akiwasilisha maoni ya upinzani bungeni, msemaji wa kambi hiyo katika Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu alisema muswada huo hauna tija kwa muda huo kwani unatoa nafasi finyu kwa wabunge kujadili jambo ambalo ni muhimu zaidi kwa wananchi. Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema uharaka wa muswada huo ni kiashiria tosha kwamba Serikali inataka kuminya uhuru wa wabunge kupitia kwa kina sheria hiyo. “Kanuni zinasema kuwa, sheria inaweza kupitishwa kwa hati ya dharura ikiwa tu kuna mambo ambayo yanataka kutokea ambayo ni pamoja na majanga au vita. Je, kuna uharaka kiasi gani wa kupitisha muswada huu?” alihoji Lissu. Mbunge huyo mbali na kutoa ufafanuzi katika vifungu vingi katika muswada huo, lakini alisisitiza kuwa ukipitishwa utakuwa umewanyima haki watu wa kada ya chini na kuwapa mwanya viongozi wao. Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alipinga vikali muswada huo pamoja na namna ulivyowasilishwa na akazua mgogoro mkubwa baina yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), George Masaju. Malumbano ya wawili hao yalianzia pale Mnyika aliposema kuwa Serikali ni dhaifu katika suala zima la utungaji wa sheria jambo ambalo pia liliamsha hasira za Spika. Katika hoja zake, Mnyika alipinga jinsi muswada ulivyokuwa ukitoa upenyo kwa watu kutoa taarifa kwa wakubwa wao badala ya kuzipeleka kwa vyombo vingine. “Mfano, muswada unaelekeza mtu kutoa taarifa kwa kiongozi wake yaani akiwa mfanyakazi wa benki kuu anawezaje kutoa taarifa za ufisadi wa gavana kwa gavana mwenyewe?” alihoji Mnyika. AG Masaju alipinga kauli za kuwa Serikali inafanya vitu dhaifu akisema siyo nia yao, bali wanafanya kazi ya kupeleka miswada ili wabunge wenyewe ndiyo wafanye uamuzi. Kwa upande wake, Spika Anne Makinda alimtaka Mnyika kuondoa kile alichokiita ni upuuzi ili aweze kujadili mambo yaliyo mbele yake kwani anaonekana kuwa hakuwa na maandalizi. “Mnyika mbona tunabishana sana kwa mambo ya kitoto, ondoa upuuzi wako sasa na ujielekeze kwenye muswada wenyewe,” alisema Makinda. Akichangia hoja hiyo Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alipinga mfumo ambao unatumiwa katika kutengeneza sheria hiyo ya kuwalinda watoa taarifa kwamba hauna maana yoyote. Kafulila alisema ndani ya Tanzania, kuna vitu vingi ambavyo vinafanywa ikiwamo ufisadi mkubwa unaowahusisha watu wa ngazi ya juu lakini hakuna wa kuwalinda. “Mimi nilipotoa taarifa humu ndani, kwanza Spika ulisema nilichokoza mwenyewe, nikaenda kwa RCO (Ofisa Upelelezi) Mkoa wa Dodoma kisha kwa IGP, lakini kote sikupata msaada wowote,” alisema Kafulila na kuongeza; “Kutokana na hilo, nikaamua kukimbilia Israel na kwenda kupiga magoti katika ukuta wa Suleiman ili nipate ulinzi ambao hadi leo ndiyo nategemea.” Kwa upande wa wabunge wa CCM, Maria Hewa ndiye aliyekuwa mbunge pekee ambaye alisema kuwa muswada huo ulikuwa na uharaka ambao haukutakiwa kwa wakati huo. Wabunge wengine wa chama hicho; Ismail Rage, Grace Puja na Dk Mary Mwanjelwa wote waliunga mkono muswada huo. Mabishano ya vifungu vya muswada huo yaliendelea huku Lissu akionekana kuwa mwiba kwa Dk Migiro na AG lakini hata hivyo, vifungu alivyokuwa akivipinga vilipitishwa kutokana na wabunge kuhojiwa na sauti za ndiyo kuzizidi zile za hapana. Hata hivyo, muswada huo haukupitishwa jana baada ya muda wa Bunge kuisha.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment