Writen by
sadataley
3:52 PM
-
0
Comments
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
CONGO —Mjadala
mkali umeibuka baada ya maaskofu wa kanisa katoliki nchini Kongo
kumuomba rais Joseph Kabila kutobadili katiba ya nchi hiyo ili kumruhusu
kuwania muhula wa tatu.Upinzani umelezea kwamba msimamo huo wa maaskofu
ni jibu muafaka la njama ya chama tawala kutaka rais Kabila aendelee
kubaki madarakani,huku chama tawala kikiwa na tafsiri nyingine ya ujumbe
huo.
Bado chama tawala hakijatoa msimamo wake
rasmi kuhusu tangazo la maskofu wa kanisa katoliki la kumtaka rais
Joseph Kabila kutowania muhula wa tatu ifikapo mwaka wa 2016.Lakini
baadhi ya wabunge na vigogo wa chama wamepokea kwa shingo upande
pendekezo hilo la maaskofu wa kanisa katoliki.Mbunge Shiko Mwepu amesema
kwamba maaskofu hao wameunga mkono jumuiya ya kimataifa katika dhana
zisizokuwa na msingi wowote, kwake yeye ni kwamba viongozi hao wa kanisa
wamejiingiza katika siasa. "Ikiwa wanataka kufanya siasa basi wavue
kanzu ", alisema mbunge huyo kutoka jimbo la Katanga .
Kwa upande wake upinzani umepongeza msimamo
huo wa maaskofu,Vital Kamerhe kiongozi wa chama cha UNC ameandika
kwenye mtandao wa Twita kwamba maaskofu wametaka kunusuru demokrasia
kutokana na njama ya wanasiasa wa chama tawala.Katibu
mkuu wa Kongamnao la maaskofu na ambaye ni msemaji wake,padre Leonard
Santedi amewambia wandishi habari kwamba ni muhimu katiba itekelezwe.
"Tumeliomba bunge kujizuia
na kupitisha miswaada ya sheria ambayo inaweza kuhujumu katiba na
taratibu ya kidemokrasia nchini hapa".
Ombi hilo linaelezewa na
maaskofu hao kuwa ni juhudi za kuweko na mageuzi ya kidemokrasia nchini
Kongo.Katiba ya Kongo inaelezea kwamba rais amechaguliwa na raia kwa
muhula wa miaka mitano na anaweza kuwania tena muhula wa pili na wa
mwisho.Kipengele hicho kimebanwa na kile cha 220 ambacho kinaelezea
kwamba mfumo wa uchaguzi,uwingi na kipindi cha mihula ya rais havipaswi
kurekebishwa kwa sababu yeyote ile.Claude Kayembe ni mwandishi habari na
ameelezea jinsi ujumbe huo wa maaskofu unapokelewa na raia wa Kongo
Hata hivyo maaskofu hao
wameunga mkono tume ya uchaguzi CENI ili kuendelea na shughuli zake za
maandalizi ya uchaguzi na vilevile serikali imepongezwa katika kurejesha
amani huko Kivu.
Hadi sasa
rais Kabila bado kutangaza msimamo wake kuhusu mjadala uliojitokeza
kuhusu swala la kubadilishwa kwa katiba na vilevile ikiwa atawania
muhula wa tatu au hapana.Msemaji wa serikali ya Kongo Lambert Mende
amesema bila shaka rais kabila ataheshimu katiba.Mende aliendelea kusema
kwamba bado rais Kabila ana miaka 2 na nusu ya kuongoza nchi hiyo kwa
hiyo swala la kujua ikiwa atagombea au hapana haliko kwenye ajenda ya
serikali kwa sasa. Mende amelezea misimamo ya hapa na pale kuhusu
mageuzi ya katiba ni dhana ya watu binafsi.
Wakati wa
ziara yake mjini Kinshasa mwanzoni mwa mwezi Mei,waziri wa mambo ya nje
wa Marekani John Kerry aliwaambia waandishi wa habari kwamba miongoni
mwa maswala waliozungumzia na rais kabila ni pamoja kumuomba kutobadili
katiba.Haijulikani jibu la rais lilikuwa ni lipi ?

No comments
Post a Comment