Writen by
sadataley
10:12 AM
-
0
Comments
Msalaba
Iringa. Waraka uliotolewa juzi na Jukwaa la Wakristo Tanzania
wakitaka mchakato wa Katiba Mpya usitishwe, jana ulisomwa katika baadhi
ya makanisa na sasa utasambazwa katika jumuiya ndogo za Kanisa Katoliki.
Akizungumzia waraka huo katika Ibada ya Jumapili,
Paroko wa Parokia ya Mkwawa ya Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Padri
Oscar Rutechura alisema amechukua uamuzi huo ili kuwawezesha waumini
kuelewa vizuri tamko la viongozi wao wa dini kuhusu mchakato wa katiba
unaoendelea.
“Katika ibada hii ya leo nitatoa mahubiri kwa muda
mfupi, nitafanya hivyo ili niweze kufanya mambo mengi yaliyoko mbele
yangu,” alisema Padri Rutechura kabla ya kusoma waraka huo.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la
Waadventista Wasabato (SDA).
Padri Rutechura alitaja mapendekezo sita yaliyomo
kwenye waraka huo ambayo ni: Kuitaka Serikali irudishe tovuti ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kulitaka Bunge kuboresha maoni ya wananchi
yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba na kuacha kuyadharau na kuyapuuza.
Mengine ni kutaka mchakato wa Katiba usitishwe,
Bunge la Katiba liendeshwe kwa mujibu wa kanuni, wananchi waendelee
kusoma na kufuatilia mchakato na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihusishwe
na kupewa mamlaka ya kujibu maswali yanayojitokeza.
Padri Rutechura alisisitiza kuwa ametumiwa waraka
huo na Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa
ambaye kwa sasa ndiye Rais TEC kwa ajili ya kuusoma kwa waumini wote.
Alisema baada ya kuusoma angetoa nakala na
kuzigawa kwa viongozi wa jumuiya ndogondogo ili waumini wote wa parokia
hiyo wapate fursa ya kuusoma na kuuelewa na watoe uamuzi sahihi.
Padri Rutechura aliwataka waumini kuhakikisha
wanajiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la wapigakura pindi
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itakapotangaza kuanza kuandikisha upya
wapigakura.
Alisema hatua hiyo itawasaidia waumini hao
kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupiga kura ya maoni kupata
Katiba Mpya au kuipinga, kuchagua viongozi wanaofaa katika uchaguzi wa
serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Wakati huohuo, polisi wilaya mpya ya kipolisi,
Mbalizi mkoani Mbeya wamewakamata waumini 16 wa Kanisa la Katoliki,
Parokia ya Songwe kwa madai ya kutaka kufanya vurugu kwenye kanisa lao.
Paroko wa Parokia hiyo, Ernest Mwashiuya alisema waumini hao walikamatwa jana na kwamba taarifa zaidi zitatolewa na polisi.
Baadhi ya waliokamatwa walisema tukio hilo lilitokea Jumamosi
saa 12 jioni wakati wanajadili sehemu ya kusalia ibada ya Jumapili baada
ya kutokuwa na imani na paroko wao. Walisema hatua hiyo ilichukuliwa
baada ya Paroko Mwashiuya, Jumapili ya Agosti 24 kutamka kwamba waumini
wasio na imani naye wasifike kanisani hapo tena.
“Polisi walifika nyumbani kwa Emmanuel Kalomba
tulikokuwa tukisali na kutukamata,” alisema mmoja wa waumini
waliokamatwa na kuachiwa kwa dhamana.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema hakuwa na taarifa.
Nyongeza na Lauden Mwambona, Mbeya
No comments
Post a Comment