Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, March 2, 2015

SERIKALI IKO MBIONI KUUGAWA MKOA WA MBEYA

SERIKALI imeyapokea maombi ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) cha Mkoa wa Mbeya yanayopendekeza mkoa huo ugawanywe na kupata mikoa miwili ya Mbeya na Songwe. Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumamosi, Februari 28, 2015) kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imeridhia maombi hayo kutokana na ukubwa wa mkoa huo ambao una kilometa za mraba 63,000. "Tumekwishapokea maombi ya kuugawanya mkoa wa Mbeya kwa sababu mkoa huu una eneo la kilometa za mraba 63,617 zilizogawanyika katika Wilaya 8 na Halmashauri 10. Hili ni eneo kubwa sana kiutawala, siyo rahisi kuusimamia na kusukuma maendeleo," alisema. Alisema kamati hiyo imeshauri mkoa huo ugawanywe katika wilaya nne nne ambapo mkoa mpya wa Songwe utakuwa na wilaya za Ileje, Momba, Mbozi na Chunya. Wamekubaliana kuwa makao makuu yatakuwa Mbozi lakini ninyi wa chunya mmeenda mbali zaidi kwa kuigawa Chunya kwenye wilaya mbili za Songwe na Chunya ambapo chunya itaenda Mbeya," alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa. Alisema katika kikao hicho ilikubaliwa kwamba makao makuu ya wilaya mpya ya Songwe yatakuwa Mkwajuni. "Nimekubali maombi haya kwa sababu yatapunguza gharama za uendeshaji, na kama itashindikana kupata wilaya mpya basi itabidi tuwape Halmashauri ya Songwe," alisema. Mkoa wa Mbeya una wilaya nane ambazo zimegawanyika katika tarafa 27, kata 262, vijiji 842 na mitaa 252. Idadi ya wakazi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni 2,707,410. Akizungumzia kuhusu mpango wa maji katika wilaya hiyo, Waziri Mkuu alisema bado kuna changamoto kubwa ya kufikisha maji vijijini ambako upatikanaji wake uko kwenye asilimia 46. "Tuna mpango wa kuchimba visima vikubwa vitatu na mwakani tuna mpango wa kuchimba visima vingine virefu 11, tunachohitaji ni fedha na usimamizi," alisema. Alivitaja vijiji viyakavyopata visima hivyo ni Makongorosi, Mkwajuni, Kapalala, Isangawana, Galula, Lupa na Matwiga. Vingine ni Kambikatoto, Tanile, Bitimanyanga na Mapogoro. Wakati huohuo, Waziri Mkuu amezindua maabara tatu katika shule ya sekondari ya Saza ambazo zimejengwa kwa ufadhili wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta. Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya, Bi. Sophia Kumbuli alisema ujenzi wa maabara hizo tatu umegharimu sh. Milioni 268.5 vikijumuisha pia ununuzi wa samani, uwekaji wa mfumo wa maji na gesi. "Kati ya hizo sh. Milioni 23.5 ni za ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali na sh. Milioni 245 ni ujenzi wa jengo, samani na uwekaji wa mfumo wa maji na gesi," alisema. Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI – Mbimba.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment