Writen by
sadataley
2:16 PM
-
0
Comments
Rais mpya wa klabu ya Simba, Evans Aveva akihutubia katika katika
mkutano wa uchaguzi wa klabu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la
Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, jana. Picha na Michael
Matemanga.
Na Vicky Kimaro, MwananchiDar es Salaam. Evans Aveva ameula baada ya
kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa klabu ya Simba katika uchaguzi mkuu
uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Bwalo la Polisi, Oysterbay
jijini Dar es Salaam.
Aveva alipata ushindi huo wa mithili ya kimbunga
baada ya kupata kura 1845 na kumgaragaza mpinzani wake Andrew Tupa
aliyepata kura 387 huku kura sita zikiharibika.
Katika nafasi ya Makamu wa Rais, Geofrey Nyange
‘Kaburu’ ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 1043 huku Jamhuri
Kihwelo ‘Julio’ akipata kura 413 na Swedy Mkwabi akipata kura 300.
Awali, aliyekuwa mgombea Urais wa klabu hiyo, Michael Wambura alizuiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kuingia kwenye Ukumbi.
Wambura, alienguliwa kwanza kwa kuwa amesimamishwa
uanachama na baadaye kwa kukiuka taratibu za uchaguzi, alishindwa
kupiga kura kutokana na uamuzi wa kumzuia kuingia ukumbini.
Kwa mujibu wa wasimamizi waliokuwa wakihakiki
uhalali wa wanachama kwenye uchaguzi huo, jina la Wambura halikuwapo
katika orodha ya wanachama wanaostahili kupiga kura.
Wambura kama walivyokuwa wanachama wengine,
walifika katika eneo la uchaguzi kwa ajili ya kukamilisha haki hiyo ya
kikatiba, lakini alionekana kushangazwa na uamuzi huo wa kuzuiwa kupiga
kura.
Jibu alilopewa lilimfanya kuondoka maeneo hayo kwa
hasira majira ya saa 4:00 asubuhi. Wakati hayo yakitokea, wafuasi wake
walionekana kukasirishwa na kitendo hicho na kutaka kufanya fujo, hata
hivyo askari waliokuwapo maeneo hayo walizima jitihada hizo.
Katika mkutano huo wa uchaguzi ulioanza rasmi saa
5:00 asubuhi, lilipomalizika zoezi la wagombea kujinadi, zoezi la kupiga
kura liliibua vurugu nzito kutokana na wanachama wengine kukosa
karatasi za kupigia kura kwa nafasi za rais na makamu wake.
Hali hiyo ilichangiwa na wanachama kushindwa kuwa
na utulivu. Hata hivyo, baada ya muda zoezi hilo liliendelea kukiwa na
utulivu mdogo katika zoezi hilo la kupiga kura lililoanza saa 9:00
alasiri na kura kuhesabiwa saa 11:00 jioni.
No comments
Post a Comment