Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, June 30, 2014

HOJA: ONGEZEKO LA IMANI ZA UCHAWI MAKANISANI TANZANIA

Msomaji, katika matoleo mawili yaliyopita tumeshuhudia kwamba shughuli za uchawi ziko chini ya nguvu za pepo wachafu ambao wanatumika na binadamu walioamua kufanywa mawakala wa majini. Aidha, tuliona pia kwamba Mungu alikwisha kutoa mamlaka kupitia watumishi wake kukomesha shughuli za uchawi katika jamii ili watu waziache nguvu za Shetani na kumrudia na kumtegemea Mungu. Pia tuliabaini kwamba, Mungu alipiga marufuku swala zima la kuwaendea wachawi au kujihusisha na shughuli za uchawi na hukumu ya adhabu yake ni kutupwa kwenye ziwa la moto. Katika makala yaleo niahidi kwamba tutapitia uchambuzi wa chanzo kikuu cha uongezeko la kuogopa uchawi kanisani:

Chanzo Ongezeko la kuogopa uchawi kanisani dalili za kupoteza mamlaka ya Kristo

  Mpendwa Msomaji, sasa tunaingia katika kuchambuzi makini wa kutafuta chanzo cha kuongezeka kwa hofu dhidi ya uchawi iliyoshamiri makanisani siku hizi. Kama tulivyokwisha kusoma katika makala zilizopita ya kwamba Yesu aliwapa wanafunzi wake mamlaka ya “kutoa” pepo kama ishara mojawapo ya kuhubiri Injili ya kwa kila mtu asiyeamini. Huduma hizi zilikuwa ni sehemu ya kudhihirisha mamlaka ya Mungu dhidi ya nguvu za giza.

Lakini, katika kuyachunguza maandiko siku ya leo, tunakwenda kubaini baadhi ya makundi ya watu waliojihusisha na shughuli za “kupunga” pepo kama ambavyo tunasoma hapa chini:
Askofu Sylvester Gamanywa

“…Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.” (MDO 19:13)

Hapa tumesoma sehemu ya kisa hiki na kuona wayahudi wenye kutangatanga ambao wanatajwa kuwa “wapunga pepo” ambao waliamua kujiingiza kwenye usanii wa kutaka kutoa pepo kwa mamlaka ya Yesu aliyekuwa akihubiriwa na Paulo. Ni kutokana na msamiati huu wa “wapunga pepo” tunakwenda kutafuta kwanza tafsiri ya maneno haya ya “kutoa” pepo na “kupunga” pepo:

 

 Tafsiri ya misamiati ya “kutoa” na “kupunga” pepo


Kwa lugha ya kiyunani lilitumika kuhusu neno hili “kutoa” ni ekballō na linapatikana katika Injili ya Marko 16:17 ambayo inasomena hivi: “Na Ishara hizi zitafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo…..” (Mk.16:17)

Neno ekballo lilimaanisha “kukemea”, “kuondosha kwa nguvu” na “kufukuza”. Aidha, neno ekballo kwa lugha ya kiingereza limetafsiriwa kuwa ni “to lead one forth or away somewhere with a force which he cannot resist” likiwa na maana ya “kumwondoa mtu kwa lazima; au kumtoa kwa mamlaka ambayo hawezi kushindana/kupingana nayo”

Msamiati wetu wa pili ni neno “kupunga” ambalo neno la kiyunani lililotumika katika maandiko ni exorkistēs . Neno hili tunalikuta katika maandiko ya Kitabu cha Matendo ya Mitume 19:13 yanayosomeka hivi: “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu wakisema, nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.” (Mdo.13)
Neno hili exorkiates kwa kiingereza lilitafsiriwa kuwa ni: “one who employs a formula of conjuration for expelling demons” Tafsiri ya neno la Kiingereza lililotumika limetafsiriwa kuwa ni: “act or process of invoking supernatural aid by the use of magic forms; the practise of magic arts”

Tafsiri ya jumla ya maneno ya Kiingereza yenye kutafsiri neno Exorkistes inaweza kutafsiriwa kuwa ni: “mchakato wa kuwasiliana na pepo kwa kanuni za kipepo ili kuwasihi pepo waondoke kwa masharti yao

Majumuisho ya tafsiri ya misamiati
Misamiati ya maneno “kutoa” na “kupunga” pepo yamenukuliwa kutoka kwenye maandiko ya Injili ya Marko na Kitabu cha Matendo ya Mitume Lugha ya kiyunani imetupa maneno yaliyotofautiana ambayo “kutoa” ni ekballo ambalo maana yake ni kukemea, kufukuza kwa mamlaka ambayo anayefukuzwa hawezi kubisha wala kupingana nayo. Aidha neno “kupunga” ambalo ni exorkistes ambalo maana yake ni mchakato wa kuhojiana na kuwasiliana na pepo ili kujua matakwa yao na kuwabembeleza waache usumbufu baada ya kutii maelekezo ya pepo

Huduma za “kutoa pepo” kwa “mtindo” wa “kupunga pepo”

Baada ya kupitia tafsiri ya misamiati ya kutoa na kupunga pepo, hebu sasa turejee kwenye mada yetu ya msingi katika makala ya leo. Turejee kwenye uchambuzi wa chanzo au chimbuko la kuongezeka hofu ya uchawi ambayo imeanza kukithiri katika makanisa yetu siku hizi.

Uchunguzi wangu wa historia ya Biblia na thelojia ya maandiko, nimegundua kwamba, kuna mchanganyo mkubwa wa matumizi ya misamiati yenye maana tofauti katika tukio moja. Ndiyo hii nimeitafsiri kuwa ni “huduma za kutoa pepo kwa mtundo wa kupunga pepo”!

Ni maana ya “kutoa pepo” kwa mtindo wa “kupunga pepo”? Jibu la swali hili naweza kulitolea maelezo katika sehemu mbili kuu zifuatazo:

 

Kuchanganya vyanzo tofauti vya mamlaka ya kushughulika na mapepo

 

Tumesoma kwamba Yesu Kristo yeye aliwapa wanafunzi wake “mamlaka” ya “kukemea” na “kufukuza pepo” pasipo ubembelezi kutoka kwa mkemeaji pepo. Lakini pia tumesoma kisa cha kikundi cha “wapunga pepo” yaani “waganga wa tunguri” waliojaribu “kuteka nyara” mamlaka ya “kutoa pepo” ili waitumie kwa maslahi yao binafsi. Bila shaka hii ilitokana na Mtume Paulo aliyetumiwa na Mungu katika huduma ya kufukuza pepo kiasi ambacho “wapunga pepo” nao walitaka kuipata mamlaka hiyo kupitia mgongo wa jina la Paulo.

Hawa “wapunga pepo” hawakujua kwamba hizi ni mamlaka mbili tofauti ambavyo vyanzo vyake ni viwili tofauti na kamwe haviwezi kufanya kazi moja wala kufanya kazi pamoja. Ukweli huu ulithibitika pale ambapo “wapunga pepo” walihojiwa na majini waziwazi:

“Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na Yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.” (Mdo.19:15-16)


Mchezo huu wa kutaka wa “wapunga pepo” kutamani kutumia “mamlaka ya Mungu ya kutoa pepo” ndio uliowaponza hata wakashambuliwa na pepo mchafu.

 Kutumia mtindo wa “wapunga pepo” kwa madai ya “kutoa pepo”


Kinachoendelea ndani ya baadhi ya huduma za maombezi na makanisa yanayotoa “huduma za ukombozi” ni kile ninachokiona kuwa ni kuingiliwa na baadhi ya “watumishi” ambao tena wamejiingiza kwa siri katika huduma kikanisa lakini ukweli hawajatumwa na Mungu mwenyewe kufanya huduma hizo.

Na kwa kuwa hawajatumwa na Mungu kufanya huduma za maombezi, wanajikuta hawana “mamlaka” (Dunamis) kutoka kwa Mungu ya kutoa, au kufukuza pepo wakawatoka watu. Badala yake wanalazimika kukariri na kuigiza misamiati ya “kutoa pepo” inayotumiwa na watumishi wa kweli wa Mungu; ili nao wasikike na kufanana fanana na huduma za kweli za kutoa pepo. Lakini ukichunguza mitindo wanayotumia katika mchakato mzima wa kutoa pepo, utashangazwa kubaini mawasiliano yaliyopo sio “kutoa” pepo bali ni “kupunga” pepo!




Lakini lazima tukubali kwamba, huduma ya kutoa pepo ni nyeti, na yenye kuhitaji uzoefu wa kiimani uliojaa maarifa ya Neno la Mungu. Vinginevyo, ni rahisi sana huduma ya kutoa pepo kuingiliwa na “imani potofu” ambayo badala ya kutoa pepo kweli kama ilivyoagizwa katika maandiko; yakafanyika mambo mengine ambayo ni sawa na “kupunga pepo” sawa na waganga wa tunguri.

Kana kwamba hii haitoshi, ziko “huduma bandia” zinazojihusisha na misamiati ya “kutoa pepo” kama upentekoste unavyofanya; lakini zenyewe zinaendeshwa kwa mbinu za ushirikina na uchawi wa kawaida; lakini kwa kutumia mwavuli wa dini. “huduma bandia” za jinsi hii huendesha maombezi kwa vituko na mbwembwe za kimazingaombwe ambapo maelfu ya watu huvutiwa na kushangazwa kwa viini macho; lakini hakuna uponyaji wa kweli wala utendaji halisi wa Roho Mtakatifu katika huduma hizo.

Kihistoria katika huduma za kikanisa, kila wakati ambapo karama za kweli za kutoa pepo zilikuwa zikifanyika na watu kufunguliwa katika nguvu za giza; Ibilisi mwenyewe katika kujihami dhidi ya mashambulizi yanayotupwa kinyume chake naye hujaribu kupenyeza baadhi ya sera na mbinu zake kwa siri kwa wenye kufanya huduma za kutoa pepo akiwashawishi wazifuate na hasa wakati wanapowasiliana na pepo ndani ya watu.

Dalili za “kupunga pepo” badala ya “kutoa pepo” na changamoto zake

Baadhi ya mambo ambayo ni dalili za “kupunga pepo” badala ya “kutoa pepo” ni pamoja na mchakato mzima wa mahojiano kati ya “mtoa pepo” anapowasiliana na pepo ndani ya mtu huku akitaka kuambiwa na mapepo hayo ni kwanini walimwingia mhusika?; na kwa kutumwa na nani?; na nini kifanyike ili yapate kumtoka mhusika!

Kuwauliza mapepo maswali kama chanzo taarifa kama mwongozo watu kufunguliwa kuna changamoto zake kama ifuatavyo:

1. Kuambiwa na kuamini taarifa za uongo


2. Kufanyia kazi taarifa za uongo mapepo ambazo hugeuka kikwazo cha watu kufunguliwa kwa sababu "shetani hawezi kujifitini mwenyewe"

3. Taarifa za uongo wa mapepo kutumiwa katika kuchonganisha na kufutinisha waathirika wa taarifa husika na kusababisha mifarakano na migogoro


Na hii ndiyo mojawapo ya sababu za kuongezeka kwa hofu ya uchawi makanisani kwa kuwa wameaminishwa taarifa za uongo kutoka kwa pepo na zikaaminiwa na "watoa+wapunga" makanisani

Chanzo kingine ambacho kimechangia kuongezeka kwa hofu ya uchawi makanisani ni uongozi wa kanisa kutukuza sana shuhuda za baadhi ya watu wanaodai kuokoka kutokana na vitendo ya uchawi na kisha kuanza kusimulia historia zao za kichawi wakielezea jinsi walivyokuwa wamebobea katika mambo ya uchawi.

Ninajua kwamba si makosa kwa mtu aliyetubu na kuacha mambo ya uchawi anaposhuhudia mabadiliko aliyopata ndani ya wokovu. Lakini ni makosa makubwa ikiwa masimulizi ya shuhuda za kichawi yataegemea zaidi kwenye mambo mabaya ya kichawi aliyofanya, mpaka kutaja majina ya watu aliowafanyia uchawi nk! Kimsingi, shuhuda za jinsi hii zinatakiwa kuishia kwenye ngazi za ushauri binafsi katika watumishi na muhusika mwenyewe

Pale inapolazimika muhusika kushuhudia huko baadaye, ni lazima kwamba awe tayari amefundishwa na kujaa neno la Kristo na kusimama imara katika imani, ili ushuhuda wake uwe umejengwa kwenye neno la Mungu badala ya historia kavukavu za maisha ya kichawi

Kwa bahati mbaya siku hizi; hususan tangu enzi za akina Emmanuel Eni kuchapisha na Kusambaza vitabu vinavyosimuliwa maisha yao ya uchawi na kuyafanya kuwa fundisho la imani ktk huduma za maombezi na huduma za kikanisa. Huu ulikuwa ndio mlango wa hofu za uchawi kuingia makanisani! Watu wakaanza kuangaliana na kutazamana kushukiana kuwa ni “mawakala wa shetani” !
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment