Writen by
sadataley
1:19 PM
-
0
Comments
Na Lilian Lucas, Mwananchi
Morogoro. Hali ya mtoto Nasra Rashid (4) aliyekuwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka minne, imebadilika ghafla juzi na jana kuwalazimu madaktari kumweka katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rita
Lyamuya alisema jana kuwa tatizo kubwa la mtoto huyo ni kubadilika
ghafla kwa upumuaji wake na utaratibu unafanyika ili leo asafirishwe
kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
“Tunatarajia kumpeleka Muhimbili mapema asubuhi kwa gari maalumu la wagonjwa ili kupata matibabu zaidi,” alisema Dk Lyamuya.
Alisema juzi Nasra alikuwa mwenye furaha na mchangamfu lakini jioni yake hali ilibadilika katika mfumo wake wa kupumua.
Alisema kwa msingi huo, uongozi wa hospitali ya
mkoa umeamua kumsafirisha kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Uchunguzi wa awali wa afya ya Nasra ulibaini kuwa
mtoto huyo alikuwa na maradhi ya nimonia (kichomi), mifupa ya miguu na
mikono kuvunjika pamoja na utapiamlo.
Watuhumiwa kortini
Katika hatua nyingine, watu watatu akiwamo baba
mzazi wa Nasra, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro
kujibu mashtaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Baba wa mtoto huyo Rashid Mvungi (47), mama mlezi
wa Nasra, Mariamu Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30), walifikishwa
mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo jana na kusomewa mashtaka
hayo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alidai kuwa
washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Desemba, 2010 na Mei mwaka huu
katika eneo la Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Alidai kuwa katika kipindi hicho walimfanyia
ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na hivyo
kumsababishia magonjwa.
Alitaja maradhi yaliyomkumba akiwa ndani ya boksi ni utapiamlo, kichomi na mvunjiko wa mifupa.
Hyera alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama kutaja tarehe ya kuisikiliza.
Mahakama ilitoa masharti ya dhamana kwa kila
mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh5 milioni
kila mmoja na barua kutoka kwa waajiri wa kuaminika au Serikali za
Mitaa.
Hata hivyo, walishindwa kutimiza masharti hayo na
kurejeshwa rumande. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9, mwaka huu
itakapotajwa tena.
No comments
Post a Comment