Writen by
sadataley
5:50 PM
-
0
Comments
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akichangia
mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15,
mjini Dodoma juzi na akiwa ameshikilia gazeti la Mwananchi. Picha na
Edwin Mjwahuzi
Na Mwandishi Wetu, MwananchiDodoma. Serikali italazimika kulipa hasara ya
zaidi ya Sh5.2 bilioni (Dola za Marekani milioni 3.1) ambazo ni riba ya
malimbikizo ya malipo ya miezi sita kwa Kampuni ya Jacobsen Elekron AS
inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa Kinyerezi, Dar es
Salaam.
Gazeti hili limebaini kuwa kampuni hiyo ya Norway
inaidai Serikali Dola 48.8 milioni (Sh80.52 bilioni), yakiwa ni
malimbikizo ya malipo kuanzia Novemba mwaka jana na Mei mwaka huu.
Mbali ya hayo, kampuni hiyo ilitishia kusitisha
utekelezaji wa mradi huo na kuondoa vifaa vyake kama isingelipwa walau
Dola milioni 25 za Marekani (Sh41.25 bilioni) hadi Juni 15 mwaka huu.
Katika barua yake ya Juni 5, 2014 iliyosainiwa na
Meneja wa Mradi wa Kinyerezi wa Jacobsen, Stein Sundbye kwenda kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kunakiliwa
kwa Katibu Mkuu - Hazina na mwenzake wa Nishati na Madini, kampuni hiyo
imelalamikia ucheleweshaji wa malipo hayo kinyume cha mkataba baina ya
pande hizo mbili.
“Rejea barua yetu ya 23 Mei, 2014 iliyotoa ilani
ya siku 14 kwamba tutasitisha kazi zetu kwa mujibu wa kipengele 41.2 cha
mkataba, isipokuwa kama tutapokea malipo tunayodai ya Dola 48.8 milioni
kama ankara ya madai iliyoambatanishwa hapa inavyoonyesha,” inasema
sehemu ya barua hiyo na kuongeza:
“Kama tulivyoeleza ilani hii inamalizika Juni 6,
2014 wakati usitishaji wa kazi utakapoanza. Licha ya kuomba tulipwe au
tuambiwe ni lini malipo hayo yatatolewa, hatujapokea majibu yoyote ya
kupewa fedha zetu zote au kwa awamu kama ilivyokuwa imeahidiwa na Wizara
ya Fedha katika barua yenye Kumbukumbu namba CDA.327/602/01 ya Aprili
4, 2014.
Laibuka bungeni
Juzi jioni, suala hilo liliibuliwa na Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema Serikali imekuwa
ikipata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na kupanga utekelezaji wa
miradi mikubwa pasipokuwa na uhakika wa fedha.
Akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali, Mbowe
ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) alisema: “Wakati Serikali
ikitafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, tumekuwa tukiingia
kwenye madeni ya ajabu ambayo kama tungekuwa makini yangeweza kuepukwa.
“Ninao mfano halisi hapa ambao unaonyesha jinsi
Serikali itakavyolazimika kulipa riba ya zaidi ya Sh5 bilioni kutokana
na kushindwa kulipa fedha za Kampuni ya Jacobsen inayojenga mradi wa
Kinyerezi One, hii ni aibu kubwa maana tumelimbikiza madeni ya miezi
sita na wanatudai Dola za Marekani 48 milioni.”
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius
Likwelile alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema hakuwa amepata taarifa
kuhusu tishio la Jacobsen kusitisha mradi, lakini akaahidi kufuatilia
ili kutoa taarifa baadaye... “Nafahamu kwamba Jacobsen tunafanya nao
kazi tena vizuri sana, sidhani kama wanaweza kufikia hatua ya kusitisha
kazi, ila ahsante kwa taarifa nitafuatilia ili kujua ukweli ni upi.”
Baadaye kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi Dk
Likwelile alisema: “Naomba nikuhakikishie kwamba jitihada za kuhakikisha
nchi inakuwa na umeme wa uhakika ni kipaumbele cha kwanza cha Serikali
na mkataba baina ya Serikali na Jacobsen ni sehemu ya jitihada hizo.
Nitashangaa sana iwapo jambo kama hilo litatokea pasipo sisi (Serikali)
kufahamu na kuliridhia.”
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Serikali-kulipa-riba-Sh5-bilioni-deni-la-miezi-sita/-/1597296/2352278/-/11w2w3z/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Serikali-kulipa-riba-Sh5-bilioni-deni-la-miezi-sita/-/1597296/2352278/-/11w2w3z/-/index.html
No comments
Post a Comment