Writen by
sadataley
3:43 PM
-
0
Comments

Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi
nchini mwaka 1992, hali ya kisiasa imekuwa ni ya mvurugano. Watawala,
CCM wamekuwa wakilinda nafasi yao ili isichukuliwe na wapinzani.
Mfumo wa chama kimoja uliwaaminisha watu kwamba
CCM ndicho chama pekee kinachostahili kutawala na watu waliamini. Hivyo
kimantiki ujio wa vyama vingi ulikuwa ni vita.
“Siasa siyo harusi, wala sherehe, siasa ni vita na
siasa inahusu kutawala na madaraka yananoga. Hakuna anayependa kuachia
kirahisi,” alisema mwanasiasa mmoja wa Kenya katika kipindi cha kampeni
za uchaguzi mkuu mwaka 2007.
Kiuhalisia, inaonekana wazi kwamba CCM walilazimishwa au kushinikizwa kukubali mfumo wa vyama vingi.
Tangu hapo siasa za Tanzania hazijatulia hadi
tunafikia leo muda wa kujaribu kuandika Katiba mpya. Vita hiyo bado
imeingizwa huko kiasi cha kutia shaka kwa wananchi kama kweli tutapata
katiba bora au bora katiba.
Pia muda wote huu vita hii ilikuwa baina ya
serikali ya CCM, yaani chama tawala na wapinzani wao hasa wale
wanaounda chama kikuu cha Upinzani; mwanzoni walikuwa NCCR-Mageuzi,
wakaja CUF na sasa Chadema.
Wapinzani nao wamekuwa na mbinu za jinsi za kuendesha siasa zao pamoja na kwamba chama tawala kinajaribu kuwabana kila kona.
Hata hivyo pamoja na upinzani kubanwa na vyombo
vya dola, Tume ya Uchaguzi pamoja na Serikali, bado upinzani unaendelea
kukua kwa kiwango kikubwa.
Kuna baadhi ya mikoa kama Arusha, Mbeya, Mwanza,
Mara, Kagera na hata Iringa na Ruvuma upinzani unasonga mbele hata kama
ni kwa kupitia mateso, dhuluma na pengine hata kupoteza maisha.
Kama tunapenda kuambiana ukweli lazima tuseme wazi kwamba kwa sasa Watanzania hawadanganyiki katika mambo mengi.
Siasa za Tanzania zimekuwa na dosari nyingi hata
kama chama tawala hakitaweza kukubali. Muda wote kumeonekana wazi kuwa
hali halisi ni ya vita kati ya serikali ya CCM na upinzani.
Hata hivyo, jinsi siku zinavyopita na hasa katika
zoezi la kuandika Katiba mpya kupitia mijadala ya Bunge la Katiba
lililoahirishwa, vita hii inaonekana kuhama. Imehamia kwa nani?
Kwa mtu mwenye kupenda kutafiti nini kinaendelea katika nchi
yetu atagundua kwamba vita ya kisiasa imehama kutoka kwa serikali ya CCM
na kuhamia kwa wananchi na siyo tena wapinzani.
Hili limefanyika bila serikali ya CCM kufahamu kana kwamba Mungu ndiye alifanya jambo hili bila mtu kufahamu.
Hata hivyo, kilichotokea ni kwamba inaonekana wazi
wananchi wengi wamechoshwa na siasa za chama tawala, siasa za
kuahidiahidi kila wakati, lakini vitendo ni kidogo.
Pia ukweli ni kwamba ukisoma alama za nyakati
utagundua kwamba, nyakati hizi ni nyakati za mabadiliko duniani.
Tanzania siyo kisiwa na hivi nayo imekumbwa na mkondo huu wa mabadiliko
itake isitake huu ndiyo ukweli.
Mabadiliko si wingi wa serikali
Mabadiliko hayo hayategemei serikali moja, mbili,
tatu, saba wala kumi. Hii siyo hoja ya msingi. Naona hilo ni jambo la
msingi kwa chama tawala kulifahamu na wala siyo kitu cha kubeza.
Watanzania wa leo si wa jana, wala juzi, wala wa mwaka l968.
Ukweli mwingine ambao umesaidia kuhamishia vita
hii kwa wananchi badala ya kuendelea kubaki kwa wapinzani ni kwa sababu
wapinzani wanaonekana kutetea masilahi ya umma (taifa au watu wote
bila kujali itikadi za kisiasa, dini, kabila, wala rangi).
Kinyume chake ni kwamba kila wakati CCM
wanaonekana kutetea masilahi ya chama chao, ili kuendeleaa kuwepo
madarakani kwa kutumia mbinu mbalimbali hata kama ni dhalimu.
Mfano ni mjadala wa Rasimu ya Pili ya Katiba mpya
ambayo imesheheni maoni, mawazo na matashi ya wananchi na ambayo ndiyo
msingi wa katiba yetu, lakini CCM wameamua kujaribu kupenyeza mawazo ya
chama chao. Je, kwa mantiki hii wananchi watampenda nani?
Siyo hili pekee. Hata taasisi kama vile taasisi za
dini, mathalan maaskofu wa Kanisa Katoliki katika umoja wao, wametoa
ujumbe unaowataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu mawazo na maoni ya
wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Je, viongozi wakuu kama hao kwa nini waje na
ujumbe kama huu, wakati wa mvurugano kama huu? Serikali ya CCM
imejiuliza vya kutosha maana yake ni nini?
Pia tumeona Taasisi ya Kiislamu nayo imekuja na tamko kama hilo na hivi kuungana pamoja na maaskofu.
Dini kuu mbili nchini kama zinakuja na wazo moja maana yake ni
nini? Lakini, pia kuna taasisi nyingine kama Chama cha Walimu (CWT),
Tanzania, Tucta, na wengineo, wote wanatetea mabadiliko yaliyoletwa na
rasimu ya Tume ya Warioba.
Hivi sasa wale wanaofikiri kwamba kumshambulia,
kumdhalilisha na kumtukana Warioba ni mbinu yao ya kuudhoofisha mawazo
ya wananchi, basi wajue wanajisumbua.
Mwalimu Nyerere alitufundisha mambo mengi, lakini moja la msingi ninalolikumbuka ni “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.”
Wana CCM nchini ni zaidi ya milioni nane, na hivi wao si wengi kuzidi wananchi wanaobaki.
Kwa mantiki hii kama wananchi wanataka mabadiliko,
basi yatapatikana tu. Mtazamo mwingine ni huu kwamba wananchi
wameanza kugundua kwamba Watanzania wanaishi katika dunia inayobadilika.
Msimamo wa Ukawa
Kususia vikao kulikofanywa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni alama nzuri ya kujua nini kinaendelea katika bunge hilo.
Hatua yao ilikuwa ni kupinga kuwa sehemu ya
kuwasindikiza wajumbe wa CCM katika kile wanachokiita kusimamia msimamo
wao wa kubadilisha rasimu ya katiba yenye muundo wa serikali tatu na
kuchomeka ile ya serikali mbili ambayo ni msimamo wa chama tawala.
Ni vyema kwa chama tawala kutambua kuwa
kuishinikiza Katiba kwa nguvu hakuleti maana yeyote ile kwa sababu
wananchi wenye Katiba ndiyo mwishowe watakaokuwa na uamuzi wa kuikubali
au kuikataa katika sanduku la kura ya maoni.
Nakumbuka nchini Kenya kuna rasimu ilikataliwa na
wananchi kwa sababu chama tawala, KANU wakati ule kilikuwa kimepenyeza
sera zake ili kiweze kuendelea kutawala na kukandamiza wananchi.
Wakati ule Wakenya walikuwa amechoshwa na vitendo
vya KANU vya rushwa, unyanyasaji wa wananchi wa kawaida, kupendeleana,
kubebana, vyombo vya dola kuua raia hovyo hasa wakosoaji wa serikali,
kuua viongozi wa dini, ubambikizaji wa kesi na kadhalika.
Rasimu hiyo ya Kenya ilikataliwa kwa sababu vita ya serikali ilikuwa imehamia kwa wananchi na siyo kubakia kwa wapinzani.
CCM na propaganda
Kitu kingine ambacho kimehamisha vita hii ya
serikali ya CCM na kwenda kwa wananchi ni kutokana na propaganda
(porojo) zinavyotumiwa na wahusika.
Wengi wameanza kuelewa propaganda, yaani kusema uongo unaolingana na ukwei na hivi kuweza kuwashawishi watu wawe upande wako.
Kila wakati nchi yetu inapokuwa na tukio la
kuashiria mabadiliko katika serikali au chama, mfano uchaguzi mkuu, kwa
kawaida propaganda hutumika sana.
Mfano, wakati wa uchaguzi iliibuka porojo kwamba
CUF walikuwa wameleta majambia ya kutumika katika uchaguzi na kule
Igunga ilisemekana Chadema walikuwa wamekodi Mungiki kutoka Kenya.
Hii propaganda ilitumika kuwaharibia wapinzani
kwamba hawafai kuchukua nchi. Propaganda nyingine ni ile ya kusema
kwamba mkichagua wapinzani nchi itaingia katika vita kama Rwanda ama
Burundi.
Hivi karibuni, Waziri William Lukuvi alitumia
propaganda alipokaribishwa kutoa hotuba katika sherehe za kumsimika
askofu kanisani mjini Dodoma.
Alisema: “Kama tutapitisha serikali tatu, basi
huenda Serikali haitakuwa na fedha ya kuwalipa wanajeshi wetu na hivyo
kusababisha kuipindua Serikali na hivyo kusababisha maasi ambayo
yatapelekea makanisa kufungwa.”
Huku ni kuwatisha ili watu wakati wa kura za maoni
waipigie kura ya ndiyo Katiba itakayopendekeza serikali mbili hata kama
mbaya. Tumshukuru Mungu ameiweka propaganda hii hadharani ili watu
wapate kuijua.
Hiyo ni lazima ifike mahali siku moja wananchi waamke kutoka usingizini na kushagaa kujiuliza: “Jamani tupo wapi’?”
*Baptist Mapunda ni mtaalamu wa mawasiliano Frmapunda91@gmail.com
No comments
Post a Comment