Writen by
sadataley
12:00 PM
-
0
Comments
Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo
kujenga dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi
hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na
Serikali.PICHA|MAKTABA
Na Peter Elias, Mwananchi
Dar es Salaam. Ongezeko la kasi ya ujangili
nchini limedaiwa kusababishwa na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya
madaraka na mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria katika Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopewa jina la
Urasimishaji wa Ujangili wa Kitaalamu Afrika, tangu mwaka 2000 wizara
hiyo imejikuta katika kashfa za rushwa na kusababisha mawaziri na
watendaji wakuu kuvuliwa nyadhifa zao.
Katika ripoti hiyo, Taasisi ya Kimarekani ya
Utunzaji Wanyamapori ya Born Free USA kwa ushirikiano na Shirika la
Ripoti za Kichambuzi na Takwimu la C4ADS, imeeleza pia jinsi vikundi vya
waasi barani Afrika wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi huu nchini Kenya,
inaitaja Tanzania kama kitovu cha kusafirisha pembe za ndovu katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam imekuwa
ikishindana na ile ya Mombasa katika kutumia bandari kibiashara.
Kutoka mwaka 2008 mpaka 2013, inaelezwa zaidi ya
tani 20 za pembe za ndovu ama zilikamatwa zikisafirishwa kuingia au
kutolewa katika Jiji la Dar es Salaam, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya
Taasisi ya C4ADS.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa uchunguzi wa vinasaba
(DNA), katika tani 11 za pembe za ndovu zilizokamatwa Taiwan, Japan na
Hong Kong mwaka 2006, ilibainika kuwa pembe 1,500 zilitoka Tanzania
(Selous).
Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe
hizo vilifanana, hivyo kujenga dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa
wakiwinda katika hifadhi hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu
unaotambuliwa na Serikali.
“Kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa uwindaji
halali na wawindaji wenye vibali hawasimamiwi ipasavyo kufanya uwindaji
kwa taratibu zilizowekwa kisheria. Hivyo hutumia nafasi hiyo kufanya
vitendo vya ujangili,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Serikali yakanusha
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Paul
Sarakikya alikanusha madai hayo akisema siyo kweli kwamba wawindaji
halali huachwa bila usimamizi, bali wana mifumo ya kusimamia shughuli
hiyo.
“Sikubaliani na ripoti hiyo, tumeshaongea sana juu
ya suala hili, Rais alishalizungumzia na waziri pia. Ufafanuzi ndio
huo, hamna ukweli wowote katika ripoti hiyo,” alisisitiza Sarakikya.
Salakikya alisema idadi ya tembo nchini inazidi kuongezeka katika hifadhi tofauti na upungufu unaoelezwa katika ripoti hiyo.
Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kama hakuna usimamizi madhubuti
katika uwindaji halali, wamewezaje kusimamia uwindaji miaka yote mpaka
idadi ya tembo inaongezeka, baada ya upungufu uliokuwepo miaka ya nyuma.
Wakati Sarakikya akisema tembo wanaongezeka,
ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi ya tembo katika hifadhi za Selous na
Mikumi kwa mwaka 1976, ilikuwa ni 109,419 lakini kufikia mwaka 2009,
idadi hiyo ilishuka hadi kufikia tembo 38,975.
Nchi zilizoathirika zaidi na ujangili barani
Afrika, zinatajwa kuwa ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Cameroon, Msumbiji, Kenya, Zimbabwe na
Tanzania ambayo pia inatajwa kuwa kitovu cha usafirishaji wa pembe za
ndovu.
Idadi ya tembo waliosalia
Na kwa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Frankfurt
Zoological Society mwishoni mwa mwaka 2013, ripoti hiyo inaeleza kuwa ni
tembo 13,084 wanaokadiriwa kusalia katika hifadhi, sawa na upungufu wa
asilimia 66 katika kipindi cha miaka minne tangu 2009.
Hii imefafanuliwa kuwa zaidi ya tembo 25,000
waliuawa katika Hifadhi ya Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia,
ripoti hiyo inabainisha upungufu wa tembo katika hifadhi ya Ruaha-Rungwa
kutoka tembo 35,461 mpaka tembo 20,090 sawa na upungufu wa asilimia
36.5 kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa.
No comments
Post a Comment