Writen by
sadataley
11:35 AM
-
0
Comments
Sheikh Ahmed Haidar Jabir akiwa amelazwa katika Hospitali ya Alrahma
iliyopo Kilimani Zanzibar, baada ya kujeruhiwa na bomu na watu
wasiojulikana na kusababisha kifo cha mtu mmoja. Picha na Mwinyi
SadallahTanga. Kamati ya Amani na Uhusiano wa viongozi
wa madhehebu mbalimbali ya dini Mkoa wa Tanga imelaani kitendo cha
ulipuaji wa bomu mjini Unguja uliosababisha kifo cha mtu mmoja.
Akitoa taarifa ya pamoja na viongozi wa dini
kulaani mauaji hayo, Sheikh wa Mkoa wa Tanga na Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Juma Luwuchu aliitaka Serikali kuchukua hatua kuwasaka wote
waliohusika na mlipuko huo.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameliagiza Jeshi la
Polisi kuhakikisha linawatia mbaroni wote waliohusika na mashambulizi
hayo yaliyosababisha maafa na kujeruhi wengine.
Alikemea tukio hilo na kuitaka jamii ya Watanzania
kukataa matukio ya mauaji kama hayo kwa sababu yanahatarisha amani
ambayo Watanzania wanajivunia.
Akifungua kikao cha kamati ya viongozi wa
madhehebu ya Kiislamu na Kikristo Wilaya ya Tanga jana kuzungumzia
mustakabali wa amani nchini, Sheikh Luwuchu alisema tukio la kuwaua
viongozi wa dini kwa mabomu siyo kwamba limewashtua, bali pia limeleta
taswira mbaya ya Tanzania kwa nchi nyingine duniani.
“Ili kukabiliana na matukio hayo ya mauaji,
nimewaagiza viongozi wa madhehebu yote ya dini kupaza sauti zao kukemea
kila wanapopata nafasi ya kuzungumza na waumini wao ikiwamo kulaani
vitendo hivyo.
“Wanaoendesha vitendo hivyo wakiona kila kona
wanalaaniwa wataona jamii haiwataki na hatimaye wataacha tu,” alisema
Sheikh Luwuchu.
Pia alilaani mauaji ya albino, vikongwe na vitendo
vya kumwagiwa tindikali vinavyoshamiri nchini akisema havina budi
kupigwa vita kwa kushirikiana na Serikali.
Kabla ya kuanza kikao hicho, wajumbe wa kikao
hicho ambao ni masheikh, maaskofu, wachungaji na mapadri walitembelea
kituo cha vijana walioamua kuacha kutumia dawa za kulevya na kuzungumza
nao juu ya masuala ya amani.
Wakiwa katika kituo hicho kilichopo Duga, wajumbe
hao walielezwa na vijana hao juu ya changamoto wanazokabiliana nazo
baada ya kuacha kutumia dawa za kulevya na kuomba jamii isiwatenge.
No comments
Post a Comment