Writen by
sadataley
1:15 PM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Bunge jana liligeuka uwanja wa kurushiana makombora pale
wabunge walipoumbuana kuhusu baadhi yao kudaiwa kuwa ombaomba katika
Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF).
Kuumbuana huko kuliegemea taarifa ya Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kuwalipua baadhi ya mawaziri na
wabunge kwa kuchota fedha katika mfuko huo.
Sakata hilo lilienda mbali zaidi baada ya Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe kulipuliwa kuwa anadaiwa
zaidi ya Sh1 bilioni na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na
tayari kuna hati ya kumkamata.
Hata hivyo, Mbowe alipoulizwa jana ofisini kwake
bungeni alisema: “...Sina taarifa yoyote ya kukamatwa. Nipo hapa bungeni
mbona sijakamatwa? Muulizeni aliyesema awaeleze imetolewa lini na
nani,” alisema Mbowe.
Wabunge hao walianza kuumbuana baada ya Mbunge wa
Mbinga Magharibi (CCM), John Komba kutaka mwongozo wa Spika, akidai
Lissu alimtaja kuwa naye ni miongoni mwa wabunge waliochota fedha LAPF.
“Kati ya wabunge hao wanaofilisi mashirika ya
umma, mimi sikumbuki wala sijui LAPF iko wapi wala ofisini kwa
mkurugenzi wake wala kwa mfanyakazi wake na sijachukua fedha yoyote
LAPF,” alisema.
Akionyesha kukerwa, Komba alisema anachokumbuka
Mfuko wa Maendeleo wa Nyanza ambao ni wadau wa LAPF waliomba msaada wa
kununua boti na walipewa Sh1.5 milioni... “Leo Lissu amekuja hapa
anawadanganya watu kuwa mimi nimehusika kutoa mapesa LAPF, sijui huu ni
wendawazimu ama nini?... Hizi ni siasa za majitaka kabisa naomba
mwongozo wako.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alijibu hoja hiyo akisema wabunge
kuomba katika mashirika hayo si jambo la ajabu na kwamba yeye mwenyewe
aliomba kwa barua.
“Nilitaka kusema jambo hili si kubwa kiasi hiki kwa sababu fedha hizi zipo kwa ajili ya maendeleo...”
Hata hivyo, Lissu alipopewa fursa ya kujibu
alipigilia msumari akisema wabunge ndio wenye jukumu la kusimamia mifuko
hiyo na kwamba kama wanachukua fedha za mifuko hiyo wanaingia moja kwa
moja katika mgongano wa kimasilahi.
Aidha, alisema LAPF kwenye fungu hilo la msaada
kwa jamii inatoa kwa wabunge wa CCM pekee yake... “Kwa sababu wabunge
waliopewa fedha na nyaraka zake zipo ni hao wanaopiga kelele kina Pindi
Chana, Mwigulu Nchemba, wanaochukua fedha ni wa CCM tu.”
Alihoji kutumika kwa fedha za LAPF kununua jezi katika Jimbo la Chato linaloongozwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kuomba-fedha-LAPF--Wabunge-waumbuana/-/1597296/2327702/-/musv5z/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kuomba-fedha-LAPF--Wabunge-waumbuana/-/1597296/2327702/-/musv5z/-/index.html
No comments
Post a Comment