Writen by
sadataley
3:15 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
London. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali inaandaa kongamano la siku mbili litakalojadili mustakabali wa Watanzania kutoka nchi zote duniani ikiwa ni pamoja na kukutanisha kampuni na wafanyabiashara mbalimbali.
Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipokutana na
Watanzania wanaoishi Uingereza kwenye mkutano uliofanyika katika
ubalozi wa Tanzania jijini hapa.
Waziri Mkuu alisema kongamano hilo limepangwa
kufanyika Agosti 14-15, mwaka huu, linalenga kuitambulisha rasmi
diaspora ama jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni kama wadau muhimu
katika kuleta maendeleo nchini Tanzania
“Lengo letu hasa ni kutaka jamii ya Watanzania
ielewe kwamba tunao Watanzania walioko nje ya nchi kwa maelfu na kuna
sehemu mnaweza kuchangia katika maendeleo ya nchi,” alisema.
Mbali na hilo, Waziri Mkuu alisema katika
kuitambua rasmi jamii ya wanadiaspora, Serikali itapenda kujua wako
wangapi na wanafanya nini ili kama Serikali itahitaji ujuzi/utaalamu wao
inaweza kuwapata wapi.
Alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa
ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Umoja wa Wanadiaspora waliorudi
nchini waitwao Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
“Kongamano hilo litasaidia wanadiaspora kuweza
kuona fursa zilizopo nchini, kuvutia wawekezaji wageni kuwekeza
Tanzania, kukuza utalii nchini, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa
diaspora pamoja na kuunganisha wawekezaji wa Tanzania na walioko nje ya
nchi,” alisema waziri mkuu.
Mada kuu ya kongamano hilo ni “Connect, Engage,
Inform and Invest” na kauli mbiu yake ni “Nyumbani ni Nyumbani”.
Aliwataka wajitokeze kwa wingi kushiriki kongamano hilo alilosema
limeandaliwa mahsusi kwa ajili yao na wasipojitokeza kwa wingi
halitakuwa na maana.
No comments
Post a Comment